Wednesday, September 23, 2015

WANAWAKE WALIOPONA FISTULA CCBRT WAAMUA KUJIAJIRI

 Mratibu wa Kituo cha Mabinti centre cha mikocheni jijini Dar es Salaam Bi. Katia Geurts(kulia) akimwelezea jambo Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa  Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia(katikati) na waandishi wa habari jinsi kazi za ushonaji zinazofanywa na baadhi ya wakina mama waliotibiwa na kupona  fistula wakati walipotembelea kituo hicho na kujionea miradi mbalimbalia inayofadhiliwa na Vodacom Foundation,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu katika Hospital ya CCBRT na kupona  ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.
 Mmoja  wasichana  wa kituo cha Mabinti Centre cha mikocheni jijini Dar es Salaam aliyepata kutibiwa Fistula, Happiness Christopher(kushoto)akimsikiliza Mratibu wa Kituo hicho, Katia Geurts wapili toka kushoto akimuonesha nguo anayoendelea kuishona binti huyo  wakati walipotembelea kituo hicho na kujionea miradi mbalimbalia inayofadhiliwa na Vodacom Foundation,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu katika Hospital ya CCBRT na kupona  ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.
 Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia(kushoto)akichagua moja ya begi lililoshonwa na wakina mama wa kituo cha Mabinti centre kilichopo mikocheni jijini Dar es Salaam wakati alipowatembelea kituoni hapo  na kujionea miradi mbalimbalia inayofadhiliwa na Vodacom Foundation,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu katika Hospital ya CCBRT na kupona  ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.Kulia ni Cherry David.


Wanawake waliotibiwa na hatimaye kupona  fistula katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam wameamua kujikita katika sanaa ya kazi za mikono kwa lengo la kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini.

Takribani wanawake wapatao 81, chini ya mpango madhubuti ulioratibiwa na hospitali ya CCBRT, wamekuwa wakihitimu mafunzo mbalimbali ya kazi za mikono zikiwemo sanaa za ushonaji wa batiki, nguo za aina tofauti, utengenezaji wa mabegi, kofia, ususi na kadhalika, katika Kituo kinachoendeshwa na hospitali hiyo kijulikanacho kama ‘Mabinti centre’ tangu mwaka 2007.

Akizungumza mbele ya ujumbe wa wadhamini waliotembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Kituo hicho, Katia Geurts, alisema kituo hicho kinatoa mafunzo mahususi kwa wakinamama waliopona baada ya kusumbuliwa na fistula.

“Wengi wao wanatoka katika familia duni, hivyo mafunzo haya wanayoyapata baada ya kumaliza matibabu ya Fistula yanakwenda kuwasaidia kujiajiri wao wenyewe jambo linalowasaidia kupunguza ukali wa maisha,” alisema Geurts.

Aliongeza kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo kituo hicho huwapatia vyeti vya uhitimu vinavyotambulika, sanjari na vitendea kazi vinavyoendana na stadi stahiki aliyohitimu mwanafunzi kwa minajiri ya kuwarahisishia upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha yao.

Nae Mkufunzi wa Kituo hicho ambaye awali alikuwa mmoja wa waathirika wa ugonjwa wa fistula hospitalini hapo, Jane Rugalabamu, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aanze kufundisha wenzake kituoni hapo amebaini kuna idadi kubwa ya wanawake wenye matatizo ya fistula ndani ya jamii lakini waume zao wamekuwa wakiwaficha kwa dhana ya kufisha aibu.

“Kuna haja kubwa ya kuelimisha akinababa wawaruhusu wake zao wenye matatizo waje kutibiwa. Fistula ni hali inayotibika na wala sio hali ya  kurogwa kama wengi wanavyodhani, sisi sote hapa kwenye kituo cha mabinti tulikuwa na hali hiyo na sasa tumepona kabisa wanawake jitokezeni,” alisema Rugalabamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia,  baada ya kukagua shughuli mbalimbali za mafunzo zinazoendelea kituoni hapo, alisema kwa niaba ya wafanyakazi wa Vodacom na Vodafone duniani kote, wataendelea kuwasaidia akinamama wote wanaopatwa na hali hiyo ya fistula hatua kwa hatua, sanjari na kuhakikisha wanazidisha kasi katika kampeni inayoendelea dhidi ya hali hiyo.

“Tutaendelea kuwa karibu zaidi na waathirika wa fistula kuanzia hatua ya kuwasafirisha kutoka vijijini na mikoani kwa kuwatumia fedha kupitia huduma yetu ya M-Pesa, pia tutakuwa pamoja wakati wote wa matibabu na baada ya kupona tutawaunga mkono kwenye mafunzo kama haya ili kuwaletea ustawi ulio bora kwa maisha bora kwa ajili yao na familia zao,” alisema Mworia.  

No comments: