Sunday, February 27, 2011

Ajali yaua Watano



WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 34 kujeruhiwa katika ajali ilihoyahusisha magari mawili ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Kahama na Dar-Es-Salaam na jingine Itigi –Dodoma.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa sita mchana eneo la Mbwanga karibu na mizani ya Tanroad ,nje kidogo ya mji wa Dodoma ilihusisha basi la kampuni Ally`s lenye namba T312 AUU lililokuwa likitokea Kahama kuelekea Dar-Es-Salaam ambapo liligongana na gari aina ya Coaster leny namba T896BGH ambalo lilikuwa likitokea Dodoma kuelekea Itigi wilayani Manyoni .

Kwa mujibu wa miongoni wa majeruhi wa ajali hiyo,chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa basi dogo ambaye alitaka kulipita gari jingine huku akiwa katika mwendo mkali.

Walisema alipokuwa akitaka kulipita gari jingine huku akiwa katika mwendo mkali,ghafla alikutana na gari jingine hivyo akaamua kukatisha barabara jambo ambalo lilisababisha dereva wa basi kubwa(ally`s) kujikuta ameligonga basi dogo ubavuni.

BONGO FLEVA WAITUNGUA BONGO MOVIE BAO 2-0

Mshambuliaji wa kushoto wa timu ya Bongo Freva,KR Mullah akimtoka mchezaji wa timu ya Bongo Movie katika mchezo uliopigwa jioni hii katika uwanja wa Taifa.
Timu ya Bongo Movie

Timu ya Bongo Freva
Wasanii wa filamu na wale wa muziki wa Bongo Flava jana walichuana katika mpambano wa mpira wa miguu ili kuchangia waathirika wa mabomu Gongo la mboto. Bongo Movies walilala bao 2-0.

Habari zaidi waweza kubonya hapaUpate tukio hilo kwa kina.


Thursday, February 24, 2011

Wahariri walipokutana na Mr Dowans

Hongera Mpangala kwa mchoro wako kiboko, maana expression zako katika mchoro hata kama tusingeipata picha basi katuni hii ingetusaidia kuitambua sura ya Mr Dowans

Tuesday, February 22, 2011

Mmomonyoko wa barabara Zenji


Wahenga walisema usipoziba ufa utajenga ukuta, pichani ni uchakavu wa ukingo wa bahari unaotishia kufunga barabara kuu kutoka Forodhani hadi bandarini mjini Zanzibar ambapo hivi sasa shimo kubwa limejitokeza juu ya barabara hiyo kiasi cha kuyafanya magari kupita eneo hilo kwa shida. Picha na Martin Kabemba.

Monday, February 21, 2011

Wake za viongozi wawatakia


Me wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda na mke wa waziri mkuu mstaafu Rejina Lowasa wakimjulia hali mgonjwa Mwajuma Jumanne miaka 25 mkazi wa Gongo la Mboto ambaye ameumia paja katika milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto wiki iliyopita. Picha naOfisi ya Waziri Mkuu.


Mke wa Waziri wa Ulinzi, Mariam Mwinyi ambaye ni miongoni mwa wake waviongozi akitoa pole kwa mwathirika wa mabomu Gongo la Mboto katika Hospital ya Amana.

NOMINEE WA KILI MUSIC AWARDS WATAJWA

Mratibu wa Tuzo za Kili 2011 kutoka Basata, Angello Luhala (kushoto) akipokea bahasha yenye majina ya nominees kutoka kwa Loyd Zhungu wa kampuni ya INNOVEX ambao wamepewa jukumu la kusimamia zoezi zima la uteuzi na upigaji kura za wasanii hao. Mpango mzima umefanyika leo katika ofisi za TBL.

President Kikwete in Ivory Coast

President Jakaya Mrisho Kikwete with South Africa’s President Jackob Zuma leave Noaukchott’s conference hall at the end of High Level meeting Panel for The Resolution of The Crisis in Ivory last night.
President Jakaya Mrisho Kikwete during the meeting of the High Level Panel For The Resolution of The Crisis in Ivory Coast held in Noaukchott, Mauritania yesterday. Others in the picture flanking the president are The Foreign Affairs Minister Bernard Membe, Burkina Fasso’s President Blaise Compaore and extreme left is South Africa’s President Jackob Zuma (picture by Freddy Maro)

Sunday, February 20, 2011

Athari za mabomu





ZAIDI ya mabomu 1,360, miongoni yakiwemo makombora, yamekusanywa Maofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ili kuondoa hatari ya kuwepo kwa milipuko mingine kwenye maweneo ya makazi ya watu.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), Luteni Kanali Kapambala Masoud Mgawe alisema kuwa, kazi hiyo imefanywa usiku kucha na askari hao ili kuzuia athari zilizojitokeza kwenye maeneo hayo.

Alisema, mpaka sasa askari hao bado wanaendelea na kazi hiyo kwenye maeneo tofauti yaliyoathirika na mabomu hayo.

“Askri bado wanaendelea na zoezi la kutafuta mabomu kwenye maeneo ya wananchi, hivyo basi tunawaomba watoe ushirikiano ikiwa ni pamoja

Aliongeza maeneo ambayo yameanza kufanyiwa kazi ni pamoja na Majohe, Gongo la Mboto karibu na kambi na Pugu, ambako ndiko kulikohathirika zaidi na mabomu hayo.

Alibainisha, kutokana na hali hiyo wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya hali ya mabomu hayo kwa sababu askari wapo kwa ajili ya kulishughulikia suala hilo ili lisiweze kuwaathiri wananchi na mali zao.

Kwa mujibu wa Mgawe, wananchi wasichezee mabomu hayo kwenye maeneo hayo, kwa sababu wanaweza kusababisha hatari, hivyo basi wametakiwa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika pindi wanapoyaona ili waweze kuyachukua.

Tuesday, February 15, 2011

Onyesho la wazi, bure la aina yake mara ya Kwanza nchini








Katika kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, na miaka mia moja ya siku ya mwanamke kimataifa, mbunifu nguli wa mavazi Tanzania, Mustafa Hassanali aliyebobea katika ubunifu wa mavazi ya jioni na Harusi, kwa kushirikiana na wabunifu waalikwa wa kimataifa toka Uingereza watafanya maonyesho ya mavazi tarehe 4-5 mwezi Machi mwaka huu, kwa lengo la kusaidia suala zima la uzazi salama nchini.

Akizungumzia maonyesho hayo, Mustafa Hassanali, ambae anaamini katika kuitumia mitindo kama njia mbadala ya kuchangia, kuhamasisha na kueneza taarifa kwa jamii zinazohusiana na masuala ya afya amesema”kwa kushirikiana na shirika la utepe mweupe la Tanzania kwa pamoja tumeamua kufanya maonyesho ya mavazi kwa siku mbili, lengo si tu kuonyesha mavazi ya Mustafa Hassanali kwa mwaka 2011, na utu mwanamke, bali pia kuhamasisha uzazi salama nchini”.

‘Kila dakika moja dunia inapoteza mwanamke mmoja kwa matatizo ya uzazi, tunahitaji kufanya mabadiliko hususani katika kipindi hiki ambacho dunia inasherehekea miaka mia moja ya siku ya mwanamke, na taifa pia la Tanzania likitimiza miaka 50 toka uhuru, hivyo hatuna budi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunampa mchango mwanamke katika suala zima la afya ya uzazi” alisema Mustafaa Hassanali.

Mustafa Hassanali, mwenye elimu na uelewa mzuri wa udaktari, ambae ndie alieanzisha mpango wa ‘Fashion 4 Health’, mpango ambao umefanya maonyesho ya mavazi katika kusaidia masuala mbalimbali yahusuyo afya toka mwaka 2008, na moja kati ya harakati zake, ni pamoja na ile ya kuchangia hospitali ya wenye matatizo ya akili huko Zanzibar, ambapo kiasi cha shilingi milioni 23 zilipatikana kutokana na mradi huo.
Akiwa kama nguli wa mitindo Afrika Mashariki na kati, na mwenye nia ya kuiweka fani hii ya mitindo mbele, Mustafa Hassanali alisema”tunatarajia kufanya onyesho la wazi kwa tarehe tano ya mwezi wa tatu, hii itasaidia kuipa nafasi jamii yote bila kujali uwezo wa mtu, kupata taarifa kamili na sahihi kuhusu uzazi salama hapa nchini”.

Akichangia katika hilo, meneja mauzo na masoko wa Mustafa Hassanali, ndugu Hamis Omari alisema kuwa “maonyesho haya yataenda sambamba na utoaji elimu bure kuhusu afya ya uzazi salama, tekinolojia husika na haki ya kila raia katika hili”

Meneja Masoko huyo aliwaomba wadau na makampuni mbalimbali kujitokeza ili kudhamini onyesho hilo lenye nia njema, ili kutoa mchango wao katika kumsaidia mwanamke wa Tanzania na uzazi salama.

‘Mamma Mia’ ni jina lililotokana na wimbo uliovuma sana katika miaka ya 80 na kundi la ‘ABBA’, ambapo onyesho hilo litajumuisha mitindo mipya na ya nguvu toka kwa Mustafa Hassanali, pamoja na wabunifu waalikwa toka wiki ya mitindo ya Uingereza.

Monday, February 14, 2011

Precision Air yatua Bukoba


Ndege ya shirika la ndege la Precision juzi Jumamosi, ilitua rasmi katika uwanja wa ndege wa Bukoba na kulakiwa kwa furaha na watu wa mkoa wa Kagera baada ya kuisha kwa matengenezo ya uwanja wa ndege wa Bukoba.

Akizungumza baada ya kutua Bukoba Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air Alfonse Kioko alisema;

“Hii ni fursa na furaha kubwa kwetu kupata nafasi ya kutoa huduma zetu kwa wakazi na wadau wa mkoa wa Kagera baada ya kutokuwepo kwa muda wa mwaka mmoja sasa”

Uzidnuzi wa safari hizo unafuatia kumalizika kwa ukarabati wa kiwanza cha ndege cha Bukoba uliofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania.

“Huduma ya safari itakuwepo kila siku kutoka Dar es Salaam kupitia Mwanza na kutoka Bukoba kwenda maeneo tofauti katika mtandao wetu,” alisema Kioko.

“Tunaanza na bei ya Tshs. 454,000 kwa safari ya kwenda na kurudi,” aliongeza Kioko.

Katika safari za Bukoba Precision Air itatumia ndege aina ya ATR42-500 iliyobatizwa jina la Bukoba kama ishara ya shukrani kwa watu wa Kagera.

Ndege hii inauwezo wa kubeba abiria 48. Ndege ya aina ya ATR42-500 ni ya kisasa kabisa katika soko la ndege kwa sasa. Ndege hii ni mpya kabisa ambayo imefungwa na vifaa vya kisasa na bora zaidi vya michezo ya kufurahisha abiria. Ndege hii ilinunuliwa mnano mwezi wa Nane mwaka jana kwa hiyo ni moja kati ya ndege mpya kabisa za Precision Air.


Kampuni ya ndege ya Precision imedhamiria kutoa huduma bora kwa wateja wake kwa kutumia vifaa vyake vipya na vya kisasa katika soko la biashara ya ndege. Pia kampuni ina mpango wa kupanua mtandao wake nje ya nchi ikiwemo kuanzisha safari kwenda Johannesburg- Afrika Kusini.

Hivi karibuni watanzania watapata nafasi ya kumiliki sehemu ya Precision Air kwa kunua hisa zake katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Mnamo mwaka 2006 Kampuni ya Ndege ya Precision na kampuni ya kutengeneza ndege ya ATR walisaini mkataba wa Dola milioni 129 kwa ajili ya ununuzi wa ndege saba mpya katika mpango wake wa kuboresha ndege zake. Ndege ya mwisho kutoka ATR iliwasili Jijini Dar es Salaam mwezi Septemba mwaka jana.

Thursday, February 10, 2011

Mkapa: Kura ya maoni Sudan Kusini ilikuwa ya uhuru


Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya watu watatu iliyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuangalia mchakato wa maandalizi na hatimaye upigaji kura ya maoni katika Sudan ya Kusini. Ameliambia Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa matokeo ya kura hiyo ni ya haki, huru na kuaminika.

Rais Mstaafu Mkapa, ameyasema hayo siku ya jumatatu wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa yake mbele ya Baraza hilo, ikiwa ni siku mbili zimepita tangu kutangazwa rasmi matokeo ya kura hiyo yaliyoonyesha, kuwa asilimia 98.83 ya wananchi waliopiga kura wameamua kujitenga na kuwa na taifa lao.

“ Timu yetu inapenda kuhitimisha kwamba matokeo ya kura hiyo ya maoni yameonyesha matakwa ya wananchi wa Sudan ya Kusini, mchakato mzima wa upigaji wa kura ulikuwa wa uhuru, haki na wa kuaminika”. Anasema Mkapa.

Akasema kukamilika kwa zoezi hilo ni moja ya hatua muhimu sana kuelekea upatikanaji wa amani ya kudumu.

Baada ya matokeo ya mwisho ya kura hiyo kutangazwa na baada ya pande zote mbili kuridhia na kuyakubali, huku Jumuia ya Kimataifa ikiyaridhia, Taifa huru la Sudan ya Kusini litakaribishwa rasmi katika Jumuia ya Kimataifa Julai 9 mwaka huu.

Mkapa ambaye timu yake ilitembelea Sudan ya Kusini mara tano katika kipindi cha kuelekea upigaji wa kura hiyo. Amelieleza Baraza hilo kwamba, katika kutathimini mchakato huo wote, timu yake ilizingatia misingi yote iliyoainishwa katika Sheria ya Kura ya Maoni ya Sudan ya Kusini. Na kwamba Timu imejiridhisha kuwa zoezi lilifanyika katika mazingira ya uwazi wa hali ya juu.

Maonyesho ya Harusi kufanyika Dar



Maandalizi ya maonyesho ya pili ya Harusi Tanzania ‘Harusi Trade Fair 2011’, yanayotarajiwa kuanza tarehe 1- 3 mwezi ujao katika ukumbi wa Diamond Jubilee yanaendelea vizuri , huku yakiwa yanajumuisha wataalamu waliobobea katika nyanja zote zinazohusiana na suala zima la Harusi.

Muaandaaji na msimamizi wa maonyesho haya makubwa ya Harusi Tanzania , Mustafa Hassanali amesema kuwa “maonyesho ya mwaka huu yatakuwa makubwa, mazuri na yenye kuvutia zaidi ya mwaka uliyopita, na tunatazamia kuyafanya yawe maonyesho makubwa zaidi kwa ukanda huu kwa miaka ijayo”

Nukuu zinasema kuwa, maonyesho ya mwaka huu tayari yameshawavutia zaidi ya washiriki 32 , wakiwemo washiriki wa maonyesho yaliyopita na wapya.

Maonyesho ya Harusi ya mwaka 2011, ni maonyesho ambayo uboreshaji wake umevuka kutoka siku mbili za maonyesho hadi siku tatu kwa mwaka huu, huku likiongezewa na kujumuisha vionjo vingi zaidi.

“Harusi ni tukio zuri, ambalo hutokea mara moja tu, huku likiunganisha familia na jamii pamoja, hivyo nia yetu ni kuwapa maharusi mahitaji yao yoote muhimu kwa pamoja na kwa wakati mmoja, na maonyesho haya ndio sehemu muafaka kwa hilo ” alisema Mustafa Hassanali.

Maonyesho haya ya Harusi ambayo hufanyika kila mwaka, huwaleta pamoja wahusika wote wa mambo ya Harusi katika kujenga na kutengeneza mtandao wa kimafanikio baina yao, na ndio maana maonyesho haya yamekuwa ni ya kwanza na ya aina yake Tanzania, ambapo kwa mwaka huu yatapambwa na vitu kama keki, maua, wapiga picha, magauni ya Harusi, bila kusahau mengi na yenye ubunifu katika Harusi.

Gabriel Makupa wa ‘GRM Production’, ambae ni mmoja wa washiriki wa mwaka huu wa maonyesho haya alisema kuwa, wamekuwa na wakati mzuri kibiashara, hali iliyosababishwa na ushiriki wao katika maonyesho haya kwa mwaka uliyopita.

“tumekuwa na wakati mzuri kibiashara, hii imetusaidia kujenga mtandao mzuri kibiashara, tulitangaza huduma zetu vilivyo, na hii ndo sababu ya sisi kushiriki tena mwaka huu” alisema Gabriel wa GRM, kampuni inayojihusisha na upigaji picha katika maharusi.

“makampuni yajitokeze kutangaza huduma zao mwaka huu katika maonyesho haya, ni nafasi nzuri, kwani tumeshapata makampuni 32 mpaka sasa yatakayoshiriki mwaka huu, idadi ambayo inaongezeka kila siku, “ alisema Mustafa Hassanali.

Mmoja wa washiriki wa mwaka huu wa maonyesho kutoka ‘Karibu Holiday’, kampuni inayoshughulika na maandalizi ya fungate kwa maharusi na mapumziko binafsi nchini, Bw. Susai Nathan alisema kuwa, maonyesho ya mwaka huu ni njia mbadala ya kutangaza huduma zao mpya zenye ubora maalum kwa fungate, mahususi kwa maharusi au watakaofunga ndoa katika miezi hii mitatu ijayo.

Haya ni maonyesho ya siku tatu ambayo yana mengi, na si yakukosa kushiriki ama kuhudhuria kwa maharusi, familia, na wale wote wanaohusika na kamati za Harusi, ili kujionea na kujua mengi yahusuyo Harusi na mahitaji yake.


Monday, February 07, 2011

Usafiri wa mitaa ya Mbambabay




Hii ni sehemu ya barabara ya Mbinga - Mbambabay kama ilivyoshuhudiwa na mdau wetu aliyepita maeneo hayo juzi.

Sunday, February 06, 2011

JK aunda tume matatizo ya vyuo vikuu


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEUZI WA TUME YA KUTAYARISHA MFUMO MPYA WA KUGHARIMIA/KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

Katika hotuba yake ya kukizindua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma Novemba 25, 2010, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliahidi mambo makubwa mawili kama ifuatavyo, nanukuu:

Moja: “Kuhusu mikopo ya elimu ya juu napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni. Serikali iliongeza fedha za mikopo kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/06 hadi kuwa shilingi 237 bilioni mwaka 2010/11 na wanafunzi waliopatiwa mikopo hiyo wameongezeka kutoka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi; na

Pili: Pia tutautazama upya mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ikiwepo na utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuuboresha na kuleta ufanisi zaidi. Mawazo ya wadau wakiwemo wamiliki wa vyuo, wahadhiri na wanafunzi, yatasaidia sana”.

Ili kutekeleza ahadi hiyo ya Pili, Mheshimiwa Rais ameteua Tume ya wataalam 11 kufanya mapitio ya mfumo na uendeshaji wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mikopo hiyo. Tume inatakiwa kufanyakazi kwa siku 60, kuanzia tarehe 14 Februari 2011 na kuwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi tarehe 15 Aprili 2011.

Tume hiyo itaongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Makenya Abraham Maboko.

Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Bw. Masoud Mohamed Haji, Ofisa Uhusiano wa Kimataifa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Zanzibar; na Dkt. Eliawony Kristosia Meena, Mhadhiri Mwandamizi (Elimu), Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha.

Wengine ni Bw. Daniel Paul Magwiza, Naibu Katibu, Tume ya Vyuo Vikuu; Bibi Sarah K. Baharamoka, Mkurugenzi Msaidizi (Uandishi Sheria), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Profesa Penina M. Mlama, Mkurugenzi Mtendaji wa Tawi la Tanzania la Taasisi inayopigania Elimu kwa Wanawake (Campign for Female Education Tanzania Chapter).

Katika Tume hiyo pia yumo Bw. Deo Mbasa Daudi, Ofisa Taaluma, Chuo cha Usimamizi wa Fedha, ambaye ni Rais Mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-DARUSO (2007/2008), na Katibu Mkuu Mstaafu wa DARUSO (2006/2007); Bw. Kassim Almasi Umba, Makamu Mkuu wa Chuo (Utawala na Fedha), Chuo Kikuu cha Kiislamu, Morogoro; Bw. Anderson Y. Mlambwa, Mkurugenzi wa Mikopo, Benki ya CRDB; Prof. Wilbert Abel, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Bibi Rosemary Rulabuka, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Tume itateua Makamu Mwenyekiti kutoka miongoni mwa Wajumbe. Sekretarieti ya Tume hiyo itatokana na Wajumbe kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Ikulu.

Hadidu za Rejea za Tume hiyo ni pamoja na kuchambua kwa kina Sheria Na. 9 ya mwaka 2004, iliyounda Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, na Kanuni zake na kubainisha vifungu vinavyohitaji marekebisho kulingana na hali halisi ya utoaji mkopo na kuangalia upya vigezo na sifa zinazozingatiwa katika utoaji wa Mkopo endapo vinakidhi haja na mahitaji halisi ya waombaji na taifa kulingana na makusudio ya kuundwa kwa Bodi ya Mikopo.

Nyingine ni kuangalia kwa kina muundo wa Bodi na ufanisi wake katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na kutoa mapendekezo na kuchunguza kiini cha malalamiko na mahusiano yasiyoridhisha kati ya Bodi na Wanafunzi, Bodi na Taasisi ya Elimu ya Juu na kati ya Bodi na Wizara ya Elimu na kutoa mapendekezo ya namna ya kurejesha mahusiano mazuri.

Hadidu nyingine za rejea ni kuchambua mfumo mzima wa namna ya kubaini wanafunzi wanaohitaji mikopo (Means Testing) ili kuibua mapungufu yake na kupendekeza taratibu za kuuboresha au kuwa na mfumo mbadala na kuangalia mambo yanayosababisha mifuko mingine kama vile “Resource Endowment Fund” wa Maliasili unafanikiwa na Nchi nyingine zenye mazingira kama ya Tanzania zinavyofanikiwa kugharimia Elimu ya Juu kwa mfumo wa Mikopo.

Nyingine ni kutoa ushauri na mapendekezo yatakayowezesha Mkopo utolewe kwa wanafunzi wengi wahitaji wa Elimu ya Juu ili kuondoa lawama zilizopo na kushughulikia mambo mengine yoyote yatakayoweza kuboresha mfumo huo kwa kadri inavyoonekana inafaa.

Ni matumaini ya Serikali kwamba baada ya Tume hiyo kukamilisha kazi yake, itatoa ushauri utakaosaidia kujibu malalamiko mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Mizengo P. Pinda (Mb)

WAZIRI MKUU

6 Februari 2011

Palestina wawasili kukipiga na Stars





Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Palestina wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu JK Nyerere kabla ya kwenda katika Hoteli ya Transoma jijini Dar es Salaam.

Matembezi ya Mshikamano


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mkewe Tunu wakiwapungia wananchi katika matembezi ya mshikamano ya kuadhimisha miaka 34 ya CCM Mkoani Iringa yaliyofanyiak kimkoa kwenye Kijiji cha Tungamalenga wilayani Iringa Mjini jana. Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Mbunge wa Ismani, William Lukuvi na Kushoto ni Kamu Mkuu wa mkoa wa Iringa Issa Machibya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)