Tuesday, December 29, 2015

TANROADS KUENDELEA NA UJENZI WA BARABARA YA KAMANGA

TANROAD MWANZA 11
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa Barabara itokayo Kamanga Ferry kuelekea Sengerema kwa kiwango cha lami ili kurahisisha  usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Hayo yamesemwa leo na Meneja wa TANROADS Mkoa wa  Mwanza Mhandisi Leonard Kadashi alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa Habari ofisi kwake kutolea ufafanuzi suala la Barabara ya Kamanga Ferry mpaka Sengerema ambayo haipo katika hali nzuri na kusema mkandarasi yupo na ujenzi huo unaendelea.
Pia amekanusha suala la kuwa Barabara hiyo imekuwa ikitumiwa na wanasiasa katika kampeni na kusema kuwa Barabara hiyo ipo katika mipango ya TANROADS na mkandarasi yupo katika ujenzi wake kwa kiwango cha  lami
.
“Barabara hii ya Kamanga Ferry tunaijua, tunaifanyia kazi na ipo katika matengenezo ila  ni mvua ndio zilikwamisha kwa muda ujenzi huu ila mkandarasi yupo katika ujenzi.” Alisema Mhandisi Kadashi.
Mbali na Barabara ya toka Kamanga Ferry mpaka Sengerema kujengwa katika kiwango cha lami pia TANROADS inazishughulikia Barabara za Kamanga mpaka Katunguru,Katunguru mpaka Sengerema na Bukoba mpaka Nyehunge.
Katika kurahisisha usafiri na usafirishaji nchini, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS) imefanikisha ujenzi wa Barabara nyingi nchini kwa kiwango cha lami na changarawe ambazo zimekuwa ni viungo vya nchi yetu na nchi jirani,Mikoa, Wilaya, Kata, Tarafa na vijiji katika kufanikisha usafiri na usafirishaji hasa katika sekta za kibiashara, na utalii pia kurahisisha mawasiliano hivyo kuleta maendeleo kwa wananchi na nchi kiujumla.

No comments: