Wednesday, December 30, 2015

TCRA YAZICHUKULIA HATUA ZA KISHERIA KAMPUNI ZA SIMU ZILIZOSHINDWA KUWALINDA WATEJA WAKE KITEKNOLOJIA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Ally Simba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na makampuni ya simu  za mkononi ya Tigo, Airtel, Halotel na Zantel na Smart kwa kuto kukidhi vigenzo. Pia amesema kuwa Makampuni hayo yamepigwa faini ya shilingi milioni 25 kwa mamlaka ya mawasiliano Tanzania kabla ya Januari 29 mwakani.
Mwanasheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Elizabeth Zagi akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Ally Simba jijini Dar es Salaam leo.
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.

JAMHURI YA YA MUUNGANO YA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

HATUA ZA KISHERIA NA KIUDHIBITI KWA MAKAMPUNI YA SIMU YALIYOSHINDWA KULINDA WATEJA WAKE KITEKNOLOJIA NA KISHERIA KUHAKIKISHA USALAMA WA MAWASILIANO YAO

1. Katika shughuili zake za udhibiti wa huduma za mawasiliano nchini, Mamlaka ya Mawasilaino Tanzania imepokea malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi ya kuwepo mazingira yasiyo salama katika huduma za mawasiliano na hivyo kusababisha kufanyika kwa vitendo vya utapeli unaofanywa kwa kutuma jumbe za udanganyifu na kulaghai, hivyo kusababisha watu kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu. Kwa mfano kupokea ujumbe kutoka namba unayoifahamu ukikuagiza utume fedha au ujumbe wa kashfa au matusi wakati hautoki kwa mhusika mwenye namba. Mamlaka imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja na malalamiko mengine hupelekwa Polisi. Kwa miezi miwili tu, matukio 42 yameripotiwa Polisi pamoja na TCRA ambayo tukio moja tu linakuwa na ulaghai wa takribani milioni 25 peke yake.

2. Tarehe 16 Oktoba, 2015 Mamlaka iliwakumbusha watoa huduma za simu nchini juu ya wajibu wao kuchukua hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya utumaji wa jumbe za kilaghai na kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao kutumika kutuma jumbe za udanganyifu na kulaghai. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mamlaka tarehe 16 Desemba, 2015 Mamlaka ilibaini kuwa  kampuni za Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart), MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo), Airtel Tanzania Limited, Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel) and Zanzibar Telecom Limited inayojulikana kama Zantel) zimeshindwa, zimepuuzia na zimekataa kufuata maagizo ya Mamlaka kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao kutumika kutuma jumbe za kilaghai kinyume na Kanuni Na.8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011 [the Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011].

3. Tarehe 18 Disemba, 2015 Mamlaka iliwaamuru watoa huduma za mawasiliano waliotajwa hapo juu kufika mbele ya Mamlaka na kujieleza kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao kwa kuvunja sheria na kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielectroniki na Postal ya Mwaka 2011 [the Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011] kwa kushindwa kuweka mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.

4. Watoa huduma walifika na kutoa maelezo ya utetezi kati ya tarehe 21 na 23 Desemba, 2015.

5. Baada ya kuwasikiliza na kutilia maanani utetezi wa watoa huduma na kwa mujibu wa uchunguzi na majaribio uliofanywa na Mamlaka, Mamlaka imejiridhisha kuwa mitandao ya watoa huduma waliotajwa hapo juu haikuwa salama na kuwa watoa huduma hao walishindwa kufuata maelekezo ya Mamlaka juu ya kuweka mazingira salama katika huduma wanazotoa. Hivyo Mamlaka imejiridhisha kuwa watoa huduma wamekiuka matakwa ya Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielectroniki na Postal ya mwaka 2011 (The Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011) inayowataka watoa huduma kuweka mazingira ya mitandao salama kwa kuchukua hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya uhalifu ikiwa ni pamoja na utumaji wa jumbe za kilaghai kupitia mitandao yao.

6. Kwa mujibu wa Kifungu cha 17 cha Jedwali la Pili katika Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 ya Sheria za Nchi, kinachoipa Mamlaka uwezo wa kutoa adhabu kwa Wenye Leseni dhidi ya uvunjifu wa Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni, Mamlaka ya Mawasiliano imetoa:

A. Onyo kali kwa Kampuni za:
(i) Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart),
(ii)  MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo),
(iii)  Airtel Tanzania Limited,
(iv)  Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel), na 
(v) Zanzibar Telecom Limited (inayojulikana kama Zantel). 

kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Postal ya mwaka 2011  [the Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011] kwa kushindwa kuweza mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.

B. Imeamuru Kila Kampuni husika:
(i)   Kuhakikisha kuwa, kuanzia siku ya kutolewa kwa amri hii, inaweka mazingira salama katika mtandao wake yatakayozuia utumaji wa jumbe za kilaghai (yaani ‘spoofed messages’) na matishio mengine ya kiusalama;
(ii)   Kulipa faini ya Shilingi za Kitanzania Milioni Ishirini na Tano (Shs 25,000,000.00) kwa Mamlaka ya Mawasiliano kabla ya tarehe 29 Januari, 2016; na
(iii) Endapo Makamuni haya yatashindwa kutimiza amri Na.2 hapo juu, Mamlaka itachukua hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti dhidi ya Kampuni ya Simu husika.

7. Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inapeda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi kuwa makini na jumbe za kuwataka kutuma fedha bila ya kuwa na uhakika. Inashauriwa kuhakiki ujumbe husika kwa kupiga simu na kuongea na mhusika kabla ya kufanya maamuzi ya kutuma fedha hata kama namba inayotumika unaijua. Vilevile wawe makini wanapopokea jumbe zinazoonesha zinatoka kwa mtu fulani wanayemjua kumbe ni matapeli wanaotumia ulaghai kwa njia hii ya “spoofing”.

IMETOLEWA NA

Dkt. Ally Y. Simba
MKURUGENZI MKUU
30 Disemba, 2015

No comments: