Tuesday, December 29, 2015

WAZIRI MBARAWA AANZA KAZI RASMI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akipata ufafanuzi kuhusu namna ya kuhifadhi makontena kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce Matei (kushoto), mara baada ya kukagua Mamlaka hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce Matei (wa tatu kushoto), huku Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Eng. Edwin Ngonyani (wa pili kulia), akifatilia.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa na Naibu wake wakikagua mtambo wa kuchunguza makontena (scanner) katika eneo la TPA.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua mtambo wa madai na malipo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania alipotembelea Mamlaka hiyo leo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya kazi kwa uadilifu na uharaka wenye tija ili kukudhi matarajio ya wananchi katika wizara hiyo.

Akizungumza na watumishi wa wizara hiyo mara baada ya kuapishwa, Profesa Mbarawa amesema kipaumbele chake kwa wafanyakazi hao ni kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia matokeo chanya kwa haraka.

 “Tuwe tayari kubadilika, tufanye kazi ya kuwahudumia watanzania kwa moyo, tuendeleze taswira nzuri ya Wizara kwani Wizara hii ina sifa nzuri tangu ilipoanza hadi sasa’, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa amefafanua kuwa uwazi na uhusiano mzuri kwa wafanyakazi ni ngao kubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo kati ya watendaji na watumishi. 

Aidha, amewataka watendaji na watumishi wa Wizara hiyo  kushirikiana na kutokuwa wanyonge kutokana na mfumo wa mabadiliko ya kiutendaji wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwani Wizara hizo zina uhusiano mkubwa katika kumhudumia mwananchi hivyo kuungana kwake kutaleta tija na ufanisi kwa haraka.

 “Jambo la msingi ni kufuata kanuni na sheria katika utendaji wenu pamoja na kusimamia miongozo iliyopo, utendaji wenu lazima uwe na malengo yanayotekelezeka kwa haraka”, amesema Prof. Mbarawa.

Akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Waziri huyo amehimiza matumizi ya teknolojia katika huduma za bandari ili kuweza kuwahudumia wateja kwa haraka hata wakiwa mbali.
Amewataka watumishi wa bandari kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa ushindani ili kuvutia wadau wengi kupitisha mizigo yao katika bandari za Tanzania.

“Fanyeni kazi kwa maslahi ya nchi, acheni kufanya kazi kwa maslahi binafsi, tambueni Serikali na wananchi wanahitaji huduma bora zitakazokuza uchumi wa taifa kutoka katika bandari zenu”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Eng. Edwin Ngonyani amewataka watumishi wa bandari kuacha tamaa, kuishi kwa uaminifu ili kujenga taswira mpya ya taasisi hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa taifa na jamii kwa ujumla.

Katika ziara hiyo Waziri Mbarawa na Naibu Waziri Ngonyani waliambatana na viongozi mbalimbali wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: