Wednesday, December 16, 2015

KILOMBERO SUGAR: TUZO ZA ATE NI HAMASA KWA WAAJIRI

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa (Kulia) akimkabidhi kombe Meneja masoko wa kampuni ya sukari ya Kilombero Ephraim Mafuru baada ya kuibuka washindi wa tatu wa Jumla katika tuzo za muajiri bora wa mwaka zilizo andaliwa na chama cha waajiri Tanzania (ATE). Hafla hiyo ilifanyika Dar-es-Salaam, mwishoni mwa wiki. 

Kampuni ya Kilombero Sugar Ltd imesema kuwa tuzo za Mwajiri Bora zinazotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), zinachangia kwa kiasi kikubwa kuleta hamasa kwa waajiri na kupelekea kutoa huduma nzuri kwa wafanyakazi. 

Akizungumzia tuzo hizo zinazotolewa kila mwaka, Meneja Rasilimali watu wa Kilombero Sugar Beda Marwa Chacha amesema kuwa shindano hilo linasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wajiri kutimiza majukumu yao ili kuweza kujinyakulia tuzo.

“Napenda kuwaomba waajiri wenzangu kushirikiana na ATE ili kuwawezesha kuboresha tuzo hizo. Tutambue kwamba sisi ndio muhimili mkubwa wa kuweza kuwafanya wao waendelee kuwepo,” alisema Beda ambaye kampuni yake imekuwa imefanikiwa kuwa mshindi wa tatu wa jumla.Amesema kuwa kadri wanavyoshiriki wanaendelea kujifunza mambo mengi kwa waajiri wenzao na hivyo kuendelea kufanya maboresho na kuwaasa ATE kuendelea kupanua wigo wa mashindano hayo.

Aliwaomba wanachama wenza kuhakikisha wanaendelea kutoa michango ili kukifanya chama kiendelee kuwepo  na kusaidia kuwapa changamoto waajiri.Alisema kuwa Kampuni ya Kilombero Sugar imefanikiwa kupata tuzo kwa utoaji huduma bora kwa  wafanyakazi wake, juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI, utoaji huduma bora za maendeleo ya jamii na vilevile ushirikiano bora kwa wafanyazi pindi wawapo kazini.

Tuzo hizo zilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Baada ya kukabidhiwa tuzo, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero Ephraim Mafuru alisema:  “Tumekuwa karibu kwenye kila kinyang’anyiro lakini katika sehemu hizi zote tumekuwa bora sana”.

Katika kampuni hiyo Serikali inamiliki asilimia 20 ya hisa zote, Kilombero Sugar inamiliki asilimia 55 ya hisa zote za Kampuni (hisa kubwa kuliko zote), asilimia 25 inamilikiwa na ED&F Man, kundi ambalo makazi yake yako jijini London. Kampuni ya Sukari Kilombero inatoa ajira za kudumu kwa wafanyakazi  zaidi ya 4000. 

Ikiwa kama moja ya makampuni yanayotoa huduma bora zaidi za kijamii, kampuni imejenga hospitali iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 700 ambayo hutoa huduma zake bure kabisa kwa wakazi wa eneo hilo.Vilevile kampuni hiyo imejenga shule ya sekondari ambayo inachukua wanafunzi kutoka pande zote za nchi, ujenzi wa mabweni, miradi ya maji pamoja na vyoo vya shule.

Moja ya vitu vinavyounda Kampuni ya Sukari ya Kilombero ni mashamba makubwa kwa ajili ya kilimo na viwanda cha sukari vya Msolwa na Ruembe vilivyopo karibu na Mto Ruaha Mkuu ambao umeunganishwa na daraja dogo.

No comments: