Tuesday, October 13, 2015

WATANZANIA TUTAMBUE AMANI YETU NI FAHARI YETU (KUIDUMISHA BAADA YA UCHAGUZI)

 Msajili wa Vyama vya  Siasa Jaji Francis Mutungi  akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya   utofauti wa itikadi wa vyama ndiyo ukomavu wa demokrasia nchini hivyo ni jambo la busara kuvumiliana na kufanya siasa za kistaarabu, ameyasema hayo wakati  wa  kikao hicho kimefanyika jana jijini Dar es Salaam kulia ni Balozi wa Amani Mrisho Mpoto na kushoto ni Balozi wa Amani Christina Shusho.
 Balozi wa Amani Mrisho Mpoto akifafanua jambo katika kikao hicho jana jijini Dar es Salaam.
 Msajili wa Vyama vya  Siasa Jaji Francis Mutungi, katika kikao kilicho fanyikajana jijini Dar es Salaam.
(Picha na Emmanuel  Massaka)

Na Magreth Kinabo-maelezo
OFISIya Msajili wa Vyama  Vya Siasa imewaasa na kuwataka viongozi wote wa  vyama  vya siasa kutoa kauli na maelekezo kwa wafuasi wao na wanachama wa vyama vyao kutoshiriki katika aina yoyote ile ya uvunjifu wa amani hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu na baada  ya uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa jana na Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wakati akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi hiyo jijini Dares Salaam.

“Dhamana  ya nchi iko mikononi mwenu,ushawishi wenu kuhusu amani katika kipindi hiki ndio utakaoliokoa taifa la Tanzania ama  utaliingiza taifa katika vurugu na mfarakano,” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi alisema katika kipindi cha kampeni kumekuwepo na viashiria vya uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii yakiwemo baadhi ya makundi ya wanachama, wafuasi na mashabiki wa vyama siasa.

“Makundi hayo yanadiriki kutoa maneno ya kejeli, matusi, kuvamia, kupigana, hata kujeruhi makundi mengine, ambayo siyo ya upande wao. Hali  iiachwe mara moja ili kuiweka nchi yetu Tanzania  katika hali ya amani na kuiepusha kuingia kwenye vurugu, mfarakano na machafuko yasiyokuwa na  ulazima.

“Dumisheni amani na kamwe  tusijiingize kwenye siasa zinazoleta mfarakano na uvunjifu wa amani, kumbukeni  kuna maisha baada ya uchaguzi na amani ya nchi yetu ni fahari  yetu sote,alisema  Mutungi.

Aliongeza ni vyema Watanzania, wakatambua kwamba utofauti wa itikadiya vyama ndio ukomavu wa demokrasia nchini hivyo ni jambo la busara kuvumiliana na kufanya siasa za kiustaarabu.Hivyo kutovumiliana kwa utofauti wetu wa itikadi za kisiasa kunaweza kulata madhara makubwa kwa jamii itakatopelekea idadi kubwa ya Watanzania kupata athari ikiwemo ulemavu, vifo, ukimbizi,njaa na maradhi.   
 
Aidha ofisi hiyo imetoa rai kwa waandishi wa habari watumie kalamu zao vysema kuhubiri amani  na kuepuka kuandika habari za uchochezi, bali wawasaidie wananchi kupata taarifa sahihi zitakazowasaidia kufanya maamuzi wakati wa kuchagua viongozi wao.

Kwa upande wao mabalozi wa amani, ambao ni Mrisho Mpoto na Christina Shusho walisema kwa nyakati tofauti kuwa wamejitolea kuhubiri amani kupitia fani yao  ili nchi yetu iendelee kuwa na amani.

Akizungumzia suala hilo, Mpoto aliwapa changamoto waandishi wa habari wajiulize kuwa wana mchango gani  katika nchi yao ili kuhakikisha inakuwa na amani. Hivyo wanapoandika habari yoyote wakumbuke kwamba kuna watoto, yatima, walemavu na wajane, isije ikawa ni chanzo cha kuvuruga  amani.

Naye Shusho alisema kwamba yeye si mfuasi wa chama chochote,bali balozi wa kuhubiri amani. 
 
Ofisi hiyo imetoa kauli hiyo, kwa kuwa ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha ukuaji wa demokrasia unakuwepo kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kikatiba.

No comments: