Friday, September 11, 2015

PALESTINA KUPEPESHA BENDERA YAKE MAKAO MAKUU YA UMOJA WA MATAIFA

   Bendera ya  Palestine itapepea nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,   hii inafuatia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  kupitisha azimio ambalo linatoa fursa kwa nchi ambazo si  mwanachama kamili wa Umoja huo  kupeperusha bendera yake Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Ubao wa Matangazo ndani ya Ukumbi Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  ukionyesha matokeo ya kura katika tukio la kihistoria  kufanyika ambapo Baraza hilo  limepitisha azimio linalotoa fursa kwa Palestina kupeperusha bendera yake. Nchi wanachama walipiga makofi kushangilia kupitishwa kwa azimio hilo, ambalo Israel imesema Palestina inatafuta umaarufu kwa njia za mkato badala  ya kurejea kwenye meza ya mazugumzo.
 
Na Mwandishi Maalum New York
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  jana Alhamis, limepitisha Azimio ambalo kwa mara ya kwanza   tangu kuanzishwa kwa Umoja huo, litaruhusu nchi ambazo  siyo mwanachama kamili kupeperusha  bendera yake katika  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kupitishwa kwa azimio hilo ambalo  limepigiwa kura  za ndiyo 119 za hapana  nane na zisizofungamana na upande wowote 45 kunaipa   fursa Palestina kupeperusha bendera yake nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mara baada ya  matokeo ya kura kutangazwa rasmi, Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa walipiga makofi kama ishara ya kufurahia kupitishwa kura nyingi azimio hilo.

Palestina   kama ilivyo kwa Vatican inahadhi ya Nchi Mwangalizi isiyo Mwanachama wa Umoja wa Mataifa (Non -Member Observer States)
Kwa mujibu wa  Azimio hilo nambaA/69/L.87 linaloelezwa kuwa ni la kihistoria, linamtaka   Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba Bendera  ya Palestina inapeperushwa ndani ya siku 20  ( septemba 30)wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la  70 la Umoja wa Mataifa.

Akiwasilisha azimio hilo mbele ya  wajumbe,  Mwakilishi wa Kudumu wa  Iraq na ambaye ni mwenyekiti wa kundi la nchi za kiarabu alisema  kupeperushwa kwa bendera ya   Palestina ni kielelezo  cha utekelezaji wa matakwa yaliyomo ndani ya Katiba ya Umoja wa Mataifa ya kwamba, nchi zote  na watu wake wako sawa na wana haki  sawa.

No comments: