Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akitoa hotuba kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza(hawapo pichani) kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016. Baraza hilo limefanyika Desemba 31, 2015 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Magereza wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza wakati akitoa hotuba yake kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakiwa timamu kumpokea Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(hayupo pichani) wakati akiwasili tayari kwa kulihutubia Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
Maafisa ngazi ya juu wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini hotuba fupi aliyoitoa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).
…………………………………………………………………………………………………
Na Lucas Mboje, Dar es Salaam
WATUMISHI wa Jeshi la Magereza wametakiwa kuzingatia utendaji kazi wenye tija mahala pa kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea(Business as usual).
Rai hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja wakati akizungumza kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini, Dar es Salaam.
Jenerali Minja amewaagiza Watumishi wote wa Jeshi hilo kuhakikisha kuwa wanawajibika kwenye maeneo yao ya kazi ili kufikia ufanisi uliotarajiwa pamoja na kutumia vizuri rasilimali za Ofisi kwa manufaa yaliyokusudiwa.
“Utekelezaji wenu wa kazi za kila siku lazima uwe na tija na uendane sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ili kufikia ufanisi unaotarajiwa”. Alisema Jenerali Minja.
Aidha Jenerali Minja amezungumzia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka 2015 ambayo ni pamoja na kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Magereza ambayo italiwezesha Jeshi hilo kutekeleza mpango wake wa Maboresho ya maeneo mbalimbali, kusainiwa kwa Mkataba na Kampuni ya Poly Teknology ya China itakayojenga nyumba 9,500 za Makazi ya Maafisa na Askari, kusainiwa kwa Mkataba wa Magari 9,05 na Kampuni ya Ashok Leyland ambapo magari hayo yanatarajiwa kupokelea mapema mwakani.
Mafanikio mengine ni pamoja na Usajili wa kudumu wa Chuo cha Urekebishaji ambapo Chuo hicho kitatoa elimu stahiki ya Urekebishaji itakayotambulika ndani na nje ya Nchi, Jeshi la Magereza limepeleka Maafisa wake kwenye shughuli za Ulinzi wa Amani kwenye nchi mbalimbali zenye migogoro, Jeshi limeingia ubia na Wawekezaji mbalimbali katika miradi ya Kilimo, uchimbaji madini ya chokaa, ujenzi wa maduka makubwa(shopping Malls) katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro ambapo miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa Jeshi.
Vilevile Jeshi limefanikiwa kuandaa Maandiko mbalimbali ikiwemo andiko la kujitosheleza kwa chakula na miradi minane ambayo miradi hiyo ikiwezeshwa inaweza kuongeza thamani za mali zinazozalishwa na Jeshi hilo.
Aidha Jenerali Minja alieleza changamoto mbalimbali ambazo Jeshi hilo linakabilianazo ambazo ni ufinyu wa bajeti, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri, ukosefu wa zana za kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kuathiri Uzalishaji, tatizo la miundombinu ya magereza na msongamano magerezani hali inayopelekea kwa kiasi fulani kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja ametoa Salaam za kheri ya Mwaka mpya 2016 kwa Watumishi wote wa Jeshi hilo na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotawala uendeshaji wa Jeshi la Magereza.
Comments