Sunday, October 25, 2015

TAARIFA MAALUM YA CHAMA CHA MAPINDUZI TAIFA KUHUSU UPIGAJI KURA UNAOENDELEA SASA HIVI LIVE!!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI CCM inafuatilia kwa karibu zoezi zima la uchaguzi kote nchini. Leo, tarehe 25.10.2015, saa kumi alasiri, CCM itafanya mkutano na waandishi wa habari. Hata hivyo, kabla ya hapo, tunapenda kuelezea yafuatayo yanayojiri katika zoezi la upigaji kura linaloendelea:

1. Utaratibu wa kupiga kura ndani ya kituo unachukua muda mrefu na kusababisha watu kukaa muda mrefu kwenye mistari. Ni muhimu wasimamizi na wasimamizi wasaidizi vituoni kuharakisha zoezi hili ili wananchi wasikate tamaa na kuamua kuondoka.

2. Wapo wapiga kura waliojiandikisha na wakapewa kadi za kupiga kura lakini majina yao leo hayajaonekana kwenye orodha za wapiga kura vituoni. Tunaiomba Tume ifanye kila liwezekanalo ili wananchi hawa wapate haki yao ya kupiga kura. CCM inapenda kuona kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura anapiga kura na changamoto zilizojitokeza katika Tume zisiwe sababu ya watu kuikosa haki hii ya kikatiba.

3. Kumekuwa na ripoti mbalimbali zinazosambazwa na wafuasi wa vyama vya upinzani, nyingine zikiambatana na picha, zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikituhumu wizi wa kura. Pamoja na kwamba baadhi ya ripoti na picha hizi hazina maana yoyote, na nyingine ni za kutunga, na zinastahili kupuuzwa, tunaiomba Tume iwe inatoa maelezo ya mara kwa mara kuhusiana na yanayoripotiwa ili kuweka rekodi sahihi na kuwasaidia wananchi kutopotoshwa na propaganda za kisiasa. Tunasisitiza matumizi bora ya vyombo vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, katika kipindi hiki tete.

4. Bado tunasisitiza uchaguzi wa amani. Hadi sasa, katika sehemu kubwa ya nchi yetu, dalili zote zinaonyesha kwamba upigaji kura umekuwa wa utulivu. Viongozi wa CCM wa ngazi zote wameelekezwa kuwa macho dhidi ya hujuma kwa CCM. CCM inapenda kuzisaidia mamlaka husika kupata na kushughulikia na taarifa za uvunjifu wa amani na uvurugaji wa taratibu za uchaguzi. 

Mwana-CCM yoyote anayeshuhudia au kusikia mipango ya kuvunja amani na kuhujumu au kuvuruga zoezi la uchaguzi atume ujumbe mfupi kwenda nambari 15016, akielezea mahali alipo, tukio husika na ikiwezekana wahusika. Ujumbe huu ni bure. CCM itazishughulikia taarifa hizo na kuzipeleka kwa mamlaka husika.

Imetolewa na:-
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
25.10.2016

No comments: