Wednesday, October 30, 2013

DARAJA LA KIKWETE KATIKA MTO MALAGARASI MKOANI KIGOMA LAKAMILIKA


Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika mto Malagarasi mkoani Kigoma umekamilika. Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma aliweza kutembelea eneo hilo na kujionea magari yakiwa yanapita katika daraja hilo.

Kampuni ya M/S Hanil Engineering and Construction Company Limited kutoka Korea ya Kusini iliingia mkataba na kuanza ujenzi wa daraja hilo mwezi Desemba 2010 na kutakiwa kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Desemba 2013. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275 pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48 kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 64 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 90 za Kitanzania zilizotolewa na Benki ya Exim ya Korea ya Kusini kwa asilimia 90 na kiasi kilichobaki kikiwa ni fedha za ndani.

Akitoa maelezo ya mradi huo Mhandisi Yu Sing kutoka kampuni ya Hanil Engineering alimfahamisha Waziri Magufuli kuwa, Mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ambayo ndiyo iliyokamilika ni ujenzi wa madaraja matatu yenye urefu wa meta 25, meta 200 na meta 50 pamoja na kilometa 11 za lami. Sehemu ya pili ni ujenzi wa kilometa 37 za lami ambazo ndizo zinazoendelea kukamilishwa kwa sasa.

Sosi: matukio-michuzi: DARAJA LA KIKWETE KATIKA MTO MALAGARASI MKOANI KIGOMA LAKAMILIKA

No comments: