Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eusella Bhalalusesa akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome kuzindua maonesho ya Tehama yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
………………………………………….
Na mwandishi wetu
JUMLA ya wanafunzi 60,000 katika shule 150 nchini wamepitiwa na mafunzo ya programu ya Bridge IT yenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kidijiti (digital technology) katika ufundishaji na ujifunzaji wa Hisabati,Sayansi na Stadi za Maisha.
Hayo yamsemwa na Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eusella Bhalalusesa akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome kuzindua maonesho ya Tehama.
Alisema kutokana na mafanikio yaliyotokea sasa wanatanua wigo baada ya kuwezeshwa kifedha na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya elimu (Global Partnership For Education) kwa ajili ya kuendeleza teknolojia hiyo katika kujifunza na kufundisha katika shule za msingi na hasa darasa la awali la kwanza hadi la nne.
Aidha maonesho hayo yanayofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere yana lengo la kuonesha ubunifu ambao upo tayari kutumika kufanikisha mafunzo hayo.
Pia maonesho hayo yanatarajia kujadili na kuangalia mbinu za kielektroniki zitakazoweza kuendana na mazingira ya Tanzania katika ufundishaji na kujifunza kwa gharama nafuu.
Pia wanatarajia kuangalia utayari wa walimu na namna ya kuwabadilisha mtazamo ili waweze kufundisha na kufundishika.
“Lengo la serikali kupitia Wizara ya Elimu ni kupanua wigo wa elimu hasa elimu ya awali kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo itabadilisha ufundishaji kutoka kutumia vitabu vilivyopo katika mfumo wa ‘hard copy’ na kuwa katika mfumo wa sauti na picha au ‘soft copy’,” alisema Profesa Bhalalusesa.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifuatilia kwa makini risala Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eusella Bhalalusesa (hayupo pichani).
Alisema hadi kufikia wakati huu serikali imeshapiga hatua kubwa katika matumizi ya Tehama ambayo katika majaribio yake yameonesha kufanikiwa na wadau mbalimbali wa elimu wameyapongeza na kuyaunga mkono.
Profesa Bhalalusesa alisema kwa sasa wagunduzi mbalimbali wa mifumo ya Kompyuta inayoweza kutumika kufundishia ndio watakoonesha kazi zao na kutoa ufafanuzi wa kina kwa majaji wataochagua kazi chache na kuzifanyia majaribio kabla ya kuanza kutumika kufundishia.
Kwa Upande wake Mratibu wa Mpango wa Kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kutoka Wizara ya Elimu, Agripina Habichi alisema mpango huo wa matumizi ya Tehama utasaidia wanafunzi kufahamu kusoma na kuandika kabla ya kuendelea na masomo ya darasa la tatu.
“Maonesho haya yanafanyika katika wakati muafaka ukizingatia tunataka kupiga hatua kubwa katika kuboresha elimu yetu. Washiriki wa maonesho haya wamekuja kutuonesha utawaalamu wao unaoweza kutumika kufundishia.
Lengo letu ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi ambapo tumeazimia kuzifikia shule zaidi ya 2000 katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 na hivyo tutakuwa katika kiwango bora zaidi cha utoaji wa elimu inayojitosheleza,” alisema Habichi.
Comments