
(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
……………………….
Na Modewjiblog team, Mwanza
Umoja wa Mataifa (UN) umesema utaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kulinda na kudumisha amani ya pamoja kwa makundi yote ili amani iliyopo itumike kuleta maendeleo endelevu nchini.
Hayo yamebainishwa na Mgeni rasmi Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues, wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Amani Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza (Septemba 21.2015).
Bi.Rodgrigues amesema amani ya pamoja inatoa nafasi kwa kila mmoja kuwa mshirika wa kudumisha na kuendeleza amani bila kujali itikadi, imani au matabaka mbalimbali yaliyipo ndani ya jamii.
Amefafanua kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika kulinda amani, hivyo nguvu ya pamoja ni muhimu katika kufikia malengo na maendeleo yanayotakiwa kutokana na kuwepo kwa utulivu, mshikamano, umoja, na amani.
Kwa upande wake, Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewataka watanzania kuachana na propaganda za kisiasa zinazoleta chuki na hasa katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Jaji Mutungi ameeleza kuwa amani haina tabaka na kusisitiza umuhimu wa wananchi kupiga kura kwa kutumia falsafa ya kulipenda taifa na kuwaonya viongozi wa vyama vya siasa kuacha kuwadharau watanzania ambao wameilinda amani kwa muda mrefu.
Nalo Jeshi la Polisi mkoani humo, limelaani kitendo kilichofanywa na watu wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa vyama vya siasa kwa kushambulia polisi na kuvunja vioo vya gari la polisi kwa kusingizio cha kampeni za uchaguzi.
Katika tukio hilo imeelezwa kuwa, baada ya watu waliokuwa wakitokea katika mkutano wa kampeni wa umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) kushambulia Polisi, kuvunja vioo vya gari la polisi na kujeruhi askari.
No comments:
Post a Comment