Sunday, December 20, 2015

DKT. HAMISI KIGWANGALLA KUWAKUTA MADAKTARI WA ZAMU KATIKA HOSPITALI YA MKOA WA LINDI

kigw1
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo Kasanga akimkaribisha Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla alipotembelea wodi za hospitali hiyo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya leo mkoa wa Lindi.Katikati ni Mganga wa Meno na Kinywa katika hospitali hiyo, Dkt. Hussein Athumani.
………………………………………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla amefanya ziara ya kushtukiza mwishoni mwa katika hospitali za Rufaa za Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kujifunza namna wanavyofanya kazi ili Serikali iweze kuboresha na kutoa wa huduma bora za afya nchini.
Akifanya majumuisho ya ziara hiyo Dkt. Kigwangalla amesema kuwa amefurahishwa na namna hospitali hizo zinavyofanyakazi ya kuwahudumia wananchi ya kuhakikisha wanapata tiba ya uhakika katika masuala ya afya.
“Nimefurahishwa na namna Hospilali ya Rufaa ya Sokoine ya mkoa wa Lindi wanavyofanyakazi wanavyotoa huduma, kila ofisi niliyofika madaktari walikuwepo na wanafanyakazi” alisema Dkt. Kigwangalla.
Licha ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo, Dkt. Kigwangalla alisema kuwa amefurahishwa na kitendo cha kuwakuta madaktari wa zamu na watoa huduma wote wapo katika maeneo yao ya kazi katika hospitali ya Sokoine Lindi mkoani na Ligula ya Mtwara kitu ambacho kinawapa faraja wagonjwa pamoja na jamaa zao wanaohitaji kupata huduma za afya ikiwemo huduma ya dharura anayohitaji kupewa mgonjwa kulingana na tatizo lake.
“Ziara tunazozifanya katika hospiltali za rufaa, mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati, lengo letu ni kujifunza namna zinavyotoa huduma za afya kwa wananchi wetu ili baadaye kuona ni maboresho gani yafanyike na hatimaye kutoa huduma bora zenye tija na kwa wakati kwa wananchi” alisema Dkt. Kigwangalla.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kigwangalla ameziagiza hospitali zote za mikoa nchini kote waige kutoka mkoa wa Lindi namna hospitali hiyo inavyotoa huduma kwa haraka na kwa wakati kwa kutumia mfumo wa kielekroniki kuanzia mgonjwa anapopokelewa chumba cha mapokezi hadi anapomaliza kupata huduma na kuruhusiwa.
Faida ya kutumia mfumo huo wa kielekroniki ni pamoja na kuongeza makusanyo kupitia kwa wagonjwa wanaotumia huduma ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wale wanajilipia wenyewe, makusanyo yanayopatikana yanatumika kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo kununua dawa na vifaa tiba kwa wakati, kutoa motisha kwa wafanyakazi pamoja na kupunguza urasimu usiowa lazima kwa wagonjwa.
Licha ya mafanikio hayo katika hospitali za rufaa za mikoa ya Lindi na Mtwara, hospitali hizo zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa ambapo hadi sasa Hospitali ya Sokoine ina Daktari Bingwa mmoja na Hospitali ya Ligula mkoani Mtwara ina madaktari Bingwa wawili licha ya ukubwa wa mikoa hiyo pamoja na kuhudumia wagonjwa kutoka nchi jirani ya Msumbiji.
Katika kutatua changamoto hiyo, Dkt. Kigwangalla amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa (RAS) yote kuandaa vyumba vya kufanyia upasuaji pamoja na vifaa tiba na kuandaa nyumba watakapokaa madaktari bingwa ambapo ameahidi Serikali itaanza kuwapangia vituo madaktari hao kwa kuanzia na mikoa ambayo imejipanga ili waanze kutoa huduma mara moja.
Akizungumzia namna walivyofanikiwa kutoa huduma bora, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sokoine ya mkoa wa Lindi Dkt. Evaristo Kasanga alisema kuwa wameboresha namna ya kukusanya mapato hospitalini hapo kwa kufunga mashine za kielekroniki zinazopelekea wakusanye sh.milioni 24 kwa mwezi tofauti na hali livyokuwa hapo awali ambapo zilikuwa zinakusanywa chini ya sh.milioni 10 kwa wateja wanaotumia mfuko wa bima ya afya.
Mafanikio ya Hospitali ya Rufaa ya Sokoine ya mkoa wa Lindi yamejengwa juu ya falsafa yao inayosema “Sisi watumishi wa Sokoine tunaamini kwamba monjwa ndiye tajiri yetu, tunaahidi kuwa tutatoa huduma bora kwa wagonjwa wetu bila ubaguzi, hatupokei wala kutoa rushwa”.
Kwa upande wa makusanyo ya kawaida, Dkt. Kasanga alisema kuwa yamefikia sh.milioni 40 pesa tasilimu ikilinganishwa na hali livyokuwa hapo awali ambapo zilikusanywa chini ya sh.milioni 8 kwa mwezi.
“Hatua hiyo imesaidia kuboresha utoaji wetu wa huduma kwa kuanzia na usafi wa mazingira, mifumo ya kisasa ya mawasiliano ndani ya hospitali ili kurahisisha mawasiliano kati ya wagonjwa na wafanyakazi, wagonjwa kwa wagonjwa, wafanyakazi kwa wafanyakazi pamoja na masuala yote ya dharura kama daktari anahitajika kutoa msaada” Dkt. Kasanga.
 Aidha, Dkt. Kasanga alisema kuwa hospitali hiyo imefanikiwa kuwa mshindi wa pili kwa utoaji wa huduma bora Tanzania kwa mwaka 2015 ambapo wamezawadiwa kikombe cha ushindi wa nafasi hiyo na wamejipanga kuanzia Januari 2016 kuachana na mfumo wa watumishi kusaini kwenye vitabu wanapofika kazini badala yake wataanza kutumia mfumo wa kusaini kwa kuweka alama za vidole kwenye mashine maalum (Biometric) ambayo imefungwa na Shirika la Miradi la Ujerumani la GIZ hatua itakayorahisisha usimamizi wa mahudhurio kazini, kutoa huduma sahihi kwa wagonjwa na kwa wakati.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Daktari wa Kinywa na Meno Hospilali ya Rufaa ya Sokoine ya mkoa wa Lindi Dkt. Hussein Athuman akitoa taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu alisema kuwa hali inaendelea vizuri na idadi ya wagojwa imepungua kwa hatua inayoridhisha.
“Hali ya ugonjwa wa kipindupindu hadi mwishoni mwa wiki ilikuwa ni nzuri na tunaendelea kuisimamia ipasavyo, wilaya ya Kilwa ilikuwa na kesi za wagojwa wapya watatu ambapo mmoja tayari amesharuhusiwa kurudi nyumbani, manispaa ya Lindi kulikuwa na mgonjwa mmoja ambaye naye amesharuhusiwa” alisema Dkt. Hussein.
Ugonjwa wa kipindupindu mkoani Lindi umeathiri wilaya tatu za Manispaa ya Lindi, Kilwa na Lindi Vijijini ambapo wilaya ya Kilwa ndiyo imeathiriwa zaidi kuliko wilaya nyingie kutokana na ukaribu wa wilaya hiyo na mkoa wa Dar es salaam ambapo ugonjwa huo uligundulika mapema mwezi Augosti mwaka huu.
Aidha, Dkt. Hussein alisema kuwa mkoa huo umefanikiwa kusimamia ipasavyo na kuzuia maambukizi ya mapya ya ugonjwa huo yasitokee na kusambaa kwa kufanya usafi mahali pote katika makazi ya watu, hospitali, vituo vya afya na zahanati kama desturi ya mkoa huo wakichagiwa na agizo la kufanya usafi Desemba 9, 2015 la Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Zaidi ya hayo, Dkt. Hussein alisema kuwa waliweka dawa katika visima vyote vya maji hatua ambayo imesaidia kupunguza kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindi mkoani humo.
Kwa niaba ya uongozi, wafanyakazi na wananchi wa mkoa wa Lindi, Dkt. Hussein amewashukuru wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuwaunga mkono kwa kuboresha mazingira ya hospitali ya Sokoine wakiwemo wabunge, washirika wa maendeleo wakiongozwa na  Shirika la Miradi la Ujerumani la Giz kuendelea kuwaunga mkono katika kuwahudumia wananchi.
Post a Comment