Tuesday, October 13, 2015

WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA YAENDELEA NA JUHUDI ZA KUWAINUA WANANCHI

 Meneja Biashara kutoka shirika la Mzinga Morogoro Pingu Kamenyi akiwaeleza wandishi wa habari leo jijini Dar es salaam (hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya Shirika hilo katika kipindi cha Miaka kumi ya Serikali ya awamu ya nne ikiwemo uzalishaji wa zana bora  za kilimo na ujenzi zinazolenga kuwainua wajasiriamali wadogo ili waweze kuinua uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.  Wa pili kushoto ni Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Luteni Kanali Juma Nkangaa Sipe na wa kwanza kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) Frank Mvungi.
 Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Luteni Kanali Juma Nkangaa Sipe akitoa wito kwa watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa na Shirika la Mzingira ambalo ni moja ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  leo jijini Dar es salaam. Wa pili kulia ni Meneja Biashara kutoka shirika la Mzinga Morogoro Pingu Kamenyi.
 Miundo mbinu ya umwagiliaji katika shamba la mpunga.
 Moja ya Bwawa lililojengwa kwa ustadi na shirika la Mzinga.

 Mashine ya kutengeneza matofali inayotumia umeme.
 Mashine ya Kuchanganya Chakula cha Mifugo
 Mashine ya Kupukuchua Mahindi.
 Mashine ya Kukoboa Nafaka
Mashine ya Kuranda Mbao.

Frank Mvungi-MAELEZO
Serikali kupita Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeendelea kuwainua wananchi kupitia shirika la Mzinga kwa kuzalisha zana za kilimo, ufugaji na Ujenzi zitakazosaidia kukuza na kuongeza kasi ya uzalishaji wenye tija katika sekta hizo.

Hayo yamesemwa na Meneja biashara wa Shirika hilo jana jijini Dar es salaam Bw. Pingu Kamenyi wakati wa mkutano na wandishi wa habari uliolenga kueleza mafanikio ya shirika hilo katika kipindi cha miaka kumi ya Serikali ya Awamu ya Nne.

Akifafanua Kamenyi amesema  Serikali imepata mafanikio makubwa  kupitia shirika hilo kwa  kutekeleza miradi mbalimbali kama vile Ujenzi wa daraja la Mabwepande wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, Ujenzi wa nyumba za Halmashauri ya Masasi mkoani Mtwara, Ujenzi wa jengo la utawala la Hospitali ya Wilaya ya Morogoro na Ujenzi wa uzio wa Halmashauri ya Manispaa hiyo.

“Shirika la Mzinga lilianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi ili waweze kujikomboa kiuchumi ndiyo sababu iliyopelekea kuanzishwa kwa kampuni Tanzu ya Mzinga inayotekeleza miradi kama vile ya ujenzi. “Alisisitiza Kamenyi.

Shirika limekuwa na ushirikiano mzuri katika kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini.

Baadhi ya taasisi hizo zinajishughulisha na utafiti na maendeleo ni hapa nchini ni pamoja COSTECH, CoET, CAMARTECTIRDO lengo likiwa kupata teknolojia za kurahisisha utendaji kazi katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuwainua wananchi kiuchumi.

Katika jitihada za kupanua huduma zake, Kamenyi amebainisha kuwa shirika hilo limefungua vituo  vya kuuza milipuko, silaha na risasi za kiraia, na pia wameweza kufungua vituo vinne zaidi vya mauzo katika miji ya  Mererani , Arusha  , Shinyanga  na Mpanda.

Naye Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Luteni Kanali Juma Sipe alibainisha kuwa shirika hilo ni Kitovu cha maendeleo kwa kuwa lengo lake ni kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuhakikisha wanapata zana bora za uzalishaji kwa gharama nafuu.

Pia Luteni Kanali Sipe aliwaasa watanzania kutumia zana zinazozalishwa na shirika hilo  na zile zinazozalishwa na shirika la Nyumbu kwa kuwa zina ubora na zinalenga katika kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.

Shirika la Mzinga lilianzishwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China mnamo mwaka 1971 kama mradi chini ya Makao Makuu ya Jeshi (MMJ).

Kuanzia tarehe 13 Septemba mwaka1974, mradi ulibadilishwa kuwa Shirika la Umma (Public Corporation) kwa Tamko la Serikali No.219.

   
Post a Comment