Waziri Membe Akutana na Waandishi wa Habari asema Hakuna Kiongozi wa Afrika Kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC)


  Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiongea na waandishi wa habari mapema jana kwenye ukumbi wa mkutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.
 Mhe. Waziri Membe akifafanua ombi la Kenya kuhusu uhalali wa kuwafikisha Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa (ICC) kujibu Makosa ya Jinai. Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha na kushoto ni Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 Wakurugenzi wakisikiliza kwa makini maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani).  Kulia ni Bw. Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, na Bw. Ligaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango.
 Kwenye Mkutano pia alikuwepo Bw. Kaaya (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa 
 Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ukijumuisha Balozi Irene Kasyanju (kushoto), Mkurugenzi wa Kikengo cha Sheria, Balozi Simba Yahya (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Mbelwa Kairuki (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia na Balozi Dora Msechu (wa nne kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika.
 Wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Bw. Mkubwa Ally (kushoto), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Thobias Makoba (katikati) na Bw. Togolani Mavura (kulia), Wasaidizi wa Mhe. Waziri Membe.
 Mmoja wa waandishi kutoka gazeti la The Citizen, Bw. Mkinga Mkinga akiuliza swali kwa Mhe. Waziri Membe. 
Waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Mhe. Waziri Membe akihojiwa na Bw. Erick David Nampesya, Mwandishi/Mtangazaji wa Shirika la Habari la BBC.Picha Zote na Tagie Daisy Mwakawago-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
---
Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb), akutana na waandishi wa habari  jana kujadili uhalali wa kuwafikisha Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa kujibu Makosa ya Jinai. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam.

Waziri Membe alikuwa akielezea yaliyojiri kwenye Kikao cha dharura cha Viongozi Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (UA) kilichomalizika mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia jana tarehe 12 Oktoba, 2013.  Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mfalme Mswati wa III, Rais wa Swaziland, na Viongozi Wakuu na Watendaji Wakuu wa Serikali barani Afrika.

Kikao hicho kiliitishwa kutokana na ombi la Serikali ya Jamhuri ya Kenya ya kutaka UA kujadili mahusiano yaliyopo kati ya nchi za Afrika na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) na iwapo ni sahihi kwa Viongozi Wakuu wa Nchi za Afrika kufikishwa katika Mahakama hiyo kujibu mashtaka wakati wakiwa madarakani.

“Viongozi hao wa Afrika waliazimia mambo makuu matano,” alieleza Waziri Membe, huku akiyataja mawili kuwa hakuna Kiongozi yoyote kutoka barani Afrika atakayepelekwa ICC au Mahakama yoyote kujibu mashtaka wakati akiwa madarakani hata akiwa anashika nafasi ya kukaimu. 

Mengine ni kuwa mashtaka yanayomkabili Kiongozi yoyote barani Afrika yasubiri hadi Kiongozi huyo atakapomaliza muda wa uongozi wake.  Aidha, Mhe. Waziri alieleza kusikitishwa kwa Viongozi wa Afrika na namna Mahakama ya ICC inavyoendesha shughuli zake kwa kile walichokiita “kuwaandama Viongozi wa Bara la Afrika kuliko Viongozi wa Mataifa mengine hata pale panapokuwa na ushahidi wa Viongozi hao wengine kufanya makosa ya Jinai.”

Waziri Membe alihoji inakuwaje kwamba kati ya kesi 30 zilizopelekwa ICC tangu mwaka 2004, ishirini na saba (27) zinatoka barani Afrika.  “Haya yote yalijadiliwa kwa kina, pamoja na pendekezo la kujitoa kwenye uanachama wa Mahakama ya ICC,” aliongeza Waziri Membe.

Alisema suala la kujitoa uanachama wa ICC limeachiwa kila nchi kuamua, ingawaje linategemewa kujadiliwa tena katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wa Sheria wa nchi wanachama wa mahakama hiyo kitakachofanyika tarehe 29 Novemba mwaka huu nchini Uholanzi. Hivi sasa kuna nchi thelathini na nne (34) barani Afrika ambazo ni wananchama wa Mahakama hiyo.

Akiendelea kuzungumza katika Mkutano wake wa leo na waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Membe amesema kuwa Umoja wa Afrika umepeleka ombi lake rasmi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuahirisha kesi inayowakabili viongozi hao wa Kenya.

Wakati huo huo, Mhe. Waziri Membe alitumia fursa ya mkutano wake na waandishi wa habari kutoa salamu za pole kwa Bibi Ufoo Saro, Mwandishi/Mtangazaji wa kituo cha televisheni ITV, na familia yake, kufuatia  taarifa iliyomfikia kuwa Bibi Saro amelazwa hospitali akiwa mahututi baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Mama yake mzazi, Anastazia Saro na mtoto wake waliuwawa katika shambulio hilo.  Taarifa zinasema mtuhumiwa ni   mchumba wa Bibi Saro, ambaye anadaiwa kufyatua risasi kwa familia hiyo na hatimaye kujipiga risasi na kufa.

Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Waziri Membe pia aliwatakiwa wananchi sikukuu njema ya Kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo itaadhimishwa Kitaifa kesho tarehe 14 Novemba 2013.

Comments