Wednesday, December 30, 2015

AFISA BIASHARA WA HALMASHAURI YA DODOMA ASIMAMISHWA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS


Anuani ya Simu “TAMISEMI” DODOMA
Simu Na: (026) 2322848, 2321607, 
                            2322853, 2322420,
Nukushi: (026) 2322116,  2322146.
                             2321013,      
Barua pepe:ps@poralg.go.tz
Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa,
S. L. P. 1923,                         DODOMA.
  

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. George Simbachawene amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuwasimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Dodoma Bw. Elias N. Kamara na  Bibi Donatila D. Vedasto (Afisa Biashara) kuanzia leo tarehe 30/12/2015 kwa kosa la kusababisha urasimu katika utoaji wa leseni za biashara.

Kutokana na hali hiyo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kumuondoa kwenye nafasi yake Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa na Msaidizi wake na nafasi zao kukaimishwa kwa watu wengine ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa dhidi yao.

Agizo hili limetolewa na Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara ambayo yalionyesha kuwepo kwa mazingira ya rushwa.

Katika uchunguzi ambao umefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imegundulika kuwa kulikuwa na maombi ya leseni 750 ambayo yalikuwa hayajashughulikiwa bila sababu za msingi na hali hiyo ilipelekea kuikosesha Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kiasi cha shilingi Milioni 75.

Aidha, Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ameagiza Mamlaka za Serikali kote nchini kuhakikisha wanatoa leseni za biashara bila urasimu wowote na muombaji apate leseni ndani ya siku 2 au 3 anapoomba leseni.

Mhe. Simbachawene ametoa agizo kwa Maafisa biashara wote nchini kuacha urasimu katika kutoa leseni na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Imetolewa na:
Rebecca Kwandu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais - TAMISEMI
30 Desemba, 2015

No comments: