MAMIA WAJITOKEZA KWA WINGI KUTOA HESHIMA ZA MWISHO KWA MAMA WA MWANAHABARI MAHIRI WA ITV UFOO SARO ALIYEUWAWA KWA KUPIGWA RISASI TANO NA MZAZI MWENZA WA BINTI YAKE AMBAYE NAE ALIJERUHIWA KWA RISASI

 Mamia ya wakazi wa Kibaha mkoani pwani pamoja na jiji la Dar es Salaam leo walimiminika kwa wingi nyumbani kwa Marehemu Anastazia Saro Kibamba Kibwegere kutoa heshima za mwisho kwa mama wa Mwanahabari Ufoo Saro aliye uwawa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenza wa binti yake huyo ambaye pia alijeruhiwa kwa risasi. 

Kwa mujibu wa ripoti ya madkatari walioufanyia uvchunguzi mwili wa Marehemu, Muuaji ambaye alitambulika kwa jina la Anthery Mushi ambaye nae alijiua baada ya kutekeleza tukio hilo alimpiga risasi tano. 
 Mwili wa marehemu ukiingizwa katika Kanisa la KKKT Mtaa wa Kibwegere Kibamba kwa misa maalum,. Marehemu alikuwa akiimba kwaya ya Usharika huo.
  Mwili wa marehemu ukiwa nyumbani kwake.

 Mwili ukiwa ndani Kanisani
 Waombolezaji wakitoa heshima za mwisho wakiongozwa na baba mchungaji
  Mkurugenzi wa ITV na Redio One, Joyce Mhavile akitoa heshima za mwishi. Picha ya juu ni mwana jamii.
 Waombolezaji wakitoa heshima za mwisho pamoja na wanakwaya wenzake na Marehemu.
  Mtoto wa Ufoo, Alvin Mushi akiwa na masikitiko na majonzi makubwa baada ya kuondokewa na Bibi yake. Alvin anadaiwa kulelewa na Bibi na Babu.
  Ilikuwa simanzi kubwa kwa Bi Joyce Mhavile boss wa Ufoo Saro.
 Waombolezaji wakiwa kanisani hapo. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa ITV na Redio One, Joyce Mhavile ambaye wakati wa salamu zake alidai amemwakilisha Ufoo Saro ambaye yupo Hospitali na ameshindwa kuja kumuaga mama yake. Na amefanya hivyo kutokana na ombi la Ufoo.
  Waombolezaji...
  Rafiki wa siku nyingi wa Ufoo Saro, Julieth Ngalabali kutoka gazeti la Mwananchi akiwa amebebna shada la maua na mwombolezaji mwingine.
  Wanahabari waliofika msibani hapo.

 Nje ya Kanisa hilo.Picha Zote na Mdau Mroki Mroki
---- 
Mtaalam aeleza kwa nini muuaji aliua
  Anazikwa leo kijijini Shari,Machame
 
Mwili wa Anastazia Saro, mama mzazi wa mtangazaji na mwandishi wa kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Jumapili iliyopita, ulifanyiwa uchunguzi jana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), na kukutwa na risasi tano.
Anastazia aliyeuawa wakati akisuluhisha ugomvi kati ya binti yake Ufoo na mzazi mwenzie, Anthery Mushi, alikutwa na risasi hizo katika sehemu kadhaa za mwili wake.
  Mushi mbali na kumuua Anastazia, pia alimjeruhi kwa risasi Ufoo kisha kujilipua mwenyewe na kufariki dunia papo hapo.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Allelio Swai, Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya Anastazia wakati akizungumza na NIPASHE muda mfupi kabla ya mwili huo kutolewa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, na kupelekwa Kibamba kwa ajili ya ibada ya mazishi tayari kusafirishwa kwenda Machame kijiji cha Shari kwa ajili ya mazishi leo.

Swai alisema kuwa katika uchunguzi wa mwili huo ambao hata hivyo, hakumtaja daktari aliyeufanya, baadhi ya ndugu wa marehemu walihudhuria.

Swai alifafanua kuwa risasi hizo zilikutwa katika maeneo ya mapafu, maini na tumbo.
Kwa mujibu wa Swai mwili huo ulitakiwa kufanyiwa uchunguzi mapema asubuhi, lakini ulichelewa kutokana daktari huyo kuwa na majukunu mengine, walilazimika kusubiri kwa muda.

Mwili wa mama huyo uliondolewa hospitalini hapo saa 7:30 mchana baada ya kukamilika kwa taratibu zote.

Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo na kuondoa risasi hizo, alikataa kuzungumza chochote zaidi ya kusema: “Siwezi kulizungumzia jambo hili kwa kuwa nimeshakamilisha nilichotakiwa kukifanya.”

Baadhi ya ndugu wa marehemu Anastazia waliokuwapo eneo hilo na walioshuhudia uchunguzi wa mwili, walisikika wakisema kuwa kitendo alichokifanya Mushi ni cha kinyama kutokana na kutumia risasi nyingi kumuua ndugu yao.

Wakati huo huo, Ufoo hataweza kushiriki mazishi ya mama yake kutokana na matibabu anayoendelea kuyapata, hospitalini hapo.

Swai aliiambia NIPASHE kuwa walimtaarifu Ufoo juu ya mipango ya mazishi ya mama yake na kwamba naye ametoa ruhusa ili mama huyo azikwe hata kama yeye (Saro) hataweza kuhudhuria mazishi hayo kutokana na hali yake.

“Niliongea na Ufoo ili kumfahamisha kuhusu mipango ya mazishi naye alitutaka tuendelee na mipango hiyo hata kama yeye atashindwa kumzika mama yake, lakini cha msingi alituomba tuhakikishe kuwa mama yake anazikwa salama,” alisema Swai.

MWANASAIKOLOJIA AMZUNGUMZIA MUSHI
 Wakati hayo yakijiri, Mhadhiri Mwandamizi katika mambo ya Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Kitila Mkumbo, amesema kulingana na taarifa za mauaji ambazo amekuwa akizisoma kwenye vyombo vya habari juu ya mauaji hayo yalivyofanyika, ni dhahiri muuaji alikuwa amefikia ngazi ambayo hasingeweza kuacha kufanya unyama huo.
Alisema mtu huyo  alikuwa amejiandaa kufanya tukio hilo kwa muda mrefu kimkakati na kimaandalizi.

Alifafanua kuwa mhusika wa tukio hilo alikuwa ameshafikia katika hatua ya mwisho ya maamuzi inayoitwa tafsiri ya akili ambayo huwa ni vigumu kwa mtu kujizuia kutenda jambo.

Alisema kuna hatua tatu ambazo ni stress (msongo wa mawazo), depression (sonona) na tafsiri ya akili ambazo mtu anaweza kuzipitia kabla hajachukua maamuzi.
“Kuna kitu kinaitwa fluctuation, lazima kilitokea kati yake na familia hiyo siyo bure, lakini angekuwapo yeye mwenyewe angetueleza, sisi hatuwezi kujua,” alisema Dk. Mkumbo.
Dk. Mkumbo alisema kuwa sehemu aliyokuwa anafanya kazi marehemu Mushi (Darfur) siyo kigezo kikubwa cha kuamua kufanya tukio lile japokuwa watu wengi wanaoishi katika mazingira ya kuona maiti za watu huwa ni wepesi kuua.

Alisema hicho siyo kigezo cha marehemu kufanya kitendo hicho kwa kuwa hakuna mwanadamu asiyeogopa kifo.

Kuhusiana na iwapo wanajeshi wanaotoka katika operesheni za kijeshi nje ya nchi kama wanapatiwa ushauri (councelling), Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Erick Komba alisema: “Mafunzo anayopata mwanajeshi yanalenga kumjenga na kumpa uwezo wa kuyakabili mazingira mbalimbali ndani na nje ya nchi kimaumbile na kisaikolojia,” alisema.

Meja Komba alisema mwanajeshi ana uwezo wa kuishi kwenye mazingira yoyote kwa kipindi kirefu kijasiri.

“stress management-(jinsi ya kubaliana na msongo) inafanyika vizuri kwa kufanya michezo mbalimbali kwa pamoja ambayo inaimarisha fiziki (ukakamavu),”
Aliongeza kuwa maisha ya mwanajeshi ni ya umoja na ushirikiano, kitu ambacho kinamfanya ayakabili mazingira yake vizuri, na kuweza kutekeleza majukumu ya jeshi kiufasaha na kiuweledi. 

Alisema kwa kipindi wanapokuwa katika operesheni mbalimbali za ulinzi wa amani pamoja na mambo mengine wanapewa ushauri.

HALI YA UFOO YAZIDI KUIMARIKA Ofisa Habari wa  MNH, Aminiel Aligaesha, alisema jana kuwa hali ya Ufoo inaendelea vizuri kulinganisha na siku za nyuma.

Alisema kwa sasa yupo katika jengo la matibabu ya moyo na kueleza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya daktari anayemuhudumia, Ufoo anahitaji mapumziko zaidi.

“Kwa sasa Ufoo haitaji kuonana na mtu, anahitaji kupumzika zaidi kama daktari alivyoniambia na kwa kifupi yupo katika wodi ya kawaida tu,” alisema Aligaesha.

SIMANZI YATAWALA KUAGA ANASTAZIA Mwili wa marehemu Anastazia uliagwa jana katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibwegele Kibamba Shule kabla ya kuelekea kijiji cha Shari Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro kwa mazishi.
Waumini na wanakwaya ya Uinjilisti wa Kanisa hilo waliangua vilio baada ya jeneza la mwili wa marehemu ambaye alikuwa mwanakwaya na mweka hazina wa kanisa kufika kanisani hapo.

Kadhalika, ibada iligubikwa machozi na simanzi, hali iliyosababisha kusimama kwa muda.
Mchungaji wa Kanisa hilo, Magret Shekolowa, aliwaeleza waumini hao kuwa na moyo wa subira hasa katika kipindi hiki na kuwataka kuacha kulia badala yake waiombee Tanzania kwani kumekuwa na matukio mengi ya mauaji ya kinyama.

Akitoa salamu za rambirambi Mkurugenzi wa ITV, Joyce Mhavile, huku akitokwa na machozi ya huzuni alisema: “Jana nilikwenda kumuona Ufoo akaniomba nitoe salama za mwisho nisimame kwa niaba yake, nami nasema poleni sana.”

Marehemu alizaliwa mwaka 1957 huko Mbulu mkoani Arusha na alifariki juzi baada ya kushambuliwa kwa risasi tano na Mushi.

Imeandikwa na Samson Fridolin, Gwamaka Alipipi, Raphael Kibiriti na Margaret Malisa.
CHANZO: NIPASHE

Comments