Monday, March 27, 2006

Vibaka wakizidi tusije kamatana mashati

SIKU zote kitu maamuzi ni kitu kinatakiwa kuchukuliwa kwa tahadhari na mazingatia makubwa.

Maamuzi yanaweza kuharibu, kubadilisha mambo na au kuboresha, lakini pia yanaweza kuwa chanzo cha matatizo mengine makubwa ambayo huwa magumu sana kuyazima.

Yanapochukuliwa maamuzi siku zote huwa zipo pande zinafaidika na zingine zinataabika, lakini cha msingi kinachoangaliwa mara zote hizo ni 'rationality'

Yapo mengi yanaweza kuzungumzwa kuhusu 'rationality' ambayo kwa upande mmoja inaweza ikawa sawa sawa, lakini upande mwingine ikawa 'wrong' mathalani mtu akiiba chakula sababu ana njaa upande mmoja sawa upande mwingine noomaa!

Alhamisi iliyopita wachimba kokoto wapatao 3,021 waliokuwa wakiendesha shughuli zao eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam, waliamriwa kuondoka katika eneo hilo mara moja na leseni za wengine kufutwa.

Agizo la kuwaondoa wachimbaji hao, 21 wakiwa na leseni 3,000 wakiwa ni wadogowadogo, lilitolewa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya kutembelea eneo hilo kujionea uharibifu wa mazingira uliofanyika hapo.

Lowassa alichukua hatua hiyo baada ya kushuhudia uharibu wa kutisha wa mazingira ambao unatishia kubomoka kwa barabara ya Bagamoyo, aliagiza leseni za madini walizopewa wachimbaji wa kokoto wanaoendesha biashara hiyo katika machimbo ya Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam, zifutwe mara moja ili kunusuru mazingira na barabara kuu.

Kama hilo halitoshi maelfu ya wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na majiji mengine waliondolewa kwa operesheni kamambe kutokana na kufanya biashara katika maeneo ambayo hayakupangwa kwa matumizi hayo.

Sambamba na hayo kundi jingine kubwa la waliokuwa wakifaidika kutokana na biashara ya mkaa na upasuaji na usafirishaji magogo nao lilionja chungu baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii kupiga marufuku biashara hiyo hadi hapo baadaye yatakapotolewa maelezo ya kina.

Balaa kubwa zaidi ni lile lililosababishwa na upungufu wa nishati ya umeme iliyosababisha mgao wa umeme ambayo kwa maana nyingine ni kwamba wale wengine waliokuwa wakifaidika na shughuli ndodondogo za umeme sasa ndiyo basi tena wanashinda njaa!

Siwezi kusema kuwa ni sahihi kwamba serikali imechukua hatua kwasababu tatizo linakuja kwamba watu hawa walioondolewa katika maeneo waliyokuwa wakijipatia kipato watakwenda wapi.

Nafahamu kabisa kwamba zipo hatua zimependekezwa zikiwamo za kuwahamishia maeneo mengine yaliyopangiliwa, lakini pia hayo maeneo yatafahamika lini? Na muda wote huu watakaokuwa watu hawa wakisubiri watakula nini? Na je watu hawa wajitafutie kazi wapi?

Naamini kabisa kwamba Serikali zilizopita zilikuwa na ujasiri na nguvu zote za kufanya maamuzi magumu kama haya, lakini tatizo lilikuwa hali halisi ya watu wao na mazingira wanamoishi.

Ikumbukwe kwamba siyo tu wale waliotimuliwa katika maeneo husika ndiyo watakaoathirika na maamuzi machungu haya, bali ni mlolongo wa watu wengi wanaofaidika nao watakosa kupata huduma, wamo ndugu na jamaa na watoto wa familia husika, lakini pia watumiaji!

Ikumbukwe pia wakati serikali ya awamu ya kwanza ilipokuwa ikijenga vijiji vya ujamaa ilikuwa na lengo zuri, lakini lilikuja kuwa tatizo kubwa watu walipoteza maisha, vijiji vingine vilifutika, uchumi ukayumba na mambo mengi. Hivyo maombi yetu sisi ni kuwa maamuzi haya yasije kusababisha matatizo mengine. Hatua za haraka zichukuliwe.

Wednesday, March 22, 2006

Tunauondoa umaskini kwa kutumia?

UMASKINI kama ulivyo au lilivyo neno lenyewe ni maarufu sana katika mataifa yetu haya, hasa yanayoendelea. Kila kukicha kuna suala moja au mawili au hata zaidi yataugusia au kuuzungumzia au kuihusu jamii. Ni wachache au hakuna kabisa kati yetu ambaye ataepa kuguswa na umaskini.

Wengine wanadiriki kusema umaskini hauwezi kuisha, eti kwa sababu utajiri upo, hawa wanatumia 'lojiki' au mantiki za falsafa za kijamii. Inawezekana wakawa na ukweli ndani yake. Tofauti na hao, lipo kundi jingine la wenye mwelekeo wa wastani, hao hudhani umaskini unaweza ukaondoka na jamii ikaishi maisha inayotaka! Sijui.

Katika somasoma yangu, nimekumbana na kauli mojawapo iliyopo katika kitabu kimoja cha kuvutia chenye jina "The Undercover Economist" kilichoandikwa na Tim Harford inayohusu nchi ya China, ambayo nafikiria Watanzania wenzangu wanapaswa kuipata. Taarifa hii inasema hivi: "China imefanikiwa kuwaondoa mamilioni ya watu wake kutoka katika wimbi la umaskini kila mwezi." Kumbuka kwamba nchi hii ina watu zaidi ya bilioni moja.

Kauli hii inaweza kuonekana nyepesi, lakini imebeba ujumbe mzito. Sijaangalia bado katika takwimu, lakini nachoweza kukigundua katika kauli hii inaonekana kuna mafanikio. Kama hii ndivyo ilivyo, basi ni taarifa ambayo inatia faraja na kila mmoja miongoni mwetu anapaswa kuipata.

Watu katika medani za siasa wanapiga kelele katika kiwango wanachoweza kila siku na kuainisha programu na sera mbalimbali za namna ya kuupunguza umaskini, lakini wanakuwa wanaonyesha shauku kidogo sana katika mipango ya namna umasikini ulivyopunguzwa, iwe hapa kwetu au kwingineko.

Wanapanga kila aina ya mkakati, ziwe semina, sijui warsha na halafu mikakati ambayo inakuja na majina ya ajabu ajabu, nadhani majina yamekwisha! La hivi karibuni kabisa lafahamika kama MKUKUTA, Mkurabita na kadhalika. 'Mikukuta' hii haiondoi umaskini kama inavyokusudiwa badala yake yenyewe inatumia pesa na halafu mwisho wa siku maskini anabakia palepale.

Sisemi kuwa haifanyi kitu kabisa. La hasha, inapunguza umaskini, lakini kwa kasi ndogo sana, tena kwa makundi yasiyokusudiwa. Tunataka watu wetu maskini halisi waondokane na umaskini!

Msomaji wangu, nadhani unaweza kuotea kiasi ambacho watu wa magharibi wanavyochukizwa na mafanikio haya ya China. Mataifa hayo tajiri hupata shauku sana wakati mataifa mengine hasa ya kimaskini yanapokumbwa na majanga na maelfu kwa mamilioni ya watu wakiwa wanakufa ama kwa njaa au maafa. Wao, hufurahia zaidi kama mataifa hayo yana almasi, dhahabu, mafuta na maliasili zinginezo.

Wale miongoni mwetu wasiokuwa na mtazamo huo wa kimagharibi habari hii ni yenye kutia shauku na kuvutia kwa China kuweza kujitoa katika umaskini.

Awali ya yote kwa tuanze kwa kujiuliza, hivi ina maana gani kwa "China kuwainua watu milioni moja kutoka katika wimbi la umaskini kwa mwezi"? Ni wapi serikali ya China inapata fedha hizo kutekeleza jukumu hilo muhimu na nyeti? Bila shaka watu pekee serikali inayoweza kuwatoza kodi ni watu wa China pekee.

Kiuhakika kabisa nchi haiwezi kujinyanyua yenyewe kwa kiasi kikubwa namna hiyo kwa kutumia uwezo wake wa ndani pekee au hata kwa kutumia msaada wa nje hauwezi kutosha kuwaondoa masikini milioni moja kwa mwezi. Kama serikali ya China haijafanya hivyo, nani ameweza kufanya hivyo?

Hawaondolewi katika umaskini eti kwa kwa ukarimu wa mtu fulani. Kitu pekee kinachoweza kutibu umaskini ni utajiri. Wachina wameupata utajiri kwa njia ya kikale kidogo: Waliutengeneza. Baada ya kifo cha Mao Tsetung, udhibiti wa serikali katika biashara ukaanza kupungua taratibu --kwanza kwa kufanya majaribio katika maeneo waliochagua wenyewe na viwanda maalumu.

Halafu baada ya viwanda hivyo kupata mafanikio ya haraka, serikali ikaendelea hatua kwa hatua lakini kwa umakini mkubwa katika maeneo mbalimbali na maeneo yote hayo yakaibuka na matokeo yaleyale.

Umasikini hauwezi kuondoka kwa kuutumia kwa kusema sana kisha wachache wakaingia katika kumbi za mikutano na kujifaidisha kwa posho nono huku kukiwa hakuna utekelezaji. Unaondoka kama kuna utashi, nia na mipango inayotekelezeka. Jambo la maana ni kama hivi China ilivyofanya.

Monday, March 20, 2006

Kumbe tunaweza, mkoloni hakukosea kutuchapa viboko

KADRI ninavyoendelea kutaabika kama walivyo Watanzania wengi, kusota na kuhofia kesho baada ya leo kupita kimkanda mkanda, ninakaribia kushawishika kuwa utawala wa kusukumana kwa viboko ndiyo hasa unafaa kusukuma maisha.

Naaamini ile hadithi kwamba, wakoloni hasa wa Kijerumani walikuwa wakiwashurutisha wasiotaka kufanya kazi kwa kuwatandika henzerani nyingi tena hadharani umeisikia na pengine imekuwa ikikugusa kwa namna moja au nyingine.

Kwa taarifa yako, hulka hiyo ya wakoloni ilipewa jina baya kabisa na ndiyo maana baada ya kupata uhuru ililaaniwa kwa nguvu zote, ingawa kwa mtazamo wangu ukweli unabaki pale pale kwamba, viboko viliwezesha mambo mengi kusonga mbele.

Hebu angalia, tulijengewa reli ambayo inatumika hadi leo, tulijengewa nyumba ambazo mpaka leo kila unapokwenda makao makuu ya karibu kila mkoa au wilaya utayakuta na yanatumika, miundombinu mingi kama barabara, madaraja, minara ya simu, mabomba ya maji yanatokea enzi hizo ingawa sikubaliani nao kwa ubabe wao, lakini walichofanyika kimeonekana.

Sijui hawa walikuwa wakifuata zile nadharia za baba wa menejimenti aliyevuma miaka ya sitini, Douglas McGregor aliyevumbua nadharia X na Y ambapo alijenga dhana kuwa kwa kawaida mwanadamu hapendi kufanya kazi na hujitahidi kukwepa kadri awezavyo.

Kutokana na binadamu kutopenda kazi akasema, watu wengi ni lazima wadhibitiwe na kutishwa kabla ya kuwa tayari kufanya kazi kwa ridhaa zao. Na kuwa mtu wa kawaida anapenda sana kuelekezwa, huchukia majukumu, ni mtata na hupenda sana kuhakikishiwa usalama wake.

Nadharia Y inadhania udhibiti, adhabu na vitisho siyo njia pekee inayowafanya watu kuchapa kazi na kwamba mtu atajielekeza mwenyewe kama atajituma kutekeleza malengo ya taasisi au kampuni husika.

Anaendelea kusisitiza kuwa, kama mazingira ya kazi yanaridhisha, basi matokeo yake itakuwa watu kujituma kwa kampuni, jumuiya. Kwa dhana hii kikawaida mtu anajifunza katika mazingira ya kawaida, fikra na utundu vinaweza kutumika kupata suluhisho la matatizo ya idadi kubwa ya waajiriwa.

Fikra zake hizi ndizo bila shaka zinatumika sasa, na bila shaka zinatoa mafanikio kwa pande zote mbili moja ikiwa ni ile inayotumia adhabu na udhibiti wa kina na ya pili ni ile inayovumilia uvivu na kutopenda kufanya kazi.

Ingawa zote hizi mbili zina upungufu wake sababu binadamu anahitaji mengi zaidi ya adhabu na vitisho, mathalani anahitaji motisha ya kipato cha fedha kazini na pia anahitaji kuenziwa.

Kwa kuzingatia hayo ya hapo juu, ninaposema viboko sina maana ya viboko halisi ninamaanisha maamuzi makali yasiyotania kuona aibu wala kutaka sifa kwa upande mmoja, yanayoangaliwa walala hoi wanapata nini wanaishi vipi na wanasikilizwa vipi.

Kipindi cha miezi michache iliyopita kuwapo katika ofisi ya juu kwa maana ya uwaziri, ukatibu mkuu au nafasi nyingine ilikuwa ni sawasawa na kuingia likizo, kula kuku, watu walijifanya mambo walivyoweza hawakuhofia lolote na hata kama walikuwa na hofu ya kuharibu basi walikuwa nayo kidogo mno.

Imefika kipindi cha Jakaya Kikwete huyu ndiye Rais wa sasa ambaye staili yake ya kuongoza ni tofauti kabisa na staili za viongozi waliopita kwa maana kwamba staili yake inazingatia kurekebisha hali za masikini.

Watu wale wale waliokuwa katika ofisi zile zile na waliopata mafunzo yale yale ya kazi wameibuka na kuanza kucharuka, dalili zinaanza kuonyesha kwamba kumbe watu wanaweza kufanya kazi. Wanaweza kutekeleza majukumu yao kama wakitiwa hofu, wakionyeshwa njia, wakielekezwa.

Ukijiuliza nini kimewafanya kuamka namna hii jibu lake bila shaka utakuwa na mlolongo wa visingizio, labda ni kwa sababu ya kuogopa uongozi au wanaogopa adhabu ya kupoteza unga unaowafanya kuishi mijini au wameridhishwa sana na mazingira.

Kwa staili hii wapigadebe, wamachinga watastawi

NI lazima niseme kuwa ni mmoja wa watu ambao hawakushangazwa hata kidogo na matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, ingawa bado watu wengi wanabakia na hisia na au maswali mengi kwa nini CCM kinaendelea kutawala siasa za Tanzania pamoja na kushindwa kwao kukidhi matakwa mengi ya wananchi wake na haswa kwa upande wa ukosefu wa ajira.

Katika maelezo ya kitaaluma yapo maainisho ya aina mbili yanayoendana na hali hii. Ya kwanza ni kwamba wapiga kura wanakichagua chama kutokana na ufanisi wake. Hii hasa ni nadharia ya kiuchambuzi.

Ainisho la pili ni kwamba, wapiga kura walikichagua chama hicho ili kujitengenezea uchochoro wa kuweza kufanya 'madudu yao' kama kawaida kutokana na ule usemi na pengine mazoea ya 'zimwi likujualo halikuli likakwisha'

Kuna ukweli ndani ya nadharia hizi mbili kwa kutegemea hasa ni nini lengo lako msomaji ingawa ukweli halisi unabakia kwa mchambuzi.

Sina haja ya kujadili nini kilikuwa nini, lakini kiufupi matokeo ya uchaguzi kiuhakika yanathibitisha ubabe tu wa CCM katika siasa za uchaguzi na kamwe siyo ubora wa uongozi itakaoutoa kwa wavuja jasho na wafyeka nyasi wa nchi hii, kwa sasa na hata baadaye.

Matokeo hayo ya uchaguzi yanatueleza kwamba, mfumo wetu wa siasa unajionesha na kujikita mno katika uwingi wa watu, lakini hazionyeshi uhusiano wa kina uliopo baina ya chama hicho kilichochaguliwa kwa uwingi wa kura kwa upande mmoja na mahakama, bunge, vyombo vya habari, vyuo vikuu na jumuiya za kiraia kwa upande mwingine.

Fikra za kuwa uwingi ndiyo ubora bila ya kuzingatia ubora, ndizo zinazoonyesha kutawala vichwa vyetu hata katika tunavyofikiria kuunda sera zinazoathiri umma.

Kila siku tunatwikwa mizigo ya matarajio ya makuzi. Aidha ya uchumi au kitu kingine chochote kwa kuzingatia uwingi, lakini ni nadra kuwa na mijadala ya kuinua ubora ili kupunguza umasikini, kuongeza ajira na kuondoa pengo lililopo baina ya walio nacho na wasio nacho.

Hata kama tunazungumzia siasa za uchaguzi au sera za kunufaisha umma, kunaweza kukawa hakuna garantii ya demokrasia yetu na hasa katika ubora wa demokrasia hiyo tunayoilenga.

Wiki hii nzima imegubikwa na operesheni mbalimbali lakini kubwa ni tatu, yaani ya kwanza kabisa ikiwa ni ya majambazi, ya pili ikiwa ni bomoa bomoa na kisha ile ya tatu ni ya kufukuza wapiga debe.

Sina tatizo kabisa na operesheni ya kufagia majambazi. Lakini nina matatizo makubwa sana katika fikra zangu na hizi operesheni mbili za bomoa bomoa ya vibanda na kisha wapiga debe.

Hivi wakati hawa wazembe wanaoshinda vituoni kwa kupiga kelele walipokuwa wakianza huu 'usanii' wao katika vituo, mamlaka zilikuwa wapi mpaka wanajikusanya na kuwa na nguvu namna hii.

Upande mmoja wa mawazo unaweza ukatetea kuwa walikuwa sahihi kutokana na hali ngumu, kwamba walijibunia aina yao ya ajira, lakini hapana sijapata kuona katika majiji yoyote makubwa niliyotembelea duniani aina hii ya kazi.

Kwanza hebu tufuatilie kwa kina kabisa ni nini chanzo cha haya matata yote mpaka hawa wamachinga wanatanda mabarabarani, wapiga debe wanazidi vituoni, utagundua kuwa chanzo ni ukosefu wa ajira ambao una milolongo ya masuala ambayo huko nyuma hayakutiliwa mkazo kama elimu, kilimo na elimu ya stadi za maisha kama nilivyoeleza hapo juu.

Ninavyoona mimi hata kama tukibomoa vibanda na kisha tukamwaga sumu katika maeneo hayo au hata mitego ili watakaogusa wanaswe, bado vibanda vitajengwa, wapiga debe watabakia sababu suala la msingi halijaguswa. Yameguswa matawi badala ya mashina.

Mashina ni matatizo ya msingi yanayosababisha matata yote haya na matawi ndiyo hii bomoa bomoa. Tutawapiga risasi bure wafanya biashara ndogo ndogo, tutawajeruhi na tutafanya kila kitu lakini bila kuweka sawa masuala ya msingi ni bure.

Sikatai kuwa zipo jitihada za kukabiliana na umasikini za serikali zilizoibuka na mkakati wa MKUKUTA na MKURABITA, lakini zinasubiri nini. Maisha yanaendelea hivyo na wananchi ndiyo maana wanafanya vituko mabarabarani njaa haichagui. Hivyo cha msingi ni bora tukashughulikia masuala ya msingi.