Sunday, July 06, 2025

PPAA yatoa rai wazabuni kutumia moduli kuwasilisha rufaa

 





Na Mwandishi wetu, Dar

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa rai kwa wazabuni kutumia Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ili kuokoa muda na gharama zisizo na ulazima.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alipoongea na waandishi wa Habari katika banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Bw. Sando amewasihi wazabuni kuitika wito wa Serikali wa kutumia mfumo wa NeST ambapo ndani ya mfumo huo kuna moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa, hivyo watumie fursa hiyo kuwasilisha malalamiko na rufaa zao.

“Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ni suluhisho kwa wazabuni katika kuwasilisha rufaa pindi wanapokuwa hawajaridhishwa na mchakato wa ununuzi wa umma katika zabuni walizoshiriki,” amesema Bw. Sando 

Bw. Sando aliongeza kuwa baada ya matumizi ya moduli kuanza rasmi mwezi Februari 2025 mzabuni halazimiki kufika ofisi za Mamlaka ya Rufani kuwasilisha rufaa, badala yake atamie moduli kuwasilisha rufaa husika kupitia mfumno wa NeST.

Aidha, Bw. Sando ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 PPAA inatarajia kuanza kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao ili kurahisisha zaidi usikilizaji wa rufaa pale itakapoonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amesema moduli ina faida nyingi hususan kuokoa muda na grahama, imerahisisha upatikanaji wa nyaraka, kutunza kumbukumbu pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Katika kuhakikisha kuwa matumizi ya moduli yanawafikia wazabuni wengi kwa wakati uliokusudiwa, PPAA imeshatoa mafunzo ya namna ya kuwasilisha malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki katika kanda mbalimbali ambapo mpaka sasa Kanda ya Pwani, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati zimepatiwa mafunzo. 

Aidha, katika mafunzo hayo PPAA imefanikiwa kutoa elimu kwa wazabuni 873 na wakuu wa idara/vitengo vya ununuzi na sheria wapatao 1,588 kutoka katika taasisi nunuzi 500.

🌍 KIKUNDI CHA JWTZ CHATINGISHA COMORO KWA KWATA YA KIMYA KIMYA!

 






Moroni, Comoro – Julai 6, 2025

Kwa ustadi wa hali ya juu, kikundi maalum cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kimeonesha umahiri wa kupiga kwata ya kimya kimya wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Comoro yaliyofanyika tarehe 6 Julai 2025, katika Uwanja wa Malouzini, Moroni.

Uhodari na nidhamu ya askari wa JWTZ vimeacha gumzo na kuwavutia maelfu ya watazamaji waliokuwepo kushuhudia tukio hilo la kihistoria. Hii ni ishara ya mshikamano wa kweli, urafiki wa muda mrefu, na heshima ya Tanzania kwa nchi marafiki kama Comoro.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa viongozi wa majeshi ya ulinzi wa Comoro alieleza kuwa Tanzania ni ndugu wa kweli wa kihistoria kwa Comoro, si tu kwa msaada wa ukombozi, bali pia kwa namna inavyoendeleza uhusiano wa kijeshi na kijamii.

Ushiriki wa JWTZ katika maadhimisho haya ni ishara ya msimamo wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha mahusiano ya kimataifa kupitia diplomasia ya kijeshi, mshikamano wa kanda, na utangamano wa Afrika.

@Beit_Salam @PresidenceUnionComores #JWTZ #KwataKimyaKimya #UhuruComoro50 #TanzaniaComoro #DiplomasiaYaKijeshi #AfricaUnited

RAIS SAMIA AHAKIKISHA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MAENDELEO KATI YA TANZANIA NA COMORO





















Comoro, Julai 6, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kidugu kati ya Tanzania na Muungano wa Visiwa vya Comoro. Akiwa nchini humo kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Comoro, Rais Samia amesema uhusiano huo hautaishia kwenye misingi ya kidiplomasia pekee bali utaendelea kwa moyo wa ujamaa, amani, lugha ya Kiswahili, na mshikamano wa kweli wa Kiafrika.

Akihutubia katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni, Rais Samia amesema Tanzania itaendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, mazingira na diplomasia, kama sehemu ya kujenga Afrika imara kupitia urafiki wa kweli na majirani zake.

Rais Samia amekumbusha namna Tanzania ilivyoshiriki harakati za ukombozi kwa nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Comoro, kwa kutoa hifadhi, msaada wa kifedha, kisiasa na kiulinzi kwa wapigania uhuru. Amewataja pia wanawake mashujaa wa Tanzania waliotoa mchango katika ukombozi huo.

Akiwapongeza wananchi na serikali ya Comoro, Rais Samia amesema taifa hilo limepiga hatua kubwa katika sekta ya uchumi, miundombinu, afya, elimu, utalii na huduma za jamii. Amempongeza Rais wa Comoro, Mhe. Azali Assoumani, kwa kuwa kiongozi mwenye maono makubwa katika maendeleo.

Katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, Rais Samia ametangaza mikakati ya kukuza usafiri kati ya Tanzania na Comoro kupitia mashirika ya ndege ya Air Tanzania na Precision Air, pamoja na usafiri wa majini, hatua ambayo inalenga kukuza biashara na muingiliano wa watu wa mataifa haya mawili.

Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro katika kufundisha lugha ya Kiswahili mashuleni, kulinda mazingira ya Bahari ya Hindi, na kuwezesha miradi ya maendeleo kupitia taasisi kama Benki ya Exim, Benki ya Wajasiriamali Vijana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambazo tayari zina mpango wa kupanua huduma zake nchini Comoro.

Kwa kumalizia, Rais Samia ametoa rai kwa wananchi wa Comoro kuenzi uhuru wao kwa kujenga mshikamano, haki na usawa ili kufikia maendeleo jumuishi. Ameahidi kwamba Tanzania itaendelea kuwa bega kwa bega na Comoro katika safari ya maendeleo.

KATIBU MKUU DKT. HASSAN ABBAS APONGEZA TANAPA KWA KUIMARISHA UHIFADHI NA KUTANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA MAONESHO YA SABASABA





Dar es Salaam, 6 Julai 2025

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ametembelea banda la Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Dkt. Abbas amepongeza juhudi na ubunifu unaoonyeshwa na TANAPA katika kutangaza vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji, pamoja na juhudi za kuhamasisha uhifadhi endelevu wa maliasili na wanyamapori wa Taifa. Amesema kuwa muonekano wa banda hilo na umahiri wa maafisa wake katika kutoa elimu kwa wageni ni ishara ya utayari wa taasisi hiyo kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kupitia utalii wa hifadhi.

“Mmenipendeza sana. Banda lenu limekuwa moja ya vivutio vikubwa katika maonesho haya, na muamko wa wadau na wananchi waliotembelea hapa ni wa kutia moyo. Hii ni dalili kwamba kazi yenu ya kuelimisha, kuhifadhi, na kutangaza vivutio vya asili inaungwa mkono na jamii,” alisema Dkt. Abbas.

Aidha, Katibu Mkuu ameeleza kufurahishwa na ushindi wa tuzo saba za kimataifa za utalii ambazo TANAPA imepata katika kipindi kifupi, na kuitaka taasisi hiyo kuendeleza jitihada hizo ili kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kinara wa utalii barani Afrika. Alisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za asili kwa uangalifu mkubwa ili ziweze kuendelea kuchangia uchumi wa Taifa kupitia utalii wa ndani na wa kimataifa.

“Tunapopata tuzo nyingi kama hizi, maana yake ni kwamba dunia inatambua kazi yetu. Lakini pia tuendelee kulinda wanyamapori wetu, mito, misitu na mazingira ya asili – haya ndiyo nguzo za ustawi wa sekta ya utalii na kiuchumi kwa ujumla,” aliongeza Dkt. Abbas.

Banda la TANAPA katika maonesho ya Sabasaba mwaka huu limekuwa kivutio kwa wageni wa rika mbalimbali, likiwa na maonyesho ya video za vivutio, mabango ya kitaalamu, sampuli za mazao ya utalii, na maelezo ya fursa za uwekezaji katika hifadhi mbalimbali nchini.

TANAPA imeeleza kuwa inatumia jukwaa hili kubwa la kibiashara sio tu kutangaza hifadhi zake, bali pia kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na mchango wa sekta ya maliasili katika maendeleo ya Taifa.

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yanaendelea hadi tarehe 13 Julai 2025 yakihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi zaidi ya 3,500, huku yakifanyika chini ya kaulimbiu ya mwaka huu: “Biashara Endelevu kwa Uchumi Shindani”.

RAIS DKT. SAMIA AWASILI VISIWANI COMORO KWA ZIARA YA KIKAZI NA KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU




Moroni, Comoro – Julai 6, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bergamo uliopo mjini Moroni, Visiwa vya Comoro, kwa ziara ya kikazi ya siku moja kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mheshimiwa Azali Assoumani.

Mara baada ya kuwasili, Rais Dkt. Samia alilakiwa kwa heshima ya kijeshi na kukagua Gwaride la Jeshi la Umoja wa Visiwa vya Comoro, ikiwa ni sehemu ya mapokezi rasmi kwa viongozi wa kitaifa wanaoalikwa katika shughuli za kitaifa.

Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Samia atashiriki kama Mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Malouzini Omnisport, mjini Moroni.

Ushiriki wa Tanzania katika maadhimisho haya unaonesha kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Comoro, huku ukisisitiza dhamira ya Tanzania katika kudumisha mshikamano na udugu wa kihistoria na mataifa jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika na Bahari ya Hindi.

Rais Dkt. Samia anatarajiwa pia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Azali Assoumani kuhusu masuala ya ushirikiano wa pande mbili, hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji, utalii, elimu na afya.

Ziara hii inadhihirisha msimamo thabiti wa Tanzania wa kuendeleza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Saturday, July 05, 2025

VIONGOZI WA MANISPAA YA KIBAHA WATEMBELEA MBUGA YA MIKUMI KUUNGA MKONO UTALII WA NDANI

 









Mikumi, Morogoro – Katika juhudi za kuunga mkono kampeni ya kukuza utalii wa ndani iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakuu wa Divisheni na Vitengo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wamefanya ziara maalum katika Mbuga ya Wanyama ya Mikumi.

Ziara hiyo imeongozwa na Afisa Utumishi wa Manispaa ya Kibaha, Bw. Mrisho Mlela, ambaye amesema kuwa lengo kuu ni kuhamasisha utalii wa ndani kwa vitendo, huku viongozi na watumishi wa umma wakiwa mstari wa mbele katika kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini.

“Tumeona ni muhimu sisi kama viongozi na watumishi wa umma kuonesha mfano kwa kutembelea vivutio vya ndani ya nchi. Hii ni njia mojawapo ya kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha utalii wa ndani, ambayo inalenga kuongeza mapato ya ndani kupitia sekta hii muhimu,” amesema Bw. Mlela.

Ameongeza kuwa utalii wa ndani si tu chanzo cha mapato kwa taifa, bali pia ni njia bora ya kujifunza kuhusu urithi wa taifa, uhifadhi wa mazingira, na maisha ya wanyamapori. Kwa kuandaa ziara kama hizi, menejimenti ya Manispaa inalenga kuwahamasisha wananchi na watumishi wengine kuenzi utalii wa ndani kama sehemu ya maisha yao.

Washiriki wa ziara hiyo walipata fursa ya kujionea kwa karibu aina mbalimbali za wanyama waliopo katika Mbuga ya Mikumi, ikiwa ni pamoja na tembo, simba, twiga, pundamilia, nyati, viboko na aina mbalimbali za ndege na wanyamapori wengine.

Mbali na kuvutiwa na mandhari ya kipekee ya mbuga hiyo, washiriki walijifunza kuhusu namna wanyamapori wanavyohifadhiwa, changamoto za uhifadhi, na fursa za kiuchumi na kijamii zinazotokana na utalii unaozingatia misingi ya uendelevu.

Mbuga ya Mikumi ni moja ya mbuga kongwe na maarufu nchini Tanzania, inayopatikana kati ya mikoa ya Morogoro na Pwani, ikiwa ni sehemu ya mfumo wa hifadhi ya Selous (sasa Nyerere National Park). Kwa ukaribu wake na miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mikumi imekuwa kivutio kikuu kwa watalii wa ndani na wa nje wanaotaka kupata uzoefu wa wanyamapori kwa muda mfupi.

Ziara hiyo imeacha alama kwa washiriki, ambapo wengi wao walieleza kufunguka macho na kuongeza hamasa ya kutembelea vivutio vingine vya ndani ya nchi. Wameahidi kuwa mabalozi wa utalii wa ndani kwa familia zao, jamii na ofisi walizotoka.

Kwa mujibu wa Menejimenti ya Manispaa ya Kibaha, ziara kama hizi zitaendelea kufanyika kwa awamu ili kuhakikisha watumishi wengi zaidi wanashiriki, na kwa namna hiyo kutoa mchango wa moja kwa moja katika kuinua sekta ya utalii wa ndani.

“Tanzania ni hazina ya vivutio. Ni jukumu letu sote – si wageni tu – kuvithamini, kuvitangaza na kuvitumia kwa maendeleo yetu,” amesema mmoja wa washiriki wa ziara hiyo kwa msisimko mkubwa.

PPAA yatoa rai wazabuni kutumia moduli kuwasilisha rufaa

  Na Mwandishi wetu, Dar Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa rai kwa wazabuni kutumia Moduli ya kupokea na kushughulikia malal...