Thursday, December 31, 2015

MAKATIBU WAKUU NA MANAIBU KUAPISHWA KESHO 1,JANUARI 2016 JAMHURI YA MUUNGANO WAKURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

Kesho Ijumaa 01 Januari, 2016 Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wataapishwa rasmi katika Ukumbi wa Ikulu, uliopo lango kuu litazamalo baharini kuanzia saa nne asubuhi.

Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wote ambao wataapishwa na wale ambao walishaapishwa wanapaswa kuhudhuria katika tukio hili, ili mara baada ya kiapo kukamilika washiriki zoezi la kutia saini Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma (Integrity Pledge).  

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema zoezi la kutia saini hizo, litafanyika kwa uwazi mbele ya vyombo vya habari.
Aidha, Balozi Sefue amefafanua kuwa hata kama wapo baadhi ya Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu ambao walishasaini Hati hizo, watapaswa kusaini upya mbele ya vyombo vya habari.
Tukio hili pia litarushwa ‘live’ kupitia luninga.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi Mawasiliano, IKULU

31 Desemba, 2015

NAIBU WAZIRI WA ARDHI ANGELINA MABULA ATEMBELEA SHIRIKA LA NYUMBA (NHC)

1

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akiwasili Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa NHC Upanga jijini Dar es salaam huku akilakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Ndugu Nehemia Mchechu wakati waziri huyo akiwa katika ziara yake ya kujifunza na kusikiliza Changamoto na mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na shirika hilo.
2
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akiuliza jambo kwa mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Bw. Nehemia Mchechu wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
3
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Bw. Nehemia Mchechu wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
4
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akiwa katika kikao na wakuu wa vitengo mbalimbali  wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
5
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano makao makuu ya NHC , kulia ni  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Bw. Nehemia Mchechu .
6
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akifafanua jambo  kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano makao makuu ya NHC  Upanga. 
7
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akifafanua jambo  kwa waandishi wa habari  hawapo pichani katika ukumbi wa mikutano makao makuu ya NHC  Upanga. 
8
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Bw. Nehemia Mchechu  akijibu baadhi ya maswali yalioulizwa na waandishi wa habari wakati Naibu Waziri Angelina Mabula alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea shirika hilo leo.
9
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Bw. Nehemia Mchechu akijadiliana jambo na Muungano Saguya katikati na kulia ni Yahya Charahani Maafisa kutoka shirika hilo la NHC.

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA BARUA PEPE ZA KAWAIDA KATIKA MAWASILIANO YAKE


Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam. 

Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (katikati) akiwasili Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao kwa ziara ya kikazi leo jijini Dar es salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao leo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam. Mkurugenzi wa Uratibu wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao Bw. Benjamin Dotto akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini leo jijini Dar es salaam. 
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini leo jijini Dar es salaam. 


Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akizungumza na Watendaji na baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala ya Serikali Mtandao leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam. 


Na. Aron Msigwa –MAELEZO. 
Serikali imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao. 

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini. 

“Sasa kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi hii ni ndogo lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano binafsi. 

Amesema kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali. 

Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano. 

“Katika hili ninatoa siku 60 muhakikishe kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili kwa wale watakaopuuzia hatua zianze kuchukuliwa” Ameeleza Mhe. Angella. 

Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa Wakala hiyo kuweka mpango wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga utaratibu wa kuwarithisha uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji wa Wakala hiyo. 

Mhe. Kairuki amewataka kuwa wabunifu katika kuanzisha mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha dhana ya Serikali mtandao ili kupunguza gharama hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA. 

Akizungumzia kuhusu ununuzi wa vifaa vya TEHAMA serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana kwa bei ya kawaida. 

“katika hili Serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika katika upotevu wa mapato muhakikise mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika masuala ya ununuzi wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe na manufaa kwa wananchi na thamani halisi ya fedha” 

Amesema Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu na kutoa wito kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa wabunifu katika kutengeneza programu mbalimbali na mifumo salama itakayowasaidia wananchi kupata huduma. 

Aidha, katika hatua nyingine ameitaka e-Gov kuendelelea kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala hiyo iendelee kulifanyia kazi suala la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza kati ya taasisi moja hadi nyingine ili huduma zote ziweze kupatikana katika eneo moja na kuondoa urudufu wa mifumo iliyopo. 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala hiyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali toka kuanzishwa kwake Julai 11, 2012 imeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa Serikali Mtandao. 

Amesema kuwa Wakala hiyo inaendelea kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinawafikia wananchi kupitia mtandao mahali walipo na kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la huduma zote za Serikali kupatikana chini ya dirisha moja. 

Aidha amesema kuwa Wakala ya Serikali Mtandao itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya matumizi ya TEHAMA katika Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali vinazingatiwa. 

Waziri Mahiga akutana na Mabalozi wa Qatar na Kuwait waliopo nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akifanya mazungumzo na Balozi wa Qatar Mhe. Abdullah Jassim Almaadadi alipofika Wizarani kwa ajili ya kumpongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa wake mpya na pia kumhakikishia ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 30 Desemba, 2015. 
Balozi Al maadadi naye akizungumza huku Mhe. Mahiga akimsikiliza. 
Mazungumzo yakiendelea 
Waziri Mahiga akiagana na Balozi Al Maadadi mara baada ya kumaliza mazungumzo. 
.......Mkutano na Balozi wa Kuwait nchini 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Augustine Mahiga (kulia) akizungumza na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Nassem Ibrahim Al Najib, alipokuja kumtembelea Wizarani na kufanya mazungumzo naye kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kuwait na pia kumpongeza. 
Balozi Mahiga akiagana na Balozi wa Kuwait mara baada ya kumaliza mazungumzo naye. 
Picha na Reginald Philip

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI ASISITIZA UTENDAJI KAZI WENYE TIJA

JH1
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akitoa hotuba kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza(hawapo pichani) kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016. Baraza hilo limefanyika Desemba 31, 2015 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
JH2
Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza wakati akitoa hotuba yake kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
JH3
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakiwa timamu kumpokea Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(hayupo pichani) wakati akiwasili tayari kwa kulihutubia Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
JH4
Maafisa ngazi ya juu wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini hotuba fupi aliyoitoa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).
…………………………………………………………………………………………………
Na Lucas Mboje, Dar es Salaam
WATUMISHI wa Jeshi la Magereza wametakiwa kuzingatia utendaji kazi wenye tija mahala pa kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea(Business as usual).
Rai hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja wakati akizungumza kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini, Dar es Salaam.
Jenerali Minja amewaagiza Watumishi wote wa Jeshi hilo kuhakikisha kuwa wanawajibika kwenye maeneo yao ya kazi ili kufikia ufanisi uliotarajiwa pamoja na kutumia vizuri rasilimali za Ofisi kwa manufaa yaliyokusudiwa.
“Utekelezaji wenu wa kazi za kila siku lazima uwe na tija na uendane sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ili kufikia ufanisi unaotarajiwa”. Alisema Jenerali Minja.
Aidha Jenerali Minja amezungumzia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka 2015 ambayo ni pamoja na kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Magereza ambayo italiwezesha Jeshi hilo kutekeleza mpango wake wa Maboresho ya maeneo mbalimbali, kusainiwa kwa Mkataba  na Kampuni ya Poly Teknology ya China itakayojenga nyumba 9,500 za Makazi ya Maafisa na Askari, kusainiwa kwa Mkataba wa Magari 9,05 na Kampuni ya Ashok Leyland ambapo magari hayo yanatarajiwa kupokelea mapema mwakani.
Mafanikio mengine ni pamoja na Usajili wa kudumu wa Chuo cha Urekebishaji ambapo Chuo hicho kitatoa elimu stahiki ya Urekebishaji itakayotambulika ndani na nje ya Nchi, Jeshi la Magereza limepeleka Maafisa wake kwenye shughuli za Ulinzi wa Amani kwenye nchi mbalimbali zenye migogoro, Jeshi limeingia ubia na Wawekezaji mbalimbali katika miradi ya Kilimo, uchimbaji madini ya chokaa, ujenzi wa maduka makubwa(shopping Malls) katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro ambapo miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa Jeshi.
Vilevile Jeshi limefanikiwa kuandaa Maandiko mbalimbali ikiwemo andiko la kujitosheleza kwa chakula na miradi minane ambayo miradi hiyo ikiwezeshwa inaweza kuongeza thamani za mali zinazozalishwa na Jeshi hilo.
Aidha Jenerali Minja alieleza changamoto mbalimbali ambazo Jeshi hilo linakabilianazo ambazo ni ufinyu wa bajeti, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri, ukosefu wa zana za kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kuathiri Uzalishaji, tatizo la miundombinu ya magereza na msongamano magerezani hali inayopelekea kwa kiasi fulani kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja ametoa Salaam za kheri ya Mwaka mpya 2016 kwa Watumishi wote wa Jeshi hilo na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotawala uendeshaji wa Jeshi la Magereza.

TAARIFA MUHIMU KWA UMMA KUTOKA UTUMISHI

LO1Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inawatahadharisha wateja na wananchi wote kujihadhari na watu wanaotumia jina la ofisi kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kujitambulisha kuwa ni watumishi wa ofisi hii. Imebainika miongoni mwa wanaotapeli anatumia jina la James Josephat na kujifanya ni mtumishi wa masijala. Namba ya simu inayotumika kutapeli ni namba 0657 888 277. Ofisi haina mtumishi mwenye jina hilo, na huduma za ofisi hazitolewi kwa ada ya aina yoyote. Ofisi inawatahadharisha wadau na wananchi kuzingatia taratibu zilizopo na kuelewa huduma hazitolewi kwa malipo ya aina yoyote. Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Kny: Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

TAHADHARI YA JESHI LA POLISI KUHUSU MKESHA WA MWAKA MPYA

Tunapoelekea kumaliza mwaka 2015 na kuukaribisha  mwaka mpya wa  2016, wananchi hutumia muda huo kwenda  katika nyumba za ibada ama kusherekea katika maeneo mbalimbali ya starehe, ambapo uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo  vinavyohatarisha usalama wa raia mali zao.
Jeshi la Polisi nchini, limejipanga vizuri katika mikoa yote kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kwamba vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza  hususani katika kipindi hiki cha kuelekea mkesha wa mwaka mpya vinadhibitiwa. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Aidha,  Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama maeneo ya biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa ni 111 au 112.
 Pia,  Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabar
ani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Vilevile, wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabani pamoja na kupiga mafataki. Aidha, yeyote atakayefanya vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nawatakieni watanzania wote kheri ya mwaka mpya.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.        

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA FEDHA (JFC) WAFANYIKA LEO OFISI YA MAKAMU WA RAIS

ua1
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa January Makamba (mbele), akitafakari jambo wakati wa kikao cha kujadili changamoto na utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC) jijini Dar es Salaam leo,  kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Tume hiyo, Abdulrahaman Jumbe. (Picha na OMR)
ua2
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa January Makamba (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC) katika Mkutano wa kujadili changamoto na utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo. (Picha na OMR)

BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO KUANZISHA OFISI ZA KANDA

tab1
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Robert Pascal (Kulia) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa Benki, Bibi Neema Christina John (aliyevaa miwani) wakati wa uhakiki wa fomu zilizojazwa na moja kati ya vikundi vilivyofanikiwa kupata mkopo kutoka Benki hiyo.
tab2
Mwanasheria mwandamizi wa TADB, Bibi Salome Masenga (Kulia) akimuelekeza mmoja wa wanakikundi waliopata mikopo kutoka Benki hiyo.
tab6
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas Samkyi (Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Kasunga (Kulia).
tab7tab10Picha ya pamoja
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Iringa
Benki mpya ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema hadi kufikia miaka mitano ijayo itakuwa imefungua ofisi sita za kikanda zenye lengo la kuwahudumia wakulima nchi kote.
Mikakati hiyo iliwekwa bayana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Bibi Kurwijila alisema kuwa TADB inalenga kutelekeza kwa vitendo Maelekezo ya Serikali ya kupunguza changamoto zinazowakabili wakulima nchi kote.
Aliongeza kuwa kwa sasa Benki inalenga kusambaa nchi nzima kwa kuanzisha Ofisi za Kikanda ndani ya miaka mitano ijayo.
“Tunalenga kuwafikia wakulima wote nchini kadri siku zinavyoendelea kwenda na kutegemea mtaji unavyoongezeka ama upatikanaji wa fedha toka vyanzo mbali mbali ili kuweza kuwawezesha kumudu shughuli zao za kilimo,” alisema.
Aliongeza kuwa Benki inaleenga kuwajengea uwezo na kuanzisha Programu Maalumu ya Vijana wajihusishao na shughuli za Kilimo cha kibiashara na kushirikiana na wadau wengine kuhuisha shughuli za umwagiliaji na miradi ya kisasa ya umwagiliaji.
Malengo mengine ni kutafuta fedha toka vyanzo mbalimbali zenye gharama nafuu kwa minajili ya kuwakopesha Wakulima katika hatua zote za mnyororo wa ongezeko la thamani kwenye mazao ya Kilimo na kupanua wigo wa utaoji mikopo toka Minyororo Kumi na Minne (14) ya Mwanzo na kuhusisha pia mazao mengine ya Kilimo na pia kuwaunganisha Wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi amesema kwamba Benki yake imedhamiria kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini ili kuchagiza na kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Bw. Samkyi alisema TABD imejizatiti kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza tija na upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu maalum kwa sekta ya kilimo, kama njia ya kuleta Mapinduzi yenye tija kwa wakulima nchini.
“Benki imejipanga kutoa mikopo yenye riba nafuu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo,  wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika tasnia za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji nyuki),” alisema Bw. Samkyi.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba kwa kuanzia walengwa wakuu wa TADB ni wakulima wadogo wadogo, hatahivyo, hata wale wakulima wa kati na wakubwa watahudumiwa.
Bw. Samkyi imejidhatiti katika kufanya tathmini ya kina katika mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi kwa minajili ya kuongeza thamani na ushindani kwenye masoko.
“Sera ya TADB ni kutathmini mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi, na ambayo utatuzi wake utaongeza tija na uwezo wa ushindani kwenye masoko, na hivyo kukuza uchumi wa walio wengi na kupunguza umaskini,” aliongeza.
Katika hafla hiyo, jumla ya vikundi nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo wadogo 857, vilimiza vigezo na kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Kwa mujibu wa Bw. Samkyi kabla ya kutoa mikopo hiyo, benki iliwatembelea na kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla ya vikundi 89 vyenye jumla ya wanakikundi 21,526 vilifikiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mama Amina Masenza amewaasa Wakulima wote nchini kutumia vizuri mikopo wanayopewa ili kuweza kutimiza malengo yao binafsi na ya Serikali katika kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania.
Mama Masenza alisema kuwa wakulima wakitumia mikopo waliyopewa kwa malengo husika watafika mbali na kuweza kuchagiza mikakati ya Benki hiyo katika kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kilimo kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
“Naamini, wakati Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapoanza kufanya tathmini ya mikopo hii iweze kuona matunda ya uwekezaji wake hasa kwa nyie ambao mmeweza kubahatika kupata fursa ya awali kabili kunufaika na huduma za TADB,” aliwasihi.
Mama Masenza aliwaomba  wakulima hao kuwa Mfano Bora na wanaojitambua vilivyo, hasa nia ya kutoka katika kiwango fulani cha maisha kwenda katika hatua nyingine za juu zaidi kimaisha kwa kuongeza kipato na ubora wa kimaisha kwa ujumla kupitia huduma za TADB.
“Nawasihi kutotumia pesa hizi kinyume na malengo yaliyokusudiwa, kwani kwa kufanya hivyo, siyo tuu tunaiua Benki yetu bali pia tunajimaliza wenyewe kiuchumi. Wito wangu kwenu ni kujipanga kwa dhati ili kuweza kutimiza malengo makuu ya mikopo hii ambayo ni kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” aliongeza.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, mnamo tarehe 8 Agosti 2015 mjini Lindi. Uanzishwaji wa Benki hii ni utekelezaji wa malengo ya muda mrefu ya Serikali, katika kuitikia wito wa wananchi na wadau wengine wa maendeleo ili Tanzania iweze kupiga hatua endelevu za kimaendeleo.