Tuesday, December 15, 2015

WAZIRI WA WIZARA YA ULINZI MH. HUSSEIN MWINYI ARIPOTI KAZINI

HU4
Dk. Hussein Mwinyi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akisalimiana na  Maofisa mbalimbali wa jeshi na  watumishi  katika Wizara  ya Ulinzi mara baada ya kupokelewa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange kushoto na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mh. Job Masima katikati katika makao makuu ya JWTZ Upanga jijini Dar es salaam.
……………………………………………………………………………………………….
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Hussein Ali Mwinyi (Mb), aliyeteuliwa na kisha kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri jeshi Mkuu ameripoti ofisini na kuanza kazi rasmi.
Alipowasili ofisini kwake alilakiwa na Naibu Katibu Mkuu, Mkuu wa Majeshi Mnadhimu Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, wanajeshi na watumishi wa Umma wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Job Masima waliojipanga nje ofisi.
Akiongea na Menejimenti, alisema matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuongeza ufanisi, kupunguza urasimu pamoja kupunguza matumizi ya matumizi ya serikali pasipo kuathiri utendaji kazi.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufanya kazi kwa kasi mpya ambapo Wizara yake nayo inahitaji kuendana nayo.
Kwa awamu iliyopita Wizara ilitekeleza majukumu yake ya msingi ya Ulinzi wa Mipaka na pamoja na kusaidia Mamlaka za Kiraia pale ilipohitajika kufanya hivyo kwa mafanikio. Kwa sasa kinachotakiwa ni kuendelea kufanya maboresho katika utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi.
Licha ya kufanya kazi kwa ufanisi, alikiri kuwa bado zipo changamoto chache zinazoikabili Wizara hii, ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka iwezekanavyo.
Akizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na idadi ndogo ya Vijana wanojiunga na JKT kwa Mujibu wa Sheria, ikilinganishwa na wanohitimu Kidato cha Sita, uboreshaji ya Mashirika yaliyo chini ya Wizara pamoja na migogoro ya ardhi inayotkana na aidha watu kuvamia maeneo ya Jeshi au kuchelewa kutoa fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao.
Waziri mwinyi ni miongoni mwa mawaziri waliokuwa kwenye Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne.  Na Awamu hii ya Tano ameteuliwa kwa mara nyingine kuingoza Wizara hii. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ulinzi na JKT
14 Disemba, 2015
Post a Comment