Thursday, December 31, 2015

BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO KUANZISHA OFISI ZA KANDA

tab1
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Robert Pascal (Kulia) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa Benki, Bibi Neema Christina John (aliyevaa miwani) wakati wa uhakiki wa fomu zilizojazwa na moja kati ya vikundi vilivyofanikiwa kupata mkopo kutoka Benki hiyo.
tab2
Mwanasheria mwandamizi wa TADB, Bibi Salome Masenga (Kulia) akimuelekeza mmoja wa wanakikundi waliopata mikopo kutoka Benki hiyo.
tab6
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas Samkyi (Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Kasunga (Kulia).
tab7tab10Picha ya pamoja
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Iringa
Benki mpya ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema hadi kufikia miaka mitano ijayo itakuwa imefungua ofisi sita za kikanda zenye lengo la kuwahudumia wakulima nchi kote.
Mikakati hiyo iliwekwa bayana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Bibi Kurwijila alisema kuwa TADB inalenga kutelekeza kwa vitendo Maelekezo ya Serikali ya kupunguza changamoto zinazowakabili wakulima nchi kote.
Aliongeza kuwa kwa sasa Benki inalenga kusambaa nchi nzima kwa kuanzisha Ofisi za Kikanda ndani ya miaka mitano ijayo.
“Tunalenga kuwafikia wakulima wote nchini kadri siku zinavyoendelea kwenda na kutegemea mtaji unavyoongezeka ama upatikanaji wa fedha toka vyanzo mbali mbali ili kuweza kuwawezesha kumudu shughuli zao za kilimo,” alisema.
Aliongeza kuwa Benki inaleenga kuwajengea uwezo na kuanzisha Programu Maalumu ya Vijana wajihusishao na shughuli za Kilimo cha kibiashara na kushirikiana na wadau wengine kuhuisha shughuli za umwagiliaji na miradi ya kisasa ya umwagiliaji.
Malengo mengine ni kutafuta fedha toka vyanzo mbalimbali zenye gharama nafuu kwa minajili ya kuwakopesha Wakulima katika hatua zote za mnyororo wa ongezeko la thamani kwenye mazao ya Kilimo na kupanua wigo wa utaoji mikopo toka Minyororo Kumi na Minne (14) ya Mwanzo na kuhusisha pia mazao mengine ya Kilimo na pia kuwaunganisha Wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi amesema kwamba Benki yake imedhamiria kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini ili kuchagiza na kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Bw. Samkyi alisema TABD imejizatiti kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza tija na upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu maalum kwa sekta ya kilimo, kama njia ya kuleta Mapinduzi yenye tija kwa wakulima nchini.
“Benki imejipanga kutoa mikopo yenye riba nafuu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo,  wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika tasnia za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji nyuki),” alisema Bw. Samkyi.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba kwa kuanzia walengwa wakuu wa TADB ni wakulima wadogo wadogo, hatahivyo, hata wale wakulima wa kati na wakubwa watahudumiwa.
Bw. Samkyi imejidhatiti katika kufanya tathmini ya kina katika mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi kwa minajili ya kuongeza thamani na ushindani kwenye masoko.
“Sera ya TADB ni kutathmini mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi, na ambayo utatuzi wake utaongeza tija na uwezo wa ushindani kwenye masoko, na hivyo kukuza uchumi wa walio wengi na kupunguza umaskini,” aliongeza.
Katika hafla hiyo, jumla ya vikundi nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo wadogo 857, vilimiza vigezo na kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Kwa mujibu wa Bw. Samkyi kabla ya kutoa mikopo hiyo, benki iliwatembelea na kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla ya vikundi 89 vyenye jumla ya wanakikundi 21,526 vilifikiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mama Amina Masenza amewaasa Wakulima wote nchini kutumia vizuri mikopo wanayopewa ili kuweza kutimiza malengo yao binafsi na ya Serikali katika kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania.
Mama Masenza alisema kuwa wakulima wakitumia mikopo waliyopewa kwa malengo husika watafika mbali na kuweza kuchagiza mikakati ya Benki hiyo katika kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kilimo kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
“Naamini, wakati Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapoanza kufanya tathmini ya mikopo hii iweze kuona matunda ya uwekezaji wake hasa kwa nyie ambao mmeweza kubahatika kupata fursa ya awali kabili kunufaika na huduma za TADB,” aliwasihi.
Mama Masenza aliwaomba  wakulima hao kuwa Mfano Bora na wanaojitambua vilivyo, hasa nia ya kutoka katika kiwango fulani cha maisha kwenda katika hatua nyingine za juu zaidi kimaisha kwa kuongeza kipato na ubora wa kimaisha kwa ujumla kupitia huduma za TADB.
“Nawasihi kutotumia pesa hizi kinyume na malengo yaliyokusudiwa, kwani kwa kufanya hivyo, siyo tuu tunaiua Benki yetu bali pia tunajimaliza wenyewe kiuchumi. Wito wangu kwenu ni kujipanga kwa dhati ili kuweza kutimiza malengo makuu ya mikopo hii ambayo ni kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” aliongeza.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, mnamo tarehe 8 Agosti 2015 mjini Lindi. Uanzishwaji wa Benki hii ni utekelezaji wa malengo ya muda mrefu ya Serikali, katika kuitikia wito wa wananchi na wadau wengine wa maendeleo ili Tanzania iweze kupiga hatua endelevu za kimaendeleo.

No comments: