JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapenda kutoa taarifa kwa umma kuhusu utangazaji wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu kwa vyombo vya utangazaji kwa mujibu wa Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015. Kanuni hizi zipo kwa mujibu wa Sheria kama ilivyotolewa na Gazeti la Serikali la Tarehe 26 Juni, 2015. Kanuni hizi zinalenga kuweka utaratibu mzuri wa kutangaza shughuli za kampeni na uchaguzi mkuu kuwa wa amani na utulivu.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inapenda kuwakumbusha kuwa ni marufuku kwa vituo vyote vya utangazaji kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu bila kupata taarifa sahihi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa utaratibu waliojiwekea.
Vilevile, vituo vyote vya utangazaji vinapaswa kuzigatia Sheria na Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015.
Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015, Na. 16 (1) na 16(2) inaelekeza kama ifuatavyo:-
16(1) kwamba kila mtoa huduma za maudhui atakuwa na wajibu wa kuuarifu umma juu ya matokeo ya uchaguzi, kadiri yanavyopatikana. uangalizi maalumu ufanyike kuhakikisha usahihi wa matokeo yote yanayotangazwa.
16(2) Mtoa huduma za maudhui hatatangaza maoni ambayo yanaweza kuchochea vurugu au kuhamasisha chuki kwa misingi ya mbari, kabila, jinsia, dini au Imani za kisiasa na ambayo yanajenga uchochezi wa kusababisha madhara.
Hivyo basi, vituo vya utangazaji vinatakiwa kufuata kikamilifu Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015 na kwamba vituo vya utangazaji vitawajibika na matokeo ya maudhui ya matangazo ambayo hayatozingatia Kanuni.
Mamlaka inatoa wito kwa vituo vya utangazaji kutumia weledi katika maamuzi ya kihariri kuchanganua kipi kinafaa kutangazwa na uangalizi maalumu ufanyike kuhakikisha kuna usahihi katika kutangaza matokeo yote yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
IMETOLEWA NA:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAREHE 25/10/2015
Comments