Wednesday, November 30, 2011

JK awakubalia CUF kuonana naye sheria ya katiba

Ofisi ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Mheshimiwa Rais amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza maandalizi ya mkutano huo yafanyike mara moja.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

Monday, November 28, 2011

NMB yazindua Kituo cha Biashara Arusha

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Sila, akizindua rasmi Kituo cha Biashara kwa wafanya biashara wadogo, wakati na wakubwa wa Benki ya NMB mkoani Arusha jana. Wengine wanaoshuhudia kutoka kushoto ni CEO wa NMB, Mark Wiessing, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Misheck Ngatunga na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema. (Picha na Mpigapicha wetu).
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Sila, akipeana mkono wa shukrani na CEO wa Benki ya NMB, Mark Wiessing (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Misheck Ngatunga baada ya kuzindua rasmi Kituo cha Biashara kwa wafanya biashara wadogo, wakati na wakubwa wa Benki ya NMB mkoani Arusha jana. Kushoto ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema. (Picha na Mpigapicha wetu).
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Sila, akifurahi baada ya kuzindua rasmi Kituo cha Biashara kwa wafanya biashara wadogo, wakati na wakubwa wa Benki ya NMB mkoani Arusha jana. Wengine wanaoshuhudia kutoka kulia ni CEO wa Benki ya NMB, Mark Wiessing, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Misheck Ngatunga na kushoto ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema. (Picha na Mpigapicha wetu)

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Sila, akisoma kibao cha uzinduzi mara baada ya kuzindua rasmi Kituo cha Biashara kwa wafanya biashara wadogo, wakati na wakubwa wa Benki ya NMB mkoani Arusha jana. Wengine wanaoshuhudia kutoka kulia ni CEO wa Benki ya NMB, Mark Wiessing, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Misheck Ngatunga na kushoto ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema. (Picha na Mpigapicha wetu).

Tamasha la Str8t Music lafana Dar

Fabolous akifanya makamuzi
Sehemu ya nyomi iliyohudhuria
Sehemu ya nyomi iliyohudhuria
Naseeb Abdul ‘Diamond’ akiwajibika. Picha zote ni za Venance Nestory wa Mwananchi.

TAMASHA la Str8Muzik Festival Inter-College Special 2011 la vyuo kwa mwaka 2011 lililofanyika katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, Jumamosi na kuhudhuriwa na maelfu ya watu, limefana vilivyo.

Kwa muda wa saa tano, tamasha hilo lilipambwa na nyota wa Hip Hop wa Marekani, Fabulous aliyewarusha vijana wa kike na kiume wanaopenda burudani kadri muda ulivyoyoyoma.

Kundi la kwanza kutumbuza kwenye tamasha hilo lilikuwa ni Alleluyah lililokuja na free-style, ambalo lilivumbuliwa katika tamasha kama hilo lililofanyika mwaka
jana.

Fabulous alipanda stejini saa nne na kufanya vitu vyake na kuimba ngoma 20 zinazopendwa na mashabiki.

Baadaye ndipo ukaja wakati wa wanamuziki nguli wa Bongo Fleva waliopanda jukwaani kuanza na kundi la Manzese Crew, Inspekta Haroun, Amani Temba 'Mheshimiwa Temba' na Chege nao walikamua kwa ngoma zao.

Elius Barnaba alikuja akiwa na kundi lake la THT
pia Mfalme wa Rhyme, Afande Sele alipata wasaa wake wa kupiga shoo akifuatiwa na Pina wa Kikosi cha Mizinga alikamua ngoma mbalimbali pamoja na ngoma yake ya Umoja ni Nguvu na kuungwa mkono na wapenzi wa muziki waliokuwa wanamshangilia na kudhihirisha kuwa rapu si tu kwa Fabolous, bali hata kwa Wabongo.

Nao wana-Hip Hop kutoka Arusha Nako 2 Nako waliruka stejini na baadaye kupigwa tafu na wakali Jo Makini na Niki wa Pili.

Usiku huo ulipambwa pia na MwanaFa, Shetta,Diamond Platinum, Big Boy Baghad, Juma Nature, Mchizi Mox na Jay Mo walikamua
na kuwapagawisha wapenzi na sauti zao.

Tamasha la StrMuzik lilianzishwa mwaka 2005 na baadaye lilijulikana kama Inter-College Bash, na kufanyika Dar es Salaam na mwaka 2008 lilifika
hadi Mwanza, Morogoro na Dodoma.

Sugu afanya vitu vyake viwanja vya Ustawi wa Jamii


Mr II akiwa jukwaani na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika. Wabunge takribani wanane walisindikiza uzinduzi wake huo ulioenda sambamba na uzinduzi wa kitabu kinachoeleza historia yake katika maendelea ya muziki wa Rap Bongo.
Msanii Mr II Sugu akifanya vitu vyake usiku wa kuamkia jana kwenye viwanja vya Ustawi wa Jamii
Mheshimiwa Mbunge Joseph akiwa anachana mistari jukwaani usiku wa kuamkia jana, nyomi ilikuwa ya kutisha
**********************************

Boniface Meena

MKALI wa muziki wa Hiphop nchini, Joseph Mbilinyi maarufu kama 'Sugu' usiku wa kuamkia jana akisindikizwa jukwaani na wabunge kadhaa, aliteka nyoyo za maelfu wa mashabiki wa sanaa ya muziki waliofurika kushuhudia uzinduzi wa albamu yake mpya iliyopewa jina la 'Anti Virus' kwenye viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii, Jijini Dar es Salaam.
Sugu ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), alifunika tamasha hilo kwa kuimba nyimbo zake za zilizowateka kimawazo mashabiki wake wengi vijana.
Kivutio kikubwa kwenye onyesho hilo, alikuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye alipanda jukwaani na kuwasalimia mashabiki: "Oyoooo Oyoooo...nimefurahi kupanda jukwaani kucheza pamoja nanyi."
Katika onyesho hilo lililopambwa na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya muziki wa kizazi cha wakati huu (Bongo Fleva), Sugu pia aliimba na kucheza sambamba na wabunge wenzake kama John Mnyika, Joyce Mukya na Regia Mtema na Highness Samson.
"Oyoooo...Oyoooo. Nawashukuruni sana kwa kutuunga mkono, leo nauweka pembeni uheshimiwa na kushusha mawe. Pigeni kelele mpaka walioko Leaders Club wasikie," alisema Sugu.
Baada ya salamu hizo, alianza kwa kuimba wimbo wa 'Sugu Moto Chini' ambao uliwaamsha mashabiki kwa furaha, kisha akachombeza mashairi kadhaa ya wimbo 'Yamenikuta' na kupiga wimbo mwingine 'Kiburi' aliomshirikisha Stara Thomas.
Hakuishia hapo, akaimba wimbo mwingine 'Mambo ya Fedha', 'hayakuwa mapenzi' na mwisho akateremsha wimbo wenye jina la 'Sugu' ambao uliwapa utumwa wa kushangilia bila kuchoka mashabiki wake.
Kabla ya kushuka jukwaani Sugu alisema yuko mbioni kufanya wimbo na kumshirikisha mwenyekiti wake Mbowe.
Katika uzinduzi huo Sugu alisindikizwa na wasanii kama Danny Msimamo, Mabaga Fresh, Adili na Soggy Doggy Hunter, Mgosi Mkoloni, Mapacha, Suma G, Zay B na wengine wengi.

Sunday, November 27, 2011

JK akutana na Chadema

Rais Jakaya Kikwete, akimkaribisha mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Ikulu jijini Dar es salaam muda mfupi uliopita leo. (picha: K-VIS blog)


Ujumbe wa CHADEMA ukijongea lango la Ikulu

Rais Kikwete anakabidhiwa kabrasha la mapendekezo

Picha ya pamoja ya viongozi wa pande zote mbili
Mbowe na JK

RAIS Jakaya Kikwete jana alikutana na ujumbe wa Chadema kukabidhiwa kabrasha la mapendekezo yao na kujadili mchakato wa utungwaji wa Katiba mpya.

Rais alikutana na viongozi hao majira ya saa tisa na nusu alasiri mpaka saa 12 jioni na kukabidhiwa kabrasha la maoni ya viongozi hao kabla ya viongozi hao walioongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, kupiga picha za pamoja na Rais wakiwa ndani na baadaye nje ya jengo la Ikulu na hatimaye kuendelea na majadiliano.

Mbowe alilieleza Mwananchi kwamba kikao chao hicho cha majadiliano kilidumu kwa saa tatu na kiliahirishwa saa 12 jioni na kitaendelea kesho asubuhi saa nne.

"Ndugu waandishi wa habari tumekutana na Rais na baadhi ya mawaziri na Wasaidizi wake! Kikao kilianza saa 9:30 mchana na kiliahirishwa saa 12 jioni. Kikao kitaendelea kesho asubuhi saa nne. Taarifa kamili ni baada ya kikao,"alieleza Mbowe katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari.

Mbowe aliongozana na wajumbe wa kamati hiyo Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Said Arfi na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lisu, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati hiyo wakati wa mkutano huo na John Mrema. Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa ambaye ni mjumbe hakuwapo.

Saturday, November 26, 2011

Amavubi yawang'ata Kilimanjaro Stars bao moja bila

Kilimanjaro Stars
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwapungia mikoni mashabiki kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam jioni hii, Mara baada ya kuzindua rasmi michuano ya TUSKER CECAFA CHALLENGE CUP 2011 ambapo leo michuano hiyo imekutanisha timu za Tanzania Kilimanjaro Stars na Timu ya taifa ya Rwanda Amavubi, mpira umekwisha na timu ya Rwanda imeifunga Kilimanjaro Stars goli 1-0 , katika picha kulia anayecheka ni Rais wa TFF na Shirikisho la Vyama vya michezo Afrika Mashariki na kati CACAFA Leodger Tenga.
Kikundi cha ngoma cha Mama Africa kikitumbuiza jioni ya leo kwenye uwanja wa taifa wakati timu ya Taifa Kilimanjaro Stars ilipopambana na Amavubi ya Rwanda na kuambulia kipigo cha bao moja bila.


Mashabiki wakifuatilia kwa karibu mpambano huo kati ya Kilimanjaro Stars na Timu ya taifa ya Rwanda wakati wa mchezo wao wa kombe la TUSKER CECAFA CHALLENGE CUP 2011 kwenye uwanja wa Taifa jioni hii.

Mdau Amin Yasin ahitimu Degree yake OUT


Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi( kulia)akitunukiwa Shahada ya heshima ya salfasaya udaktari na mkuu wa chuo kikuu huria cha Tanzania John Malechela kwenye mahafari ya 23 ya chuo hicho yaliyofanyika janakatika viwanja vya chuo hichokilichoko Bungo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani

Mwandishi wa Habari wa gazeti hili Amini Yasini (kulia ) akiwa na wahitimu wenzake katika mahafari ya 23 ya chuo kikuu huria cha Tanzania muda mfupi kabla ya kutunukiwa shahada ya kwanza katika sayansi ya jamii na utawala ya chuo hicho jana wa katikati ni mwandishi wa habari Mwanzo Milinga na kushoto ni Emanuel Onyango PICHA ZOTE NA SANJITO MSAFIRI

Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi Communication Ltd Amini Yasini (kushoto) ambaye pia ni Afisa mtendaji wa kata ya Chumbi iliyoko Wilayani Rufiji Mkoani Pwani akifurahi na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mchinga Mudhihir Mohammed Mudhihir muda mfupi mara baada ya kutunukiwa shahada ya kwanza katika sayansi ya jamii na utawala ya chuo kikuu huria cha Tanzania ambapo mahafari hayo ya 23 ya chuo hicho yalifanyika jana katika viwanja vya chuo hicho kilichoko Bungo Mjini Kibaha Mkoani Pwani.

Friday, November 25, 2011

Benki ya Diamond Trust yafungua tawi la 13 jijini Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Abbas Kandoro akizindua Tawi la kumi na tatu la Benki ya Diamond Trust lililopo makutano ya Barabara za Lupa na Market mkoani Mbeya.

Tawi la kumi na tatu la Benki ya Diamond Trust lililopo makutano ya Barabara za Lupa na Market mkoani Mbeya.


Tuesday, November 22, 2011

Mataka apandishwa kizimbani
MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kuweka kumbukumbu za manunuzi ya magari chakavu yenye thamani ya zaidi ya Sh 1 bilioni.

Mbali ya Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Elisaph Ikomba ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa shirika hilo na William Haji ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa mahesabu wa shirika hilo.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincon alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo kati ya Juni na Julai 2007.

Katika shitaka la kwanza ambalo linawahusu washtakiwa wote, ilidaiwa kuwa kati ya Juni na Julai 2007 Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa nafasi zao walishindwa kutunza kumbukumbu za taarifa za kukubali zabuni ya ununuzi wa magari chakavu 26.

Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa shtaka la pili nalo linawahusu washtakiwa wote ambapo inadaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 washtakiwa kwa pamoja walishindwa kufuata taratibu za manunuzi ya umma katika ununuzi wa magari chakavu 26 yenye thamani ya Dola za Marekani 809,300,000 kutoka katika kampuni ya Bin Dalmouk Morots Co. Ltd ya nchini Dubai.

Katika shtaka la tatu linalomuhusu Mattaka, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 mshtakiwa akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa ATCL alitumia madaraka yake vibaya katika ununuzi wa magari hayo bila kuwepo kwa mkataba wa zabuni uliosainiwa na pande zote mbili na kuhakikiwa na bodi ya zabuni ya shirika hilo suala ambalo ni kinyume cha sheria.

CASTLE LAGER KUDHAMINI KUONYESHWA KWA MICHUANO YA LIGI KUU YA BARCLAYS AFRIKA

Premier League Fans Playing Games During Launch of Castle Lager's Perfect Moment Premier League Promotion.

Marian Ntuah Picking her T Shirt she won during Castle Lager's Premier League Perfect Moment Promotion.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

Castle Lager inadhamini kuonyeshwa kwa michuano ya ligi kuu ya uingereza ya Barclays kwenye vituo vya luninga katika nchi 48 barani Afrika. Shuhudia bia yako ya Castle ikionyesha klabu kubwa za ulaya zikichuana live, wachezaji bora na kukuacha ukishangilia timu uipendayo.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Castle Lager kudhamini kuonyeshwa live kwa michuano hii ya ligi kuu ya barani ulaya katika vituo vya luninga barani Afrika.

Ni sehemu ya kusaidia uendeshwaji matukio ya michezo katika bara zima na kufanya kila muda kuwa muafaka - hata kama utatazama michuano hii ukiwa nyumbani na rafiki zako kadhaa.

Mashabiki wapenzi wa soka watapata nafasi ya kuangalia timu nne zenye kiwango cha juu. Timu hizo ni kama Manchester United, Liverpool, Chelsea na Arsenal zitachuana katika ligi kuu ya Uingereza ya Barclays kila jumamosi katika michuano hiyo itakayoendelea.

Bia yako ya Castle imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika soka kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 ikiwa inadhamini Baraza la chama cha soka cha Afrika ya kusini (COSAFA) Michuano mkubwa, Kombe la Kagame Castle Tanzania na ligi kuu maarufu ya Soka nchini Afrika ya kusini.

Meneja wa kinywaji cha Castle Lager, Bi Kabula anasema “Castle Lager kwa makusudi imechagua vituo vingi vya luninga vitakavyosaidia michuano kuonwa na watazamaji wengi zaidi.

Amesema pia “kujihusisha kwa kinywaji cha Castle Lager katika kudhamini mpira wa miguu inatokana na wao kutambua mapenzi ya wateja wao”. “Tukiwa tunashirikiana na michuano hii ya ligi kuu ya Uingereza tunakiweka kinywaji chetu katika sehemu nzuri barani Afrika,” Alisema.

Bi. Kabula anasema pia kwamba Castle Lager ina mipango ya kuanziasha vitu vya kusisimua zaidi mwaka huu. “Kwahiyo iwe utatazamia michuano hii katika baa uipendayo au nyumbani ukiwa unachoma nyama na marafiki zako, hakikisha kila tukio linakuwa la uhakika ukiwa na Castle Lager yako mkononi. Bia yenye ladha kamili itakayokuwanya ukate kiu yako."

Kama sehemu ya mipango hii, Castle Lager pia imezindua promosheni ambayo itawawezesha wateja wa Castle Lager kujishindia zawadi mbalimbali wakienda kwenye baa au watakaponunua chupa ya Castle Lager.

Baa maalum zitakuwa na mabango ya Castle Lager yakiwa na namba maalum za kuscan. Wateja wataweza kuscan namba hizo kwa kutumia simu zao za mkononi, ambazo tovuti ya www.theperfectmoment.mobi itafunguka na kuwawezesha kucheza mpira wa miguu ndani ya tovuti hiyo na kujishindia zawadi mbalimbali.

Wateja ambao pia watanunua Castle Lager bia katika baa watapatiwa kadi ambayo ina namba maalum ambayo wataweza kutuma ujumbe mfupi kwenda namba fulani na kujishindia zawadi mbalimbali.

Monday, November 21, 2011

Nchimbi mgeni rasmi uzinduzi wa Albamu ya Anti Virus 2

Waziri kivuli wa Wizara ya Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo Joseph Mbilinyi (a.k.a. MR. SUGU -alievalia kadeti) leo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam 21-nov-2011 kuhusu shoo ijulikanyo Anti Virus wakati wa Tamasha la Burudani kwa washabiki 2011-i litalaofanyika jijini DSM hapo Nov. 26 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi,(kushoto) ni Msanii Fred Malaki (a,k,a- MKOLONI) n a Mwanadada Zainab Lipangile a.k.a ZAY –B, Katika tamasha hilo Wasanii mbalimbali watatumbuiza, -Picha zote na Mwanakombo Jumaa-MAELEZO,
Waziri kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (kulia) Joseph Mbilinyi a.k.a Mr, SUGU akionyesha kitabu ambacho ameelezea maisha yake kitakachopatikana wakati wa Shoo ijulikanayo Anti Virus katika Tamasha la Burudani kwa washabiki2011 litaakalofanyika Nov. 26,2011 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa michezo, (kushoto) ni Msanii Fred Malaki a.k.a. MKOLONI. ( Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO,)

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Emanuel Nchimbi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya wanamuziki wa kizazi kipya inayoitwa Anti Virus 2.
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam mratibu wa uzinduzi huo ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi alisema uzinduzi wa albamu hiyo unalengo la kuwakomboa vijana waweze kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa Mbilinyi amesema kwa muda mrefu wasanii wa muziki wa kizazi kipya wamekuwa wakizulumiwa na wajanja wachache kitu ambacho kimewaacha wasanii hao kuendelea kuwa maskini.
"Kuna wajanja wachache ambao kwa muda wa miaka mingi wamekuwa wakinufaika na jasho la wasanii sasa tumeamua kufanya mapinduzi kwa kuwaungunisha wasanii ili waweze kutetea haki zao".Alisema Mheshimiwa Mbilinyi.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii tarehe 26 Novemba kuanzia saa 12-6 usiku ambapo jumla ya wasanii zaidi ya 20 watashiriki ikiwa ni pamoja na waheshimiwa wabunge na mawaziri ambapo kiingilio kitakuwa ni shilingi 5000.
Katika tamasha hilo Mheshimiwa Mbilinyi atauza kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake ambacho kitauzwa kwa shilingi 5000

Vodacom FoundationTanzania Yatoa Msaada Wa Madarasa Mawili Mkoani iringa

Wazee wa kabila la Kihehe, kata ya Kalenga mkoani Iringa wakimpa heshima ya kichifu Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kusini Jackson Kiswaga kwa kumkabidhi mkuki baada ya kumvisha vazi la mgorole ikiwa ni heshima kubwa kwa mkoa huo wakati walipofika kukabidhi madarasa mawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 29 katika shule ya sekondari ya Lipuri mkoani humo.
Mkuu wa mfuko wa kusaidia Jamii wa Vodacom Tanzania Yessaya Mwakifulefule akiteta jambo na mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lipuri iliyopo kata ya Kalenga mkoani Iringa Agness John,mara baada ya kukabidhi msaada wa madarasa mawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 29 yaliyojengwa na Vodacom Tanzania kupitia mfuko huo.Akishuhudia watatu kutoka kulia ni Mkuu wa shule hiyo Alex Mwakiyanga akiwa na walimu wa shule hiyo.
Afisa Elimu wa Sekondari za Wilaya ya Iringa William Mkangwa akikata utepe kuashiria kupokea msaada wa madarasa mawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 29 yaliyojengwa na Vodacom Tanzania kwa kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii”Vodacom Foundation”kwa ajili ya shule ya sekondari ya Lipuri, iliyopo kata ya Kalenga mkoani Iringa, wakishuhudia kutoka kushoto ni Mkuu wa Vodacom Foundation Yessaya Mwakifulefule,Mkurugenzi wa Vodacom Kanda ya kusini Jackson Kiswaga,Diwani wa kata ya Kalenga Ameria Galinoma na diwani viti maalum Shakila Kiwanga.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kusini Jackson Kiswaga akiongea na wazazi na wanafunzi wa kata ya Kalenga Mkoani Iringa wakati wa hafla ya kuwakabidhi msaada wa madarasa mawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 29 kwa shule ya sekondari ya Lipuri ya mkoani humo ,yaliyojengwa na Vodacom Tanzania kupitia mfuko wa kusaidia jamii”Vodacom Foundation”Kulia ni Afisa Elimu wa Sekondari za Wilaya ya Iringa William Mkangwa na Mkuu wa Vodacom Foundation Yessaya Mwakifulefule.


Haya ndiyo madarasa mawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 29 yaliyojengwa na Vodacom Tanzania kwa kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii”Vodacom Foundation” kwa ajili ya shule ya sekondari ya Lipuri ya mkoani Iringa.

Sunday, November 20, 2011

JK atua na siri yake Dodoma

Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema) Mh. John Shibuda mara baada ya kuwasili mjini Dodoma Jumamosi jioni tayari kwa vikao na mikutano ya chama tawala. PICHA NA IKULU


Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili mjini Dodoma juzi jioni tayari kwa vikao muhimu vya chama hicho tawala vitavyofanyika kwa siku nne katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM maarufu kama White House.


Baada ya mapumziko mafupi katika Ikulu ndogo ya Dodoma Dkt Kikwete alielekea ukumbi wa St. Gaspers ambako aliongea na wabunge wa CCM na kupata nao chakula cha usiku.

Katika hotuba yake, Dkt Kikwete aliwapa changamoto wabunge hao wa CCM waende kwa wapiga kura wao na kuwaelemisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya uliopitishwa Jumamosi Bungeni Dodoma.

Kikwete aliwasisistizia wabunge hao umuhimu wa kupeleka elimu hiyo ya mchakato wa kupata katiba mpya kwani hivi karibuni kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa nini kinachoendelea, na kusema kuwa wakiwa wabunge wa chama tawala ni wajibu wao kuelimisha umma kwamba kanuni na sheria zote zimefuatwa katika kupitisha muswada huo ambao umesomwa kwa mara ya pili, baada ya kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa sheria.

Rais Kikwete aliwakumbusha wabunge hao kwamba mchakato huo si jambo geni na kwamba ndio uliofuatwa na Marais wote toka wa awamu ya Kwanza hadi ya tatu, akisisitiza kwamba ni muhimu wanancho wote wakaelewa hilo, ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya watu wachache wanaotaka kupotosha umma kwamba hatua hiyo ni batili wakati sio kweli, ikizingatiwa kwamba kila lililo katika katiba ya sasa limezingatiwa.

Pia aliwasihi Watanzania kujitokeza kutoa maoni yao ya ni katiba gani wanayoitaka pindi muda wa kufanya hivyo utapowadia, na wasikubali kughiribiwa na wachache waliopania kupindisha ukweli.

Kwa mujibu wa ratiba leo Jumapili kutakuwa na Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ukumbi wa White House kitachofanyika kutwa nzima, kitachofuatiwa na kikao cha Kamati kuu ya CCM Jumatatu na Jumanne. Halmashauri kuu ya CCM itakutana kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

Mzee Nterege: Miaka 103 ana watoto 57, wajukuu 200, vitukuu 70
Diwani na Babu

*AOA WANAWAKE SITA, AJENGA SHULE KUSOMESHA FAMILIA YAKE

KWA mara ya kwanza niliposikia habari za mzee Nterege Nyigana Mutari ana umri wa miaka 103, ana watoto 57, wajukuu 200 na vitukuu 70, sikuamini.

Nilijiuliza maswali mengi moja likiwa ni kwanini mzee huyo asiwemo katika kitabu cha maajabu ya dunia? Hiki ni kitabu ambacho huchapishwa kila mwaka kikiwa na mkusanyiko wa rekodi za dunia kuhusu mafanikio ya binadamu pamoja na maajabu mbalimbali.

Kuishi miaka 103 na kuwa na watoto 57 sio jambo dogo, watoto ambao nao wanakuletea wajukuu 200, na wajukuu nao wanakuletea vitukuu 70.

Na kama hiyo haitoshi, unaamua kujenga shule ili wapate elimu bora, tena katika shule hiyo yenye wanafunzi 744, wanafunzi 200 wanatoka katika familia yake, wakiwemo wajukuu na vitukuu. Sasa mzee kama huyu, kwanini asiwemo katika maajabu ya dunia?

Baada ya kufikiria mambo mengi niliamua kumtafuta mzee Nterege ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Nyamaitagi, kijiji cha Nyamakobiti, kata ya Majimoto Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Mzee huyu mcheshi ambaye ni wa kabila la Wangoreme anaishi umbali wa kilometa 70 kutoka makao makuu ya wilaya ya Serengeti, mjini Mgumu.

Historia ya Mzee huyo imejaa mengi yakiwemo machungu na raha, lakini kwa upande wake anasema vikwazo katika maisha ni jambo la kawaida.

“Nina miaka 103, wajukuu zaidi ya 200 na vitukuu zaidi ya 70, nilizaa watoto 57 lakini ninachoweza kuieleza jamii ni kwamba watoto wangu nimeamua kuwapa elimu bora kwa kuwa elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu hapa duniani,” anasema Nterege.

Maisha yake

Nterege alizaliwa mwaka 1908 lakini akajulikana kwa jina la "Reterenge’’, jina ambalo anasema alipewa na daktari raia wa Ujerumani.

Anasema alizaliwa katika eneo la Kyehonda -Kimeli ambalo kwa sasa ni eneo la kijiji cha Nyamutita na kwamba wakati huo baba yake alikuwa na wake wawili.

“Kwa upande wa mama yangu tulizaliwa wawili tu, mimi na dada yangu ambaye anaitwa Nyakimaiga, mama yetu alikuwa mke wa pili wa baba,” anasema Nterege.

Anasema mwaka 1918 baada ya baba yake kufariki dunia, ndugu wa baba yake walichukua mifugo yote iliyoachwa na baba yake wakiwemo Ng’ombe zaidi ya 100, na kuwanyang’anya nyumba waliyokuwa wakiishi na mama yao.

“Walitufukuza pamoja na mama kwa kuwa alikuwa mke mdogo wa marehemu baba, walisema kuwa mama yetu wa kambo ambaye alikuwa mke mkubwa ndio alikuwa na haki ya kupata kila kitu. Kuanzia hapo tulianza kuishi kwa shida.”

Anasema baada ya tukio hilo alianza maisha ya kujitegemea ambayo yalimfanya ashindwe kwenda shule na kujikita katika kilimo na wakati mwingine kufanya kazi ya kuchunga mifugo ya watu mbalimbali ili kupata fedha za kuweza kujikimu.

“Mwaka 1937 nilioa mke wa kwanza, Wansama Moremi ambaye kwa sasa ni marehemu nilihamia eneo la Nyamakobiti kuanza maisha mapya ya ndoa…, mke wangu nilimtolea maali ya Ng’ombe kumi niliowanunua baada ya kuuza Ulezi niliolima kati ya mwaka 1935 na 1936,” anasema Nterege.

Wazo la kuwa na familia kubwa

Anasema katika maisha yake mapya baadhi ya mambo yaliyokuwa yanamsumbua, ilikuwa ni jinsi gani angeweza kupata watoto wengi kwa kuwa alizaliwa yeye na dada yake tu.

“Wakati ule kuwa na familia au ukoo mkubwa kilikuwa kitu cha heshima katika mila zetu,” anasema Nterege.

Pia, anasema ukubwa wa familia ulikuwa muhimu ili kuweza kupambana na vitendo vya wizi wa mifugo ambapo mara kwa mara kuliibuka mapigano ya kikabila kati ya kabila lake na Wakulya na Wangoreme.

“Maisha ni mapambano. Nilianza kufanya biashara ya mifugo mwaka 1940 nikishirikiana na Chifu Makongoro wa Waikizu. Nilipata Ng’ombe 800 wa kwangu mwenyewe ila kwa sasa wamebaki 220 baada ya kuwapa watoto wangu kwa ajili ya kuanza maiasha yao ya kujitegemea,”

Kuoa

Akizungumza wanawake aliowaoa Nterege anasema,
“Nilioa wanawake saba lakini niliodumu nao ni sita, wanawake hao sita walizaa watoto 57, ila watoto waliopo hai ni 37,”.

Anaongeza, “Watoto wangu 20 walifariki kutokana na kwamba wakati huo vituo vya kutoa huduma ya afya vilikuwa mbali,”.

Anasema kuwa ana wajukuu zaidi ya 200, vitukuu zaidi ya 70 na anafafanua ,” Wengine siwatambui hata kwa majina,”.

Anasema mwaka 1937 alimuoa mke wake wa kwanza, Wansama Moremi, Gasawa Mayengo (1939),Mandala mwita (1953), Nyamhanga Nyamani (1963), Odela Osole (1969), Nyambura Paka (1965) na Mkami Myangosira (1974) ambaye waliachana bila kuzaa mtoto.

Anasema mpaka sasa wake zake walio hai ni wawili ambao anaishi nao na anawataja kuwa ni Nyamhanga Nyamani na Nyambura Paka.

Nterege anasema jambo kubwa analojivunia ni kumwona mtoto wake wa mwisho, Julius akisoma elimu ya sekondari ambapo alimaliza mwaka juzi.

Anasema kaka yake Julius anayeitwa Nyamanko alimaliza sekondari mwaka 1990, na wajukuu zake watano nao wamemaliza elimu ya sekondari ambao ni Gesile(2003), Bonifasi (2009), Nyakimaiga (2011).

“Kuna mmoja anaitwa Nyamitari bado yupo kidato cha tatu kwenye shule ya Sekondari ya Busawe, shule ambayo nilichangia ujenzi wake,” anaeleza kwa kujivunia kwa kitendo chake cha kuchangia maendeleo ya jamiii.

Anasema watoto wake 19 ambao wako hai ni wa kike na wa kiume 18. Mtoto wake wa kwanza anaitwa Mayengo na alizaliwa mwaka 1942.

Kujenga shule

Mzee Nterege ambaye bado ana kumbukumbu ya mambo mengi licha ya kuwa na umri mkubwa anasema kuwa mwaka 1988 baada ya kuona wajukuu zake wakipata usumbufu wa kwenda shule zilizokuwa vijiji vya mbali, aliamua kubuni wazo la kuanzisha shule ya msingi kuondoa usumbufu huo.

Anasema alianza ujenzi wa shule kwa kutumia magari yake kubeba mchanga na kokoto huku akiwahamasisha wakazi wa kijiji hicho kuchangia ujenzi.

“Ilikuwa ngumu kuwashawishi kwa kuwa kipindi hicho watu walikuwa hawapendi kuelezwa habari za kuchangia fedha kwa ajili ya jambo fulani.

Anasema kwamba mwaka 1990 alifanikiwa kumaliza ujenzi wa jengo la utawala kwa nguvu zake pamoja na wananchi.

“Licha ya kuwa mimi sikusoma niliamua kujenga shule ili wajukuu zangu wapate elimu. Elimu ndiyo kila kitu. Huwezi kufanikiwa katika maisha ya sasa bila elimu. Niliona wajukuu zangu wasiposoma watakuwa watumwa na tegemezi,” anaeleza Nterege.

Anasema mwaka 1991 shule hiyo ya msingi iliyopewa jina la Nayamakobiti ilifunguliwa kwa usajili namba PS 0904080 ikiwa na eneo la ukubwa wa Hekta 9.5.

“Shule hii niliamua kuiita jina la kijiji badala ya jina langu kwa kuwa sikutaka sifa katika suala hili, mtu unatakiwa usifiwe ukiwa umekufa si ukiwa hai,” anasema Nterege.

Mkuu wa shule hiyo anasemaje

Akizungumzia historia ya shule hiyo mkuu wa shule hiyo, Machumbe Mairo anasema kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya shule hiyo bila kumtaja mzee Nterege.

Anasema shule hiyo ina wanafunzi 744 na anafafanua kwamba pamoja na changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na uhaba wa walimu.

Pamoja na matatizo hayo alisema inafanya vizuri ambapo wanafunzi wengi hufaulu kuendelea kidato cha kwanza.

“Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010 shule hii imeweza kufaulisha wanafunzi 122 kwenda sekondari, wasichana wakiwa ni 41 na 81 wakiwa ni wavulana,” anasema Mairo.

Anasema wanafunzi 200 wa shule hiyo kati ya wanafunzi 744 wanatokea katika familia ya mzee Nterenge wa kiwemo wajukuu na vitukuu.

“Familia yake ni kubwa kweli yaani hapa kijijini wako wengi. Ukienda vijiji jirani pia wapo,” anasema.
Imeandikwa na Renatus Masuguliko. SOURCE: MWANANCHI.

Tuesday, November 08, 2011

JK awaandalia dhifa ya kitaifa Prince Charles na Duchess of Cornwall

Rais Dkt Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete wakiwa na wageni wao Prince Charles na Duchess of Cornwall katika dhifa ya kitaifa waliyoandaa kwa heshima ya mtoto huyo wa Malkia wa Uingereza na mkewe usiku huu Ikulu jijini Dar es salaam.

Prince Charles akisalimiana na binti wa Rais Kikwete wakati wa hafla hiyo
Glasi zikigongwanishwa meza kuu.
Rais Jakaya Kikwete akisalimia baadhi ya maofisa walioongozana na Prince Charles
Ngoma za utamaduni zilirindima katika hafla hiyo
Rais Jakaya Kikwete akiongea na Sir Andy Chande
Katibu Mkuu Kiongozi Mh Philemon Luhanjo (kushoto) akiwa na Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Dkt Mwinyihaji Makame na Balozi wa Tanzania nchuni Uingereza Mh Peter Kallaghe katika dhifa hiyo
Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo (kushoto) akiongea na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Paul Rupia

Mkuu wa Majeshi ya Tanzania Jenerali Davies Mwamunyange akiongea na Brigedia Potts na Ms Dinah Potts kwenye hafla hiyo


Katibu Mkuu Kiongozi Mh Philemon Luhanjo (kushoto) akiwa na Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Dkt Mwinyihaji Makame na Balozi wa Tanzania nchuni Uingereza Mh Peter Kallaghe katika dhifa hiyo