KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA CHAKULA DUNIANI, WFP INASEMA KUWEKEZA KATIKA LISHE NDIYO UFUNGUO KUELEKEA MSTAKABALI BORA ZAIDI
Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja la Mataifa (WFP) linaadhimisha Siku ya Chakula Duniani tarehe 16 Oktoba kwa kusisitiza umuhimu wa lishe katika kumbadilisha mtu mmoja mmoja, jamii na uchumi wa taifa, na umuhimu wa kuifanya lishe kama suala la msingi katika mipango yote ya maendeleo.
“Wasichana na wavulana wenye lishe duni wanapata changamoto za kiafya , hawawezi kufanya vizuri shuleni, na baadaye inakuwa vigumu kwao kufanya vizuri katika sehemu za kazi, na hii inadumaza uwezo wao wa kibinadamu na uwezo wa kuchangia kwenye jamii wanamoishi,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Ertharin Cousin.
“Kwa kutoa kipaumbele katika lishe leo tunawekeza kwa ajili ya mustakabali wetu wa jumla wa kimataifa wa baadaye. Uwekezaji ni lazima uhusishe chakula, kilimo, afya na mifumo ya elimu,” alisema.
Leo hii takribani watu milioni 842 - yaani zaidi ya mtu mmoja katika kila watu nane duniani - wanakabiliwa na njaa iliyokithiri. Zaidi ya hayo - takriban watu bilioni mbili – wanakosa vitamini na madini yanayohitajika kwa afya.
Kama jumuiya ya kimataifa ingewekeza dola bilioni 1.2 kwa mwaka kwa miaka mitano katika kupunguza upungufu wa viiini lishe, matunda yake yake katika afya bora, kupungua vifo vya watoto na kuongezeka kwa kipato, yangeleta faida ya dola bilioni 15.3.
Ukurasa wa 2 “Hapa Tanzania, kutatua tatizo la lishe duni ni sehemu muhimu ya shughuli za mpango wetu na shughuli zetu za kisera,” alisema Mkurugenzi Mkazi wa WFP Tanzania Richard Ragan.
“Tunawafikia watu milioni 1.2 walio kwenye hali tete kila mwaka, na kupitia mipango yetu ya lishe tunahakikisha akina mama, wajawazito, na watoto wanapata chakula bora na chenye lishe.
Kauli mbiu ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu ni “Mifumo Endelevu ya Chakula kwa Usalama wa Chakula na Lishe.” WFP inatoa msaada wa chakula kwa watu milioni 97 duniani kote. Hapa ni baadhi ya njia ambazo WFP inalenga kwenye lishe:
• Kuongeza idadi ya watoto na akina mama ambao wanapata vyakula vilivyoongezewa virutubishi;
• Kutilia mkazo lishe katika siku 1000 za muhimu – tangu ujauzito mpaka mtoto anapofikisha miaka miwili - ambapo mtoto anahitaji sana lishe kwa ukuaji mzuri;
• Kuongeza msaada kwa kutoa fedha taslimu na/au vocha kipindi ambapo chakula kinapatikana kwenye masoko, ili watumiaji waweze kununua vyakula vya aina mbalimbali vinavyopatikana kwenye maeneo yao;
• Kusisitiza ulaji wa vyakula anuai kutoka katika makundi muhimu kwenye mipango ya mlo shuleni, kwa kushirikiana na jamii;
• Kushirikiana na wadau binafsi na taasisi za utafiti kutathmini faida zinazotokana na mchele ulioongezewa virutubishi kwenye mlo wa shule;
• Kusaidia kujenga hoja kupitia tafiti ambazo zitaongoza nchi mbalimbali kwenye sera na mikakati ya lishe, kama vile ile ya karibuni inayojulikana kama “Utafiti wa Gharama ya Njaa Afrika” (Cost of Hunger in Africa survey).
“Nchini Tanzania, WFP inafanya kazi na serikali kusukuma mbele ajenda ya lishe. Mwezi Mei mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilizindua mpango wa kitaifa wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula vikuu ambavyo ni unga wa ngano, mafuta ya kupikia, na unga wa mahindi,” alisema Richard Ragan. “Kufuatia ukweli kwamba vyakula hivi vitazifikia kaya nyingi nchini kote, WFP inajisikia fahari kubwa kutoa msaada wa kitaalamu kuhakikisha wasagishaji wakati na wadogo wako tayari kuanza zoezi la kuboresha vyakula hivi mwaka ujao.”
WFP inasherehekea Siku ya Chakula Duniani pamoja na mashirika dada ya chakula ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Kwa picha na video tembelea tovuti ifuatayo:
Kwa taarifa zaidi kuhusu kazi ya lishe ya WFP nchini Tanzania, tembelea tovuti:
Comments