Thursday, September 17, 2015

KIAMA CHA MAJANGILI CHAJA, BATHAWK YAZINDUA NDEGE MAALUM KUPAMBANA NAO

Ndege aina ya Super Bat DA-50
…………………………..
Na Daniel Mbega, Mkomazi
NI majira ya saa tatu asubuhi Jumatano, Septemba 16, 2015 wakati tunawasili kwenye uwanja
mdogo wa ndege (air strip) katika eneo la Kisima ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Mkomazi inayotenganisha mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Uwanja unaonekana
mweupe, hakuna ndege! Nikashangaa kwa sababu wenyeji wetu kampuni ya Bathawk
Recon wametuambia tunakuja kushuhudia uzinduzi wa ndege maalum zinazopambana na
ujangili.
Kilichoonekana mbele yetu ni hema kubwa ambalo mbele yake kulionekana minara midogo
iliyosimikwa kama fimbo. Kwenye banda kubwa ikaonekana ndege ndogo aina ya Twin
otter. Nikadhani ndiyo inayozinduliwa, lakini Idrisa Jaffary, mwenyei wetu
tuliyekuwa naye kwenye gari akasema, hapa siyo hiyo.
Mshangao ukanipata baada ya gari kusimama wakati nilipokiona kifaa mfano wa ndege kikiwa
kimeegeshwa kwenye bomba maalum kana kwamba ndege inataka kupaa.
Kama nisingekuwa
nazifahamu ndege hizi maarufu kama drones,
ningeweza kusema kwamba huo ni mdoli ambao mwanangu angefurahia kama
ningempelekea akauchezea.
Kwa siku za karibuni zimekuwa maarufu kwani zinatumika kupeleka misaada mbalimbali hata
katika maeneo hatari ya vita ambako hakufikiki kirahisi.
“Hii ndiyo
ndege yenyewe,” Idrisa akatueleza. “Hee! Ndiyo hii?” tukajiuliza kwa mshangao. Kwamba
Tanzania tumeanza kuitumia teknoloia hii yanaweza kuwa maendeleo mengine mapya.
Mshangao
wetu ulimalizika wakati Phil Jones, ofisa mwendeshaji wa mitambo hiyo kutoka
kampuni ya MartinUAV ya Marekani iliyotengeneza ndege hiyo aina ya
Super Bat DA-50 UAV, alipoanza kutuelezea namna ‘ndege’hiyo (drone)

inavyofanya kazi huku akituonyesha kila sehemu na kazi yake.
“Hii ni ndege ambayo haihitaji kuwa na
rubani, inaongozwa kwa kompyuta maalum, ina antenna mbili, ina kamera maalum
ambazo zinaweza kupiga picha usiku na hata mchana,” akatueleza.
Akasema ndege hiyo ina uwezo wa kuruka
urefu wa futi 20,000 kutoka usawa wa bahari na kwenda katika nusu kipenyo cha
kilometa 35 kutoka ilipo mitambo ya kuiongoza.
Jones, ambaye baadaye alinieleza kwamba
yeye rubani wa zamani wa ndege za kijeshi katika Jeshi la Uingereza aliyestaafu
mwaka 2014 ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, akasema ndege hiyo
inayorushwa kwa mtindo wa manati (catapult
launch system
), inaweza kuruka mfululizo kwa muda wa saa 10 ikiwa angani
kabla ya kutua na kujazwa mafuta tena.
“Ina mfumo maalum wa kamera ambazo zina
uwezo wa kupiga picha hata usiku wa manane na kutambua mienendo ya viumbe wenye
damu ya moto kama hayawani na binadamu, hivyo ni rahisi kubaini kama kuna
majangili,” akafafanua.
Baada ya maelezo ya takribani nusu saa, hatimaye yeye na wasaidizi wake
wakaamua kuirusha ndege hiyo baada ya kuiwasha. Ilichomoka kwa kasi ya ajabu na
kuelekea angani ikaanza kuzunguka.
Hapo ndipo tukasogezwa kwenye hema kubwa ambako tuliwakuta wasaidizi
wake – Austin Howard na Kory Ferguson – wakiendesha kompyuta hizo na
tukashuhudia mazingira halisi ya hifadhi katika eneo husika pamoja na kuona
wanyama mbalimbali.
“Sasa hapa unaweza kuona kama kuna wavamizi (majangili) na inakuwa
rahisi kuwasiliana na askari wa wanyama pori na kwenda kwenye eneo husika
kuwakamata,” anasema Jones.
Hata ilipotua, ilikuja kama ndege za kawaida zinavyokuja, tofauti yake
tu yenyewe haina magurudumu. Naam, unaweza kuwa ufumbuzi mwingine wa kupambana
na ujangili nchini, tatizo ambalo haliko Tanzania tu, bali katika nchi nyingi
barani Afrika.
Post a Comment