UFAFANUZI KWA NJIA YA MAANDISHI KUTOKA KWA NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO, MH. AMOS MAKALLA JUU YA UAMUZI WAKE WA KULIRUHUSU GAZETI LA MWANACHI KUENDELEA NA UTOAJI WA TAARIFA NA HABARI KWENYE TOVUTI YAKE PIA GAZETI LA RAI KUTOKA KILA SIKU
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, VIJANA,UTAMADUNI NA MICHEZO
Napenda kuufahamisha umma kwamba mimi ndiye NILIYERUHUSU Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake, pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.
Ninalazimika kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi kutokana na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari kuhusiana na tamko jipya la Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Ndg Assah Mwambene kuhoji uhalali wa Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara moja kwa wiki (Alhamisi).
Tarehe 4/10/2013 nilifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006) Ltd kwa upande mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.
Katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania maombi matatu yaliwasilishwa;
1. Ombi la kumuomba waziri apitie upya adhabu iliyotolewa kwa mageazeti hayo. Katika hili Majibu yangu niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee.
2. Ombi la Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamis.
2.1 New Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi kuomba kwa maandishi (barua) kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya Naibu Msajili wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna kinachozuia gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.
2.2 Kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu Msajili alisema hakuna sheria yeyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa online ila aliwataka lisionekane gazeti zima kama lilivyo pia wabadili nembo (Master Head) kwamba waweke nembo ya MCL na siyo ya gazeti husika ambalo limefungiwa. Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa Magazeti.
3. Hoja ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara ya Habari - Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka misuguano isiyo ya lazima.
3.1 Pendekezo hili nililipokea na niliwasilisha kwa Mhe Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na ushauri wa kujenga uhisiano na vyombo vya habari.
3.2 Masuala ya Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai kutoka kila siku, NILILITOLEA UAMUZI siku hiyo hiyo, na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na waombaji.
Nimeamua kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa uipande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu waziri na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.
Hivyo aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai ni mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti.
Imetolewa na:
Amos G. Makalla
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
11 Oktoba 2013
Comments