Tuesday, September 29, 2015

MWILI WA MAREHEMU CELINA KOMBANI WAAGWA DAR ES SALAAM

1333Askari wa Bunge wakibeba Jeneza lenye mwili wa marehemu Celina Kombani, wakati likiwasili kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam Septemba 28, 2015.
…………………………………………………..
Na Ally Daud –Maelezo Dar es salaam
Mwili wa marehemu wa aliyekuwa Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Celina Ompeshi Kombani (56) umeagwa Septemba 28, 2015  Katika Viwanja vya Karemjee jijini Dar es salaam.
Waziri huyo ambae pia alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Ulanga Mashariki amefariki dunia Septemba 24, mwaka huu katika hospitali ya Apollo Nchini India kutokana na ugonjwa wa saratani ya kongosho.
Maelfu ya waombolezaji yakiongozwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Galib Bilal pamoja na Mke wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere na Mke wa Rais wa Tanzania Mama Salma Kikwete katika hafla fupi ya kuaga mwili wa marehemu kabla ya kusafirisha kuelekea Morogoro kwa ajili ya mazishi .
Wawakilishi wa mashirika na viongozi mbalimbali wa nchi walihudhuria katika viwanja hivyo wakiwemo mawaziri wa Tanzania Bara na Visiwani wakiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anna Makinda ili kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Marehemu Kombani anatarajiwa kuzikwa kesho katika shamba lake huko Morogoro baada ya waombolezaji kupata nafasi ya kutoa heshima za mwisho katika viwanja wa Jamhuri mjini humo.
Aidha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anna Makinda ametoa pole kwa wafiwa na kusisitiza kwamba jamii iendeleze ya yaliyoachwa na marehemu kwa ajili ya kujenga Taifa letu kwani alikuwa mstari wa mbele katika kupigania kuondoa malipo hewa ya watumishi wa Umma, kufanyakazi kwa bidii na kujawali watu .
Mbali na hayo Makamu wa Rais wa pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema wamepokea taarifa hizo kwa mstuko mkubwa kwani hawakutarajia kuachiwa pengo na Celina Kombani.
Vile vile Mwenyekiti na mwakilishi wa kituo cha kulelea yatima Good Hope Family ya Kigamboni Bw. Omari Rajabu amewaasa viongozi waliobakia kutowasahau kwani wamepoteza mama yao wa dunia ambaye alikuwa mstari wa mbele kuwapigania watu wasiojiweza.
Marehemu Kombani ameacha mume , watoto watano na wajukuu wanne pia ameacha pengo kubwa katika Serikali ya Jamhuri wa Muungano Wa Tanzania.
Post a Comment