Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth Minja akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)Jana jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi Septemba 2013 ambapo umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.7 ya mwezi Agosti 2013.
Badhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth Minja (hayupo pichani) wakati akielezea hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi septemba 2013 ambapo umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.7 ya mwezi Agosti 2013 jana jijini Dar es Salaam.
----
MFUMUKO WA BEI WA MWEZI SEPTEMBA, 2013
Ndugu waandishi wa habari, Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kuwashukuru kwa kuitikia mwito wa kuhudhuria mkutano huu. Naomba ifahamike kwamba, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina mamlaka ya kukusanya, kuchambua na kutoa takwimu rasmi za nchi kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351. Lengo la mkutano huu ni kuwafahamisha mambo makuu matatu;
Kwanza ni kuhusu mfumuko wa bei wa mwezi Septemba 2013 unaopimwa kwa kigezo cha mwaka, yaani; kwa kulinganisha fahirisi za bei za mwezi Septemba, 2013 na zile za mwezi Septemba, 2012;
Pili ni kuhusu mfumuko wa bei wa mwezi Septemba, 2013 unaopimwa kwa kigezo cha mwezi yaani; kwa kulinganisha fahirisi za bei za mwezi Septemba, 2013 na zile za mwezi Agosti, 2013 na;
Tatu, Wastani wa thamani ya Shilingi ya Tanzania mwezi septemba, 2013 ikilinganishwa na mwaka wa kizio, yaani septemba, 2010.
Ndugu waandishi wa habari, Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2013 umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.7 mwezi Agosti, 2013. Kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2013 kunamaanisha kuwa; kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Septemba, 2013 imepungua ikilinganishwa na kasi ya kupanda kwa bei kwa mwezi Agosti, 2013.
Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kwa mwezi Septemba kumechangiwa na kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Aidha, Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula majumbani na migahawani umepungua hadi asilimia 6.9 mwezi Septemba, 2013 ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwezi Agosti, 2013. Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, kasi ya ongezeko la bei imepungua hadi asilimia 6.0 kwa mwezi Septemba, 2013 kutoka asilimia 7.3 mwezi Agosti, 2013.
Ndugu waandishi wa habari, mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula hasa mchele umeonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa mwezi Septemba, 2013 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2012. Kwa wastani bei za mchele zimepungua kwa asilimia 17.2 kwa kipindi cha mwezi Septemba, 2012 na Septemba, 2013. Baadhi ya Mikoa ambayo imepata unafuu wa bei za mchele ni pamoja na Morogoro (asilimia 29.7), Singida (asilimia 26.7), Kagera (asilimia 25.0), Manyara (asilimia 16.7) na Dar es Salaam (asilimia 13.5).
Kwa upande wa bidhaa za mahindi, matokeo yanaonyesha kuwa bei za bidhaa hiyo zimepungua kwa baadhi ya mikoa kama; Arusha (asilimia 11.1), Pwani (asilimia 12.5), Rukwa (asilimia 5.0) na Mwanza (asilimia 18.9). Bidhaa nyingine za vyakula zilizoonyesha kupungua kwa bei kwa baadhi ya mikoa ni pamoja na mafuta ya kupikia ambapo mkoa wa Mtwara zimeshuka kwa asilimia (4.0), Kagera (asilimia 11.9) na Mwanza (asilimia 12.1). Bei za maharage mkoani Singida zimeshuka kwa asilimia 33.3, Dodoma (asilimia 6.3) na Arusha (asilimia 7.7).
Aidha, bidhaa zisizo za vyakula zilizosababisha kupungua kwa bei mwezi Septemba, 2013 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2012 ni pamoja na petroli na dizeli ambapo bei za petroli zimepungua kwa asilimia 4.0 na Dizeli kwa asilimia 2.2 katika kipindi hicho. Bidhaa nyingine ni pamoja na gesi kwa baadhi ya mikoa kama Ruvuma (asilimia 7.0), Rukwa (asilimia 7.0) na Kigoma (asilimia 8.3).
Ikumbukwe kwamba kupungua kwa Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kuna unafuu wa maisha kwa mlaji, kwa maana hiyo Tanzania inapiga hatua nzuri katika maendeleo ya kiuchumi.
MFUMUKO WA BEI KWA KIPIMO CHA MWEZI
Ndugu waandishi wa habari, kwa upande wa mfumko wa bei kwa kipimo cha mwezi, matokeo yanaonyesha kuwa, Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2013 umeongezeka kwa asilimia 0.5 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.1 mwezi Agosti, 2013. Kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa Kipimo cha Mwezi, kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi ni pamoja na; mahindi (asilimia 0.8), unga wa ngano (asilimia 2.2), samaki wabichi (asilimia 4.1), matunda (asilimia 4.5), karanga (asilimia 1.6), viazi mviringo (asilimia 0.9), unga wa muhogo (asilimia 5.2), sukari (asilimia 0.3), asali (asilimia 3.5) na vitafunwa (asilimia 1.1).
Bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi ni; vitambaa vya nguo (asilimia 0.2), mavazi ya kike (asilimia 0.3), viatu (asilimia 0.3), mafuta ya taa (asilimia 1.0), samani (asilimia 1.1), vifaa vya nyumbani vya malazi (asilimia 0.3), vifaa vya nyumbani vya usafi (asilimia 0.3), dizeli (asilimia 1.7) na petroli (asilimia 2.7).
THAMANI YA SHILINGI YA TANZANIA MWEZI SEPTEMBA, 2013 IKILINGANISHWA NA MWAKA WA KIZIO, YAANI SEPTEMBA, 2010
Ndugu waandishi wa habari, Wataalamu wa uchumi, takwimu na falsafa wanasema kwamba, uwezo wa fedha katika kununua bidhaa na huduma mbalimbali una uhusiano unaokinzana na mwelekeo wa Fahirisi za Bei. Hii ina maana kuwa, kama Fahirisi za Bei zikipungua, uwezo wa fedha katika kununua bidhaa na huduma unaongezeka.
Kwa maana hiyo, uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kipindi chote cha mwaka, yaani kutoka Januari, 2013 hadi Septemba, 2013. Hii ni kwa sababu fahirisi za bei za Taifa kwa kipindi chote hicho zimekuwa na mwelekeo ulio imara.
HALI YA MFUMUKO WA BEI KWA BAADHI YA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI
Ndugu waandishi wa habari, Kwa ujumla, Mfumuko wa Bei nchini una mwelekeo unaofanana na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Mfano; Mfumuko wa Bei nchini Kenya umeongezeka hadi asilimia 8.29 mwezi Septemba, 2013 kutoka asilimia 6.67 mwezi Agosti, 2013. Nchini Uganda Mfumuko wa Bei umeongezeka pia hadi asilimia 8.0 mwezi Septemba, 2013 kutoka asilimia 7.3 mwezi Agosti, 2013.
Ndugu waandishi wa habari, napenda kuwashukuru kwa mara nyingine tena kwa kuhudhuria mkutano huu, na natoa wito kwenu juu ya umuhimu wa kuwaelimisha Watunga Sera, Wafanyabiashara na Wananchi wote kwa ujumla kuhusu umuhimu wa matumizi ya takwimu hizi za bei na nyinginezo zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuendesha shughuli zao za kila siku.
Pia ninawaomba sana wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano wa dhati kwa Ofisi zetu za Takwimu za Mikoa wakati wa ukusanyaji wa takwimu mbali mbali kwa kutoa taarifa zilizo sahihi na kwa wakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Kwa hayo machache ninaomba niishie hapo na ninawakaribisha tena tarehe 08 mwezi Novemba, 2013 kwa ajilili ya kuwafahamisha Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2013.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Comments