Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

Thursday, October 01, 2026

SERIKALI YARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA KITUO CHA KISASA CHA UTALII KUSINI, KUKAMILIKA DESEMBA

 








Na Mashaka Mhando, Iringa

UJENZI wa kituo cha kisasa cha utalii mkoani Iringa, kinachotarajiwa kuwa mkombozi na kiungo muhimu cha kukuza utalii katika Ukanda wa Kusini, umefikia asilimia 88 na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Desemba mwaka huu.

Kituo hicho cha kimkakati kimejengwa kikiwa na huduma zote za kisasa, ikiwemo ngazi za umeme (escalators), kumbi za mikutano, pamoja na ofisi zitakazowakutanisha wadau wote wa sekta ya utalii chini ya jengo moja.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, ameeleza kuridhishwa kwake na kasi pamoja na ubora wa kazi inayofanyika alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo leo, Septemba 30, 2026.

Miradi Mingine na Mkakati wa Ukanda wa Kusini

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Dkt. Abbasi alibainisha kuwa kukamilika kwa kituo hicho ni muendelezo wa juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya utalii kusini mwa Tanzania, ikitanguliwa na kukamilika kwa jengo la utafiti mkoani humo.

“Ujio wa jengo hili unafuatia pia kukamilika kwa jengo jingine la masuala ya utafiti. Na jana tumeona uwanja wa ndege wa Mikumi ukimaliziwa, lakini pia Iringa kule Ruaha viwanja viwili vya ndege, majengo ya wageni (hostels), na majengo mengine pia vilishakamilika,” alisema Dkt. Abbasi.

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati katika Hifadhi za Kitulo na Katavi ili kuhakikisha fursa za kitalii katika Ukanda wa Kusini zinatumika kikamilifu.

“Kwa ufupi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan, ipo kazini katika kuendeleza na kukuza utalii Ukanda wa Kusini,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo.

Wednesday, September 30, 2026

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU ASAFIRI KWA SGR KUELEKEA DODOMA

 

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Septemba 30, 2026 amesafiri kwa treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma.

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo.





KUMBUKIZI YA MIAKA 121 YA VITA VYA MAJIMAJI YATOA MSUKUMO MPYA KWA URITHI NA UTALII WA KILWA

 









KILWA MASOKO: Uzinduzi wa Sherehe za Kumbukizi ya Miaka 121 ya Vita vya MajiMaji umefungua fursa na kutoa msukumo mpya katika juhudi za kuhifadhi, kutangaza na kuendeleza urithi wa kihistoria na kiutamaduni wa Kilwa, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kuenzi historia ya mashujaa wa Vita vya MajiMaji.

Sherehe hizo zimezinduliwa leo, Septemba 30, 2026, katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko, na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Malima, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, pamoja na wazee wa mila na viongozi mbalimbali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Malima amesema kumbukizi ya miaka 121 ya Vita vya MajiMaji ni zaidi ya kukumbuka historia, bali ni fursa ya kuitumia historia hiyo katika kujenga kizazi kinachothamini urithi wa Taifa na kuchochea maendeleo kupitia utalii wa kiutamaduni na 

“Ni muhimu kuandikwa kitabu kinachozungumzia  historia ya Vita vya MajiMaji na kuhifadhiwa kwa kuzingatia vyanzo vya wenyeji, simulizi za wazee na maarifa yaliyorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, badala ya kutegemea pekee maandiko yaliyoandikwa na wageni ambao hawakuwa sehemu ya jamii zilizohusika katika historia hiyo, amesema Mhe. Malima

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha maeneo yenye historia ya Vita vya MajiMaji yanatambuliwa, yanahifadhiwa na kutangazwa ili yaweze kunufaisha jamii na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Malima amewataka wananchi, hususan vijana, kuwa sehemu ya juhudi za kulinda na kutangaza urithi wa Kilwa kwa kujifunza historia ya mashujaa wa MajiMaji na kuhakikisha simulizi na maeneo ya kihistoria yanatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amesema kumbukizi hiyo ni fursa muhimu ya kuendelea kuitangaza Kilwa kama eneo lenye utajiri mkubwa wa historia, utamaduni na urithi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika kulinda na kuendeleza urithi huo.

Ushiriki wa wazee wa mila katika uzinduzi huo umeongeza thamani katika jitihada za kuhifadhi maarifa, simulizi na historia zinazorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Aidha, mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kushiriki katika uzinduzi huo umeonesha kuongezeka kwa uelewa na hamasa ya jamii katika kuenzi historia ya mashujaa wa Vita vya MajiMaji na kutambua umuhimu wa urithi wa Kilwa.

Sherehe hizo zinafanyika chini ya kaulimbiu *“MAJIMAJI NA URITHI WA KILWA”,* inayolenga kuunganisha historia ya mapambano ya MajiMaji na urithi mpana wa Kilwa katika kuibua fursa za elimu, utamaduni na utalii.

Kupitia kumbukizi hiyo, Kilwa inapata fursa ya kuendelea kuangazia maeneo yake ya kihistoria na simulizi za mashujaa wa MajiMaji, huku wadau mbalimbali wakihamasishwa kushiriki katika kuyahifadhi, kuyaendeleza na kuyatangaza.

Sherehe za Kumbukizi ya Miaka 121 ya Vita vya MajiMaji zitaendelea na shughuli mbalimbali za kihistoria, kielimu na kiutamaduni, kwa lengo la kuwakutanisha wananchi na wadau katika kuenzi mashujaa wa MajiMaji na kuimarisha uhifadhi wa urithi wa Taifa.

Kumbukizi hiyo inatoa msukumo mpya wa kuhakikisha historia ya Vita vya MajiMaji inaendelea kuwa hai, inafundisha kizazi cha sasa na kijacho, na wakati huo huo inatumika kama nyenzo muhimu katika kukuza utalii wa kihistoria na kiutamaduni wa Kilwa.

Tuesday, September 29, 2026

Uwanja wa Ndege wa Kisasa Mikumi Kukamilika Novemba

Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Katika kufungua miundombinu zaidi ya utalii nchini, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inakamilisha uwanja mwingine wa ndege wa kisasa utakaoleta mageuzi katika sekta ya utalii nchini.

Uwanja huo unaojengwa katika Hifadhi ya Taifa Mikumi, lango muhimu la utalii unaounganisha Bara na Zanzibar, una urefu wa kilometa 1.8 na ukiwa na majengo ya kisasa ya kupokea na kuondokea abiria, jengo la zimamoto na kituo maalum cha hali ya hewa, unatumia teknolojia ya kisasa ya lami maalum (polymer) inayounda tabaka gumu linalodumu kwa zaidi ya miaka 15.

“Tulipopokea taarifa ya maandishi pale Wizarani mlionesha Novemba mwaka huu mradi huu muhimu utakamilika. Hakika nimefika hapa leo na nimejionea kazi nzuri mliyoifanya na nimejiridhisha kuwa kweli Novemba 15, 2026 mradi huu wote mtakuwa mmetukabidhi,” anasema Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, alipokagua mradi huo leo Septemba 29, 2026, Hifadhini Mikumi. 

Viwanja vingine vitatu kama hivyo vimekamilika ikiwemo Hifadhi ya Nyerere (1) na Hifadhi ya Ruaha (2).







Monday, September 28, 2026

PROF. SHEMDOE ASHIRIKI MAFUNZO YA UONGOZI HARVARD

 



Na Mwandishi Wetu, Boston – Marekani

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, anashiriki mafunzo maalum ya uongozi kwa Mawaziri wa Kisekta yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Harvard, jijini Boston, Marekani.

Mafunzo hayo ya siku nne yameanza Septemba 26, 2026 na yanatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2026, yakilenga kuwawezesha Mawaziri wa Kisekta kutoka nchi mbalimbali za Afrika na maeneo mengine kubadilishana uzoefu na maarifa katika uongozi, usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya wizara za kisekta.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Mawaziri wa Kisekta kutoka Tanzania, Kenya, Nigeria, Namibia, Chile, Dominican Republic, Malawi, Benin, Côte d’Ivoire, Gabon, Ghana, Guinea, Mauritius, Mauritania, Msumbiji, Sierra Leone na Togo.

Kupitia mafunzo hayo, Mawaziri hao wanapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za uongozi wa kisekta, usimamizi wa taasisi za umma, ufanyaji wa maamuzi na namna ya kuimarisha utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, mafunzo hayo yanawapa washiriki fursa ya kujifunza kutoka kwa viongozi wenye uzoefu mkubwa, wakiwemo Mawaziri wa zamani na Marais wastaafu, pamoja na kushirikishana uzoefu kuhusu changamoto na fursa zinazojitokeza katika uongozi wa sekta za umma.

Miongoni mwa wakufunzi katika mafunzo hayo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais wa Tano wa Botswana, Mhe. Mokgweetsi Masisi.

Ushiriki wa Prof. Shemdoe katika mafunzo hayo unatoa fursa ya Tanzania kushiriki katika jukwaa la kimataifa la kubadilishana uzoefu wa uongozi na usimamizi wa sekta za umma, hususan katika maeneo yanayohusu Serikali za Mitaa na utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa wananchi.

Maarifa na uzoefu unaopatikana kupitia mafunzo ni nyenzo muhimu katika kuendelea kuimarisha uongozi, usimamizi na utoaji wa huduma za Serikali kwa ufanisi, pamoja na kuongeza ujuzi wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kisekta pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kozi hiyo imeandaliwa na T.H. Chan School of Public Health, Harvard Graduate School of Education na Harvard Kennedy School, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha viongozi wa kisekta kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu katika uongozi wa umma.

NDEJEMBI ATOA SIKU 14 KUANDAA MPANGO WA KUWAWEZESHA VIJANA 10,000 KILA MWAKA



NA MWANDISHI WETU, ARUSHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametoa siku 14 kwa viongozi wa Serikali kuandaa mpango wa kuwawezesha vijana 10,000 kila mwaka kutoka fani mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga rasilimali watu yenye utaalamu na ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Agizo hilo limetolewa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo; Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar; Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo; pamoja na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Akifungua Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026) jijini Arusha leo, Septemba 28, 2026, Ndejembi amesema Tanzania haiwezi kufikia malengo ya Dira 2050 bila kuwekeza kwa makusudi katika rasilimali watu, hususan vijana.

Amesema vijana wanapaswa kupewa fursa ya kupata utaalamu, ujuzi na uzoefu unaoendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa ili wawe sehemu muhimu ya kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa Taifa.

“Tusipime mashirika ya umma kwa kiwango cha gawio wanachotoa pekee, bali kwa namna yanavyoongeza tija kwa vijana ambao ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Ndejembi.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu unapaswa kuwa sehemu ya msingi ya utekelezaji wa Dira 2050, huku taasisi na mashirika ya umma zikitakiwa kushiriki kikamilifu katika kuwajengea vijana uwezo wa kitaalamu.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, mabadiliko ya teknolojia, ikiwamo matumizi ya akili bandia (AI) na mifumo ya kidijitali, yanaongeza umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia hizo kuongeza ufanisi, tija na ubora wa huduma.

TAASISI ZA UMMA ZITAKIWA KUONGEZA THAMANI

Katika mwelekeo mpana wa Serikali kwa taasisi na mashirika ya umma, Ndejembi amezitaka taasisi hizo kutoridhika na jukumu la kulinda mali na uwekezaji wa Serikali, bali kuhakikisha mali hizo zinaongeza thamani na kuleta manufaa makubwa zaidi kwa Taifa.

“Msije kuwa walinzi wa mali pekee; kuweni waongezaji thamani wa mali mlizokabidhiwa,” amesema.

Amesema taasisi na mashirika ya umma zinapaswa kuwa injini za mabadiliko ya uchumi, kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha huduma, kuimarisha ushindani, kutumia rasilimali kwa ufanisi na kuwekeza zaidi katika teknolojia na ubunifu.

Pia amezitaka taasisi hizo kuwa na mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari za El Niño, huku zikishirikisha sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Kwa watendaji wakuu, Ndejembi amesema mafanikio ya uongozi hayapaswi kupimwa kwa kipindi ambacho kiongozi amekaa madarakani pekee, bali pia kwa uimara wa taasisi anayoiacha, uwezo wa kuandaa viongozi wa baadaye na namna alivyojenga vipaji na rasilimali watu.

SEKTA BINAFSI KUBEBA ASILIMIA 70 YA UCHUMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Amesema Dira 2050 inalenga sekta ya umma kuchangia asilimia 30 ya uchumi, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia asilimia 70, jambo linalohitaji taasisi za umma kujenga mazingira rafiki zaidi ya biashara na uwekezaji.

“Ili sekta binafsi ifanye vizuri, ni lazima taasisi za umma zitengeneze mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji,” amesema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Masanja Kadogosa, amesema kamati hiyo inaridhishwa na kasi ya mageuzi katika taasisi za umma, ingawa bado kuna nafasi kubwa ya kuendelea kuboresha utendaji.

Amezitaka taasisi hizo kuoanisha mipango na mikakati yao na Dira 2050, kuongeza uzalishaji na kuweka mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kwa kiwango kikubwa zaidi katika shughuli za kiuchumi.

UWEKEZAJI WA SERIKALI WAFIKIA SH92.28 TRILIONI

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema mabadiliko katika taasisi na mashirika ya umma yanapaswa kwenda sambamba na mfumo mpana zaidi wa kupima utendaji.

Amesema taasisi hazipaswi kupimwa kwa gawio pekee, bali pia kwa tija, ubora wa huduma, matumizi bora ya rasilimali, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwezo wa kushindana na mchango wao katika uchumi wa Taifa.

Mchechu amesema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi na kampuni ambazo Serikali ina hisa imeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh92.28 trilioni mwaka 2024/25.

Aidha, mapato yasiyo ya kodi yaliyotokana na uwekezaji wa Serikali yameongezeka kutoka Sh637.7 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26.

Amesema ongezeko hilo linaongeza wajibu kwa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha rasilimali za Serikali zinasimamiwa kwa ufanisi na kuendelea kuzalisha thamani kwa uchumi na wananchi.

C-CEOs FORUM YAKUTANISHA ZAIDI YA WASHIRIKI 700

C-CEOs Forum 2026 ni mkutano wa nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 na mwaka huu unawakutanisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi na mashirika ya umma, sekta binafsi, taasisi za fedha, wawekezaji, washirika wa maendeleo, wataalamu na wasomi.

Mkutano huo unaofanyika Arusha kuanzia Septemba 28 hadi 30, 2026, una kaulimbiu: “Taasisi na Mashirika ya Umma yenye Ufanisi wa Juu kwa Uchumi Shindani, Jumuishi na Imara Katika Kutekeleza Dira 2050.”

Majadiliano yake yanajikita katika uongozi, utawala bora, ubunifu, rasilimali watu, ushindani na namna taasisi na mashirika ya umma zinavyoweza kuongeza thamani ya kiuchumi na kijamii katika utekelezaji wa Dira 2050.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo, amesema benki hiyo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa Dira 2050.

Amesema TCB imeendelea kuelekeza mikakati yake katika kuunga mkono sekta za uzalishaji zinazoendana na malengo ya Dira 2050, sambamba na mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea nchini.

Mkutano huo unaratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) na kudhaminiwa na TCB.

TANZANIA NA OMAN KUIMARISHA USHIRIKIANO WA WANAHABARI KUPITIA KONGAMANO LA OKTOBA MOSI

 




Na Mwandishi Wetu 

Chama cha Waandishi wa Habari cha Oman (OJA), kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kimeandaa kongamano la pamoja la wanahabari kutoka Oman na Tanzania, litakalofanyika Oktoba 1, 2026, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Mwenyekiti wa OJA, Dkt. Mohammed Mubarak Al-Araimi, amesema ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanahabari na kudumisha uhusiano wa kihistoria, kiuchumi na kitamaduni kati ya Oman na Tanzania.

Dkt. Al-Araimi, ambaye amezuru Tanzania kwa mara ya kwanza, amesema ujio wake pamoja na ujumbe wa wanahabari kutoka Oman ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Amesema jukwaa hilo halilengi tu kuwakutanisha wanahabari, bali pia linatumika kama daraja la kuendeleza uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria, kiuchumi na kitamaduni uliopo kati ya Oman na Tanzania.

Amesema kongamano hilo litawakutanisha takriban wanahabari 40 kutoka Oman, ambao watajadili mada zinazohusu sekta ya habari, uchumi, uwekezaji, utalii na biashara, kwa lengo la kutafuta fursa zitakazonufaisha pande zote mbili kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya, amesema mchakato wa ushirikiano kati ya JOWUTA na OJA ulianza mwaka 2022 wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Shirikisho la Wanahabari Duniani (IFJ), na kwamba umeendelea kukua hadi kufikia hatua ya kuandaliwa kwa kongamano hilo, ambalo amesema ni la kwanza kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki na SADC baada ya OJA kufanya kongamano kama hilo nchini Misri.

Msuya amesema kongamano hilo litakuwa na mada kuu nane, nne kutoka Tanzania na nne kutoka Oman, zitakazojadili masuala ya habari na ushirikiano wa wanahabari, uchumi na biashara, uwekezaji pamoja na utalii. Amesema mjadala huo unalenga kutumia sekta ya habari kama daraja la kufungua fursa na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman.

Amesema ushirikiano huo pia unaunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza fursa za uwekezaji nchini, huku akieleza kuwa wanahabari wanapaswa kutumia nafasi hiyo zaidi ya kuandika habari kwa kujenga uhusiano wa kisekta utakaosaidia kuvutia wawekezaji kutoka Oman kuja Tanzania na pia kutoa fursa kwa Watanzania kwenda kuwekeza Oman.

Pia amesisitiza kuwa  wanahabari sasa wanaipambania nchi si kwa kuandika habari pekee, bali pia kwa kutumia taaluma yao kujenga mahusiano ya kisekta, kutangaza fursa za uwekezaji, biashara na utalii, pamoja na kuwaunganisha wawekezaji wa Oman na Tanzania na Watanzania wanaotaka kuwekeza Oman.

Msuya amesema siku ya kongamano hilo, JOWUTA na OJA zinatarajiwa kutia saini Hati ya Makubaliano (MoU), itakayofungua ukurasa mpya wa ushirikiano na kuwezesha ubadilishanaji wa wanahabari, mafunzo pamoja na kubadilishana uzoefu kati ya wanahabari wa pande zote mbili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema jukwaa hilo litachangia kuimarisha diplomasia ya habari na uhusiano wa kihistoria na kitamaduni kati ya Tanzania na Oman, huku likitoa fursa ya kutangaza uwekezaji, biashara na utalii uliopo Tanzania Bara na Zanzibar kwa wananchi na wawekezaji wa Oman pamoja na mataifa mengine ya Kiarabu.

Balile amesema ushirikiano huo utaimarishwa zaidi kupitia MoU hiyo, itakayowezesha mafunzo, kubadilishana uzoefu, kukuza taaluma ya habari na kujenga uwezo wa wanahabari wa pande zote mbili. Amewataka wanahabari wa Tanzania kutumia fursa hiyo kuripoti habari zitakazoongeza uelewa kuhusu uhusiano na fursa zilizopo kati ya nchi hizo.

Msuya amewataka wanahabari na vyombo vya habari kutoa taarifa za kutosha kuhusu kongamano hilo, akieleza kuwa ni muhimu viongozi wakuu wa Serikali, wakiwemo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mawaziri wa sekta husika, kutambua mchango wa sekta ya habari katika kukuza uhusiano, uwekezaji, biashara na maendeleo ya taifa.

CP KOMBO AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAAFISA HABARI WA JESHI LA POLISI

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo amewataka Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi kuendelea kuwa nguzo imara katika kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu masuala ya ulinzi na usalama.

Hayo amezungumza Septemba 28, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu kwa Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi wa Makao Makuu ya Polisi, Mikoa, Vikosi na Vyuo vya Polisi katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.

CP Kombo amehimiza nafasi ya Maafisa Habari katika kujenga na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na jamii, huku akiwataka kutumia taaluma yao kuhakikisha umma unapata elimu na taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu Jeshi la Polisi ikiwemo kazi na mafanikio.

"Ninyi ni kiungo muhimu sana kati ya Jeshi la Polisi na jamii, kazi yenu sio tu kutoa taarifa bali kuwajengea uelewa wananchi kuhusu majukumu ya Jeshi la Polisi, changamoto zake, mafanikio yanayopatikana na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao" alisema CP Kombo 

Naye, Kamishna wa Polisi Jamii CP Alex Mkama amesema kuwa kitengo cha habari na uhusiano ndani ya Jeshi la Polisi kimekuwa na mchango mkubwa katika kuzuia na kutanzua uhalifu kwani jamii imekuwa ikihabarishwa na kujengewa uwezo wa kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu kabla haujatokea katika maeneo yao.

CP Mkama aliongeza kuwa, Maafisa Habari wa Mikoa wamekuwa msaada mkubwa sana kufikisha kwa umma elimu ya Polisi Jamii inayotolewa na Maafisa Polisi Jamii wa Mikoa, Wilaya na Polisi Kata na kuahidi kuendelea kushirikiana nao ili kuongeza chachu zaidi na kupata mafanikio zaidi katika kuzuia na kutanzua uhalifu.

Akitoa neno la utangulizi katika hafla ya ufunguzi wa kikao kazi hicho, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime amesema kuwa Afisa Habari wa Jeshi la Polisi amekuwa ni mtu muhimu katika kuandaa na kusambaza maudhui sahihi ya kuelimisha na kutangaza mafanikio na majukumu ya Jeshi la Polisi.

DCP Misime aliongeza kuwa, utendaji kazi wa Maafisa habari wa Polisi umeleta matokeo chanya katika jamii kwani wameendelea kuwa kiungo muhimu kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, wamekuwa chachu katika uandaaji na utoaji wa taarifa kwa wakati, upigaji picha za kihabari na kuandaa maudhui ya uelimishaji jamii na kuainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu nchini.

Kikao kazi cha Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi nchini kimelenga kuwajengea uwezo, uelewa Maafisa habari wa Polisi na kuimarisha mahusiano mazuri kati yao na vyombo vya habari nchini katika kuhabarisha umma kwa kutumia njia za kidigitali na kujenga taswira chanya ya Jeshi la Polisi Tanzania kwa wananchi.







MADAKTARI BINGWA WA BMH WAWASILI NCHINI MALAWI KWA AJILI YA KAMBI YA MATIBABU YA KIBOBEZI

 


Malawi, Lilongwe 28 Septemba, 2026.

Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamewasili nchini Malawi kwa ajili ya kambi maalumu ya matibabu. Madaktari hao ambao wamewasili, wamepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Richard Kayola, aliyeikaribisha Timu hiyo na kuitakia mafanikio katika utoaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa mapokezi, Balozi Kayola amesema kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi na Utalii Tiba inayotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba vya Kisasa na wataalamu bingwa. 

Ameongeza kuwa kambi hiyo pia itatoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kimatibabu baina ya madaktari wa Tanzania na Malawi. Aidha, alifahamisha kuwa mwisho wa Kambi hii inategemewa utasainiwa Mkataba utakaowezesha wagonjwa wenye kuhitaji huduma zaidi kusafirishwa na kwenda nchini Tanzania kupata huduma kulingana na mahitaji husika. 

Kwa upande wake, kiongozi wa msafara huo, Bi. Monica Kessy, amesema madaktari wote wamewasili salama na wako tayari kutoa huduma kwa wananchi wa Malawi, huku akibainisha kuwa utoaji wa huduma utaongozwa na hospitali husika watakazofanyia kazi.

Kambi hiyo imeanza tarehe 28/09/2026 na inategemewa kumalizika tarehe 9/10/2026, ikitoa huduma za kibingwa katika upasuaji wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu, matibabu ya magonjwa ya moyo na mfumo wa mkojo, pamoja na tathmini kwa ajili ya upandikizaji wa figo.








SERIKALI YARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA KITUO CHA KISASA CHA UTALII KUSINI, KUKAMILIKA DESEMBA

  Na Mashaka Mhando, Iringa UJENZI wa kituo cha kisasa cha utalii mkoani Iringa, kinachotarajiwa kuwa mkombozi na kiungo muhimu cha kukuza u...