Thursday, October 17, 2013

Waziri Mkuu Mizengo Pinda Awasili China apokea Taarifa Kutoka Kwa Balozi wa Tanzania nchini China Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo

 Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda na Mkewe Tunu wakimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini China Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo(kushoto)wakati aliposoma taarifa kwa Waziri Mkuu  ambaye Oktoba 16, 2013 aliwasili mjiniBeijing kwa   ziara ya kikazi nchini China
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akiagana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya China  National Machinery Industry Federation na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya TBEA, Bw, Zhang Xin  baada a mazungumzo yao mjini Beijing Oktoba 16, 2013.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
----
 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewasili Beijing, China saa 10 jana jioni (Jumatano, Oktoba 16, 2013) na kuanza vikao ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo.

Mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Beijing, Waziri Mkuu alielekea kwenye nyumba ya wageni ya Serikali ya Diaoyatui ambako alipokea taarifa fupi kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini China.

Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali (Mst.), Abdulrahman Shimbo alisema sehemu kubwa ya utekelezaji wa miradi kati ya Tanzania na China iko chini ya mwamvuli wa FOCAC (Forum on Africa China Cooperation) ambayo inagawanyika katika maeneo sita.

Alyataja maeneo hayo kuwa ni misaada (grants), mikopo ya masharti nafuu (preferential loans), mikopo ya kibiashara (preferential buyers credit), uwekezaji, ushirikiano maalum na ushirkianao wa kihistoria.

“Miradi mahsusi inayogharimiwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na China imeongezeka sana na inatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni 800 ifikapo mwaka 2014/2015,” alisema Balozi Shimbo.

Kuhusu elimu na mafunzo, Balozi Shimbo alisema programu hiyo ambayo imeanza muda mrefu, hadi kufikia Desemba 2011, ilikuwa imekwishawanufaisha wanafunzi wa Kitanzania 110 na wataalamu 1,020 ambao walipatiwa mafunzo chini ya udhamini wa Serikali ya China.

Kwa mwaka huu 2013, Balozi Shimbo alisema kuna wanafunzi zaidi ya 300 ambao wanasoma nchini humo. “Hivi sasa kuna wanafunzi 31 wanaodhamimiwa na serikali ya Tanzania, wanafunzi 249 wanaofadhiliwa na serikali ya China na wengine zaidi ya 100 wanaojidhamini wenyewe katika shahada za Uzamili na Uzamivu,” alisema. 

Pia alisema Tanzania kwa kushirikiana na Dalian University of China, itanufaika na mradi wa kupandisha hadhi Chuo cha Usafiri wa Baharini (Dar es Salaam Maritime Institute) hadi kufikia ngazi ya Chuo Kikuu cha Kanda ya Afrika Mashariki.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhi kwa kampuni ya Kichina ya China Rail Engineering Group ambayo inakifufua kiwanda cha viatu na ngozi cha Zanzibar na kukifanya kiwe kiwanda cha samani. Kiwanda hicho kilijengwa kwa msaada wa Serikali ya China katika miaka ya 70.

Hata hivyo, Balozi Shimbo alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kimahusiano na China ambapo vijana wa Kitanzania 175 wapo katika magereza ya nchini China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwemo ya kusafirisha madawa ya kulevya.

“Kati ya hao, watatu uraia wao ni wa kutiliwa mashaka. Kati yao 48 wako China Bara, Hong Kong wapo 117 na Macao wapo 10. Kati ya hao 175, wanawake ni 34, ambapo 28 wako Hong Kong na sita wako China bara,” alisema.

Akizungumza na maafisa ubalozi pamoja na wajumbe wa msafara wake, Waziri Mkuu alisema tatizo la madawa ya kulevya linaharibu sifa ya Tanzania pamoja na mahusiano baina yake na nchi marafiki.

“Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja lakini cha kusikitisha zaidi ni idadi kubwa ya wanawake waliokamatwa…wizara zinazohusika inabidi tukae na kuweka mkakati wa pamoja,” alisema.

Kuhusu misaada ya China kwa Tanzania, Waziri Mkuu alisema, kuna miradi ya kufa na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake hii na kuiainisha kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, usambazaji wa umeme na ukuzaji wa utalii baina ya Tanzania na China hasa fursa ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa moja baina ya Chiona na Tanzania.

Leo(Alhamisi, Oktoba 17, 2013) Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Li Keqiang, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China na uongozi wa China Railway Jianchang Engineering. Pia atahudhuria dhifa ya Taifa itakayoandaliwa kwa heshima yake Leo jioni.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 16, 2013

No comments: