Tuesday, October 13, 2015

BALOZI JUMA MWAPACHU AJITOA CCM


NAJIVUA UANACHAMA WA CCM.
BALOZI JUMA MWAPACHU.
Ndugu zangu,
Kesho ni siku muhimu katika kalenda ya Taifa letu. Tunamkumbuka marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetutoka miaka 16 iliyopita. Nadhani ni siku mwafaka kwangu kufanya maamuzi magumu katika maisha yangu ambayo yanahusu uanasiasa wangu. Mimi ni mwanachama wa CCM tangu mwaka 1967 wakati nilipojiunga na TANU Youth League. Nimepata fursa ya kuwa
kiongozi ndani ya Chama hiki. Lakini kuanzia kesho mimi si mwanachama wa CCM tena. Natoa maelezo yafuatayo:
Kwa kipindi chapata mwezi na nusu hivi sasa mmekuwa mkisoma makala zangu kuhusu msimamo na mwelekeo wangu katika masuala ya siasa za hapa nchini hususan kuhusu uchaguzi mkuu na mstakabali wa demokrasia nchini mwetu. Nyote mnatambua kwamba kuanzia mchakato wa kumpata mgombe wa Urais ndani ya CCM kule Dodoma, ambako nilipiga kambi, sijayumba katika msimamo wangu kwamba Edward Ngoyai Lowassa ndiye chaguo langu katika kampeni za kumpata Rais mpya wa Taifa letu.
Chaguo langu si ndoto wala mlipuko wa mapenzi juu ya Lowassa. Nimemfahamu Lowassa tangu miaka ya 90 nikiwa cadre wa Chama cha Mapinduzi kwa mahusisho katika majukumu ya Kichama. Lowassa amejaaliwa nuru na uwezo wa kuongoza na wa kupendwa na watu. Ni msikivu pamoja na kwamba ni kiongozi asiyependa ukiritimba na utovu wa nidhamu, iwe kwa upande wa watumishi au wananchi wenyewe. Kubwa kwake ni ucha Mungu wake ambao unamsaidia sana katika uongozi unaojali na kuheshimu utu, ukweli na uwazi. Wanaodhani au kutaharuki kwamba eti anaweza au ana hulka ya kulipiza kisasi kwa jambo lolote lile ni waongo; wanajilinda.
Lowassa ni chaguo la wengi na CCM, katika busara yake ya kumuengua katika mchakato wa kumpata mgombea wa Urais, kimedhihirisha kutokuwa Chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia. Dalili za Chama hiki kupoteza lengo la kuwa Chama cha watu, na kuwa cha viongozi wachache zilianza siku nyingi na hasa katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. CCM kimebadilika na kuwa Chama cha makundi na migawanyiko yakupambana, si kwa malengo ya itikadi na ujenzi wa Chama, bali ya kumalizana na kutaka kufukuzana. Lowassa angeweza kufukuzwa miaka mingi tu iliyopita! Aliweza kushinda vita hivyo kutokana na kupendwa na wengi ndani ya CCM. Hivyo, kujitoa kwake uanachama wa CCM hivi karibuni ni sahihi kabisa kwasababu CCM si Chama tena cha watu. Kimetekwa. Na mimi nakubaliana na msimamo wa Lowassa na hao waliyofuata kutoka nadani ya CCM.
Niliwahi kuandika makala katika ukurasa huu nikimnukuu mshairi mmoja wa Uingereza aliyeandika kwamba, ‘there comes a time when the door opens and allows the future in’. Mlango huo sasa umefunguka usoni mwangu na huu uamuzi wangu maana yake ni kukubali kwamba wakati mpya umewadia; ni wakati wa mabadiliko. Kuendelea kujihisi kwamba ningali mwana CCM wa kadi ni kukubali kujidanganya mwenyewe. Si sawa. Kama marehemu Baba wa Taifa alivyowahi kusema, ‘CCM si mama yangu’.
Hivyo ndugu zangu, kuanzia kesho mimi si mwana CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya kata yangu Mikocheni, Dar-es-Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na Chama kingine. Mwenyezi Mungu anilinde.

No comments: