Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Mandawa wilayani Ruangwa kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo desemba 22, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akimtambulishasha diwani wa kata ya Mandawa kwa tiketi ya CUF, Said Abdallah `Nachinga na kuahidi kuwa atashirikiana nae kwa karibu katika kazi za kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo bila kujali tofauti za vyama. Alikuwa katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mandawa Desemba 22, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema darala la mto Mbwemkuru lililoko katika barabara ya kutoka Chikwale hadi Liwale litakamilika kwa sababu ni kiungo muhimu kwa wakazi wa eneo hilo.
Ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nangurugai katika kata ya Mbwemkuru wilayani Ruangwa, mkoani Lindi ambako alikwenda kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mbunge wao.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja za diwani wa Nangurugai, Bw. Selemani Likuche aliyetoa ombi la kutengenezwa kwa daraja hilo kwani limekata mawasiliano baina ya kijiji hicho na wilaya ya Liwale. Pia aliomba wapatiwe dawa na watumishi kwenye zahanati yao.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema kazi ya ujenzi wa daraja hili itakamilishwa kwa sababu jukumu kubwa alilonalo ni kuhakikisha ujenzi wa daraja la mto Mbwemkuru unaisha.
Pia aliitaka Halmashauri ya Ruangwa isimamie uboreshaji wa barabara ya kutoka Nangurugai hadi Chikwale yenye urefu wa km. 35 kwa sababu ni muhimu kwa kusafirisha mazao ya eneo hilo. “Hili eneo ni maarufu kwa zao la ufuta, kwa maana hiyo linaongeza pia mapato ya Halmashauri, simamieni hii barabara ili wananchi wasisumbuke kuuza mazao yao,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ruangwa, Bw. Nicholas Kombe alisema milingoti (pillars) ya daraja hilo ilikwishajengwa walikuwa wakisubiri kupokea vyuma vya kutandaza juu ya daraja. “Tulikwishapeleka maombi yetu TANROADS na TAMISEMI lakini bado hawajatujibu,” alisema.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa dawa kwenye zahanati yao, Waziri Mkuu alisema ameshaongea na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye amemhakikishia kuwa ameanza maboresho ya upatikanaji dawa katika zahanati zote. Kuhusu tatizo la watumishi wa sekta ya afya, Waziri Mkuu
aliahidi kuwa watapatikana katika muda mfupi.
aliahidi kuwa watapatikana katika muda mfupi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo, alimweleza mwandishi wa habari hii kwamba ameanzisha mfumo wa ukaguzi na udhibiti wa dawa zinazoletwa kwa kutumia leja (ledger) tangu zinapoingia stoo hadi kwenye chumba cha kutolea dawa.
“Kosa la kitakwimu halina msamaha, mtumishi akikosea kuoanisha mahesabu (tallying) anapaswa kujaza commitment form na sisi tunachukua hatua kuanzia hapo,” alisema Dk. Simeo.
“Pia nimeunda Kamati ya Wilaya ya Ukaguzi wa Dawa ya Idara ya Afya kwa vituo vyote vya afya na zahanati ambayo hufanya ukaguzi mara moja kila baada ya miezi miwili. Hii inasaidia kufanya re-distribution ya dawa kwa zahanati zenye upungufu,” alisema.
Dk. Simeo alisema maboresho mengine anayofanya ni kudai taarifa za mwezi ambazo ametaka zimfikie tarehe 5 ya kila mwezi. “Nina zahanati 28, vituo vya afya vitatu na hospitali ya wilaya moja, hizi ni taarifa 32 ninazopokea kila mwezi na ninaipitia kila moja ili kujiridhisha licha ya kuwa zimetoka kwa wasaidizi wangu. Inanisaidia kupata picha halisi ya utendaji kazi,” alisema.
Comments