WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PFOF. JUMANNE MAGHEMBE AKABIDHIWA RASMI OFISI LEO NA ALIYEKUWA WAZIRI WA WIZARA HIYO LAZARO NYALANDU


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akikabidhiwa taarifa ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kulia) leo tarehe 29 Desemba 2015 ofisini kwake Mpingo House. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Selestine Gesimba (kulia).
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) akizungumza na Waziri wa sasa wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru (kulia) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika leo tarehe 29 Desemba 2015 katika ofisi za Wizara hiyo Mpingo House. Katika salamu zake Mhe. Nyalandu amepongeza uteuzi wa Prof. Maghembe ambapo amesema Mhe. Rais amefanya chaguo sahihi kwani Prof. Maghembe anao uwezo wa kufanya kazi nzuri katika Wizara hiyo. 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akizingumza na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kulia) muda mfupi baada ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisini kwake leo. Mhe. Prof. Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzrui aliyoifanya akiwa Waziri wa Wizara ya Malisili na kuahidi kuanzia alipoishia katika kuhakikisha Maliasili za nchi zinatunzwa ipasavyo ikiwemo kupambana na changamoto zilizopo za ujangili na uharibifu wa misitu na maliasili kwa ujumla.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri kabla yake Mhe. Lazaro Nyalandu, Makabidhiano hayo yamefanyika leo Makao Mkuu ya Wizara hiyo, Mpingo House jijini Dar es Salaam.

Katika makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amekabidhi taarifa rasmi ya makabidhiano kwa Mhe. Waziri Prof. Jumanne Maghembe kama ishara ya kukabidhi rasmi Ofisi ya Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Makabidhiano hayo ambayo ni utaratibu wa kiserikali wa kukabidhi ofisi umeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Selestine Gesimba, baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo na waandishi wa habari.



Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amempongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Prof. Maghembe kuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili kwa kuwa ana sifa stahiki za kuongoza Wizara hiyo nyeti.

Aliongeza kwa kusema kuwa Prof. Maghembe ana sifa ya kuwa mhifadhi kwa kusomea na pia ni mhifadhi kwa asili yake hivyo Wizara imepata mtu makini kwenye masuala ya Uhifadhi.

“Natambua umahiri wako katika masuala ya uhifadhi nina imani utapambana na ujangili pamoja na usafirishaji haramu wa magogo kwa kasi inayotarajiwa na wananchi”. Alisema Mhe. Nyalandu.

Kwa upande wake, Waziri aliyechukua nafasi yake Prof. Jumanne Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzuri na juhudi aliozoonesha wakati akiwa Waziri wa Wizara hiyo katika kuhakikisha Maliasili zilizopo zinaendelea kuwepo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. 

Prof. Maghembe ameongeza kuwa kwa sasa vita kubwa iliyoko mbele yake ni vita dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa rasilimali za misitu kinyume cha sheria. Ameomba ushirikiano kwa wadau wote wa Maliasili nchini kumpa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anafanikiwa katika vita hiyo.

Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo ya makabidhiano inaelezea kazi zilizokwisha kufanyika katika kipindi cha utawala uliopita, kazi zinazoendelea na zilizopo kwenye mpango wa utekelezaji pamoja na changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo Ujangili na uvunaji pamoja na usafirishaji wa magogo. 
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii)

Comments