Sunday, October 25, 2015

NAAMINI UCHAGUZI UTAKUWA WA AMANI-WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA


index*Apiga kura, ataka Watanzania waendelee kumuomba Mungu
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema anaamini kwamba uchaguzi wa Rais,
wabunge na madiwani unaoendelea nchini kote leo, utafanyika wa amani
na utulivu.
Akizungumza mara baada ya kupiga kura leo asubuhi (Jumapili, Oktoba
25, 2015) katika kijiji cha Kibaoni, wilaya ya Mlele, mkoa wa Katavi,
Waziri Mkuu Pinda amesema hali aliyoiona tangu asubuhi inatia
matumaini.
Waziri Mkuu ambaye alipiga kura leo saa 3:10 asubuhi, alisema: “Watu
wamejitokeza kwa wingi. Ninawasihi Watanzania waendelee kumuomba Mungu
ili uchaguzi umalizike kwa amani. Lakini zaidi tuendelee kumuomba
Mungu ili amani tuliyonayo iendelee kudumu,” alisema.
Akizungumzia hali aliyoikuta kwenye kituo chake cha kupigia kura,
Waziri Mkuu alisema amefurahi kuona utaratibu mzuri uliopangwa wa
kutenganisha wapigakura. “Nimekuta akinamama wana mistari yao,
akinababa wana mistari na hapa kituoni kuna sehemu nne za kupigia
kura,” alisema.
Alisema kwa wastani mtu mmoja anatumia dakika mbili tangu kuhakikiwa
hadi kupiga kura. “Hii ni dalili njema kuwa kuna utaratibu mzuri na
kwamba watu watamaliza mapema kupiga kura,” alisema.
Aliwataka wapigakura kote nchini wakimaliza kupiga kura waende
majumbani kwao ikiwa ni kuitikia maelekezo ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi yanayowataka wananchi wasifanye mikusanyiko mita 200 kutoka
kwenye kituo cha kupigia kura.
Naye msimamizi wa kituo hicho ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya
Kibaoni, Bw. Thomas Senga alisema watu wamejitokeza mapema tangu saa 1
asubuhi. Alipoulizwa endapo mtu aliyesahau shahada yake lakini jina
lake lipo kwenye orodha ya waliojiandikisha ataruhusiwa kupiga kura,
alijibu kwamba mtu wa aina hiyo hataruhusiwa kupiga kura.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 25, 2015.

No comments: