Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maghala unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Mtaa wa Viwandani, Kata ya Railway, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Mhe. Mmuya amefanya ukaguzi huo Julai 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Mtwara yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi iliyo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Akipokea taarifa ya mradi huo, Mhe. Mmuya ameelezwa kuwa ujenzi wa maghala hayo unagharimu shilingi bilioni 4.1, ambapo hadi sasa shilingi bilioni 2.6 zimetumika. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba 2026.
Katika ukaguzi huo, Mhe. Mmuya amelishauri Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuendelea kubuni na kuwekeza katika miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hususan ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ili kusaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa makazi nchini.
Aidha, amepongeza Shirika hilo kwa kuwekeza katika ujenzi wa maghala katika eneo lenye shughuli kubwa za kiuchumi, akibainisha kuwa uwepo wa Bandari ya Mtwara pamoja na uzalishaji wa mazao ya biashara, hususan korosho, unafanya mradi huo kuwa na umuhimu mkubwa katika kuchochea biashara na maendeleo ya uchumi wa mkoa huo.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa mbalimbali, ikiwemo mazao ya kimkakati kama korosho, hatua itakayochangia kuongeza thamani ya mazao, kuboresha huduma za uhifadhi na kuimarisha shughuli za biashara kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara na maeneo ya jirani.










No comments:
Post a Comment