Monday, September 28, 2015

BENKI YA EXIM YATOA MSAADA WA MADAWATI SHINYANGA.

 Meneja wa benki ya Exim Tanzania tawi la Shinyanga  Bw. Emmanuel Nkelebe akijiandaa kukata utepe ikiwa ni ishara ya kukabidhi msaada wa madawati 50 kwa shule ya msingi Mapinduzi ‘A’ iliyopo Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni muendelezo wa mpango wa benki hiyo katika kuboresha ubora wa elimu hapa nchini. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mwenyeki wa Bodi ya shule hiyo Bw. Sylvester senga (wa tatu kulia) na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo.
Meneja wa benki ya Exim Tanzania tawi la Shinyanga  Bw. Emmanuel Nkelebe akizungumza na mmoja wa wanafunzi wa shule ya Msingi Mapinduzi ‘A’ iliyopo manispaa ya Shinyanga mara baada ya kukabidhi msaada wa madawati 50 kwa shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa mpango wa benki hiyo katika kuboresha ubora wa elimu hapa nchini

Na Mwandishi wetu,
BENKI ya Exim Tanzania imetoa msaada wa madawati 50 kwa shule ya msingi Mapinduzi ‘A’ iliyopo Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni muendelezo wa mpango wa benki hiyo katika kuboresha ubora wa elimu hapa nchini.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi madawati hayo iliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Meneja wa benki hiyo tawi la Shinyanga  Bw. Emmanuel Nkelebe alisema msaada huo wenye thamani ya sh. Milioni nne ni sehemu tu jitihada ambazo benki hiyo imekuwa ikifanya kusaidia jamii inayoizunguka.

Alisema kuwa benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika kufanikisha mipango mbalimbali hususani katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini hatua aliyoilezea kuwa ndio chachu ya maendeleo kwa sekta zote ikiwemo ya benki pia.

“Mchango wetu huu wa kuchangia katika elimu unatokana na imani yetu kwamba bila kuwa na jamii iliyoelimika hata huduma za kibenki tunazozitoa lazima zitateteleka kutokana na ukweli kuwa biashara yetu hii inategemea sana mafanikio ya jamii inayotuzunguka…mafanikio ambayo tunaamini yataletwa na elimu,’’ alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, mkuu wa shule Bi Savera Rwabuyongo pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo alisema msaada huo umepatikana kwa wakati muafaka kwa kuwa shule hiyo ipo kwenye mkakati wa kutafuta madawati zaidi kutokana na uhaba wa madawati unaoikabili shule hiyo.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 816 wakiwemo wanafunzi wa kiume 342 na  wa kike 474 kwa sasa bado inakabiliwa na uhaba wa madawati 93 zaidi na hivyo kutoa wito kwa taasisi na mashirika mengine kuiga mfano wa benki hiyo kwa kuisadia zaidi shule hiyo.

Akitoa neno la shukrani kwa benki hiyo kwa niaba ya wanafunzi wenzie, mwanafunzi Musa Peter alisema msaada huo ni sawa na ukombozi kwao kwa kuwa awali walikuwa wanapata maumivu na uchovu mwingi kutokana na wao kukaa chini hali iliyokuwa ikichangia uzorotaji wa ufahulu wao darasani.

“Tunashukuru sana benki ya Exim kwa msaada huu kwa kuwa sasa tunauhakika wa kusoma tukiwa tumekaa kwenye madawati na tunaahidi kuyatunza madawati haya.Zaidi tunaomba na wasamalia wema wengine waje watusaidie kwa sababu bado tunahitaji madawati zaidi,’’ alisema.

No comments: