OCT21JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Maswali mengi yanaulizwa kuhusu uraia, hasa wakati huu ambapo zoezi la kuwabaini wageni wanaoishi nchini kinyume cha sheria linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, yakitaka kujua nani hasa ni raia wa Tanzania.
Kimsingi, masuala ya uraia duniani kote yanaongozwa na falsafa kuu mbili ambazo ni Haki za Kidamu (Jus Sanguinis - The rights of blood), ambapo mtu hupata uraia kutokana na uhusiano wa kidamu na wazazi wenye uraia wa nchi husika. Hii ina maana kwamba, pamoja na mtu kuzaliwa katika nchi husika anatakiwa pia kuwa na mzazi ambaye ni raia wa nchi hiyo. Falsafa hii ndiyo inayofuatwa na nchi ya Tanzania.
Kwa maana nyingine kuzaliwa pekee nchini Tanzania hakumpi mtu haki ya moja kwa moja ya kuwa raia wa Tanzania, bali mtu atakuwa raia ikiwa amezaliwa Tanzania na wakati wa kuzaliwa kwake mzazi wake mmoja sharti awe ni raia wa Tanzania.
Falsafa nyingine ni (Jus Soli - The right of Soil), ambayo mtu hupata Uraia kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi ya nchi fulani. Kufuatana na Falsafa hii, mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa katika nchi husika bila kujali uraia wa wazazi wake.
URAIA WA TANZANIA
Masuala ya uraia nchini Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka 1995 Sura 357 kama ilivyorejewa mwaka 2002, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997. Sheria hii imeanisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni;
1. Uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa
2. Uraia wa Tanzania kwa kurithi
3. Uraia wa Tanzania kwa Tajnisi, au kujiandikisha.
Uraia wa Tanzania wa kuzaliwa:
Utambuzi wa nani ni raia wa Tanzania unazingatia vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania, yaani kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika, kabla na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na baada ya Muungano wa Tanzania. Pia, mahali alipozaliwa na alizaliwa na nani kama inavyoainishwa hapa chini:
Aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru
Mtu aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alizaliwa Tanganyika na anatokana na Raia wa Uingereza,makoloni yake au nchi zilizokuwa chini ya udhamini wa Uingereza
Aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru
Mtu aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alikuwa raia wa Tanganyika.
Aliyezaliwa Zanzibar kabla na Baada ya Mapinduzi
Mtu aliyezaliwa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi alitambulika kuwa ni raia wa Zanzibar wa kuzaliwa.
Ila, mtu huyo hakutambulika kuwa ni raia wa zanzibar ikiwa wazazi wake walitokana na mataifa yafuatayo; Australia, Ubeligiji, Kanada, Ceylon (Sri Lanka), Ufaransa, Italia, New Zealand, Ureno, Jamhuri ya Ireland, Afrika Kusini na Marekani.
Aliyezaliwa Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania
Mtu aliyezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano, atatambulika kuwa ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa ikiwa mmoja wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.
Mtu hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kama wakati wa kuzaliwa kwake hapa nchini, wazazi wake wote hawakuwa raia wa Tanzania; au Baba yake ni Balozi wa nchi ya kigeni na ana kinga ya kibalozi; au mmoja wa mzazi wake alikuwa ni adui wa nchi ya Tanzania (enemy) na mtoto huyo alizaliwa katika eneo lililokuwa likikaliwa na adui.
Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) ndiyo sheria pekee inayotambua sheria zote za nyuma, zilizokuwa zinasimamia masuala yote ya uraia katika vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania.
Kwa mantiki hiyo mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kuzaliwa, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964, ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa, mara baada Muungano.
Aidha, mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa ni raia wa Tanzania mara baada ya muungano.
URAIA WA TANZANIA KWA KURITHI:
Raia wa Tanzania kwa kurithi ni mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania, na anatambuliwa kuwa raia wa Tanzania kutegemeana na kipindi alichozaliwa na uraia wa wazazi wake wakati wa kuzaliwa kwake kama ifuatavyo:
Aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya Uhuru
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya uhuru (akiwa ametokana na raia wa Uingereza na Makoloni yake au himaya ya Mwingereza) alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi endapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi, ikiwa baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Sheria ya Uraia ya Tanganyika ya mwaka 1961 haikutoa fursa kwa mama kumrithisha uraia mtoto wake aliyezaliwa nje ya nchi. Hivyo mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika katika vipindi tajwa hapo juu hakutambulika kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi kupitia mama yake.
Aidha, mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika hakutambuliwa kuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi iwapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Raia wa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanganyika.
Aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano wa Tanzania
Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano atakuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi endapo baba yake ni raia wa Zanzibar.
Vile vile, Sheria ya Uraia ya Zanzibar (The Zanzibar Nationality Decree, CAP 39, 1952)haikuruhusu mama raia wa Zanzibar kurithisha uraia kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar. Kwa maana nyingine, mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar katika kipindi hicho hakutambuliwa kuwa ni raia wa Zanzibar kwa kurithi kupitia kwa mama yake.
Ieleweke pia kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar hakutambuliwa kuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi ikiwa Baba yake alikuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Raia wa Zanzibar kwa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar.
Aliyezaliwa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania siku na baada ya Muungano atakuwa raia wa Tanzania kwa kurithi endapo mzazi wake mmoja ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa au kuandikishwa/tajnisi.
Ni vyema ieleweke kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi iwapo baba/mama yake ni raia wa Tanzania kwa kurithi.
Sheria ya Uraia Sura ya 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) imetoa fursa kwa mama ambaye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, tajnisi/kuandikishwa kurithisha uraia wa Tanzania kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanzania.
Aidha, mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964 ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ile ile mara baada Muungano.
Mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi mara baada ya muungano.
Haya yameainishwa katika Sheria ya Uraia ya Tanzania Na.6, 1995 (Sura 357, Rejeo la 2002) kifungu cha 30.
URAIA WA TANZANIA KWA TAJNISI (NATURALIZATION)
Mtu yoyote ambae siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa au kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa tajnisi kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura 357 ya mwaka 1995, (R.E,2002).
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kumpa au kutompa uraia wa Tanzania Mgeni mwenye sifa anayeomba uraia.
Sifa za Kuomba Uraia wa Tajnisi;
Mgeni anaetaka kuomba uraia wa Tanzania anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:
(i) Mwombaji awe na umri kuanzia miaka 18 na uwezo wa kufanya maamuzi yanayokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi,
(ii) Awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miezi 12 mfululizo kabda ya kutuma maombi ya Uraia,
(iii) Katika muda wa miaka kumi kabla ya miezi kumi na mbili hiyo awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali kwa muda usiopungua miaka saba.
(iv) Awe anafahamu vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza,
(v) Awe na tabia njema,
(vi) Awe na manufaa kwa taifa, yaani awe alichangia na anaendelea kuchangia katika ukuzaji wa uchumi, sayansi na teknolojia na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
(vii) Awe anakusudia kuishi moja kwa moja ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa.
Taratibu za kuomba uraia wa Tajnisi.
Mgeni yeyote mwenye nia ya kuomba uraia wa tajnisi mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo;
(i) Mwombaji anatakiwa kujaza fomu za maombi ya uraia ambazo zinapatikana katika ofisi zote za Uhamiaji za Wilaya, Mikoa, Afisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar na Makao Makuu ya Uhamiaji Dar es Salaam.
(ii) Mwombaji anatakiwa kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba Uraia wa Tanzania mara mbili mfululizo kwenye magazeti yaliyosajiliwa Tanzania.
Mchakato wa Kushughulikia Maombi ya Uraia
Ili kuhakikisha kuwa wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa kwa Taifa, maombi yote yanapaswa kupitia na kujadiliwa katika vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama za:
Ngazi ya Kata au Shehia (kwa upande wa Zanzibar)
Katika ngazi ya Kata au Shehia anayoishi mwombaji, ambapo atahojiwa na maombi yake kujadiliwa na kikao hicho na hatimaye ombi lake kupelekwa ofisi ya Uhamiaji Wilaya kwa hatua zaidi.
Ngazi ya Wilaya
Katika ngazi hii, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itajadili maombi ya uraia yaliyowasilishwa kutoka ngazi ya Kata au Shehia, hatimaye maoni na mapendekezo yake hupelekwa katika ngazi ya mkoa.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nayo itajadili maombi yaliyowasilishwa na kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na ombi husika na hatimaye hutumwa kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ambaye atatoa ushauri na mapendekezo yake kwa Mhe. Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia wa Tanzania kwa maamuzi.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mwanamke aliyeolewa.
Mwanamke mgeni ambaye ameolewa na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wowote wa uhai wa ndoa yake, anaweza kuwasilisha maombi ya uraia wa Tanzania kwa tajnisi.
Ombi la uraia kwa mwanamke aliyeolewa linatakiwa kuwasilishwa pamoja na viambatanisho vifuatavyo;
(i)Cheti cha ndoa kilichosajiliwa na Mamlaka husika nchini
(ii) Pasipoti ya taifa lake ambayo haijaisha muda wake
(iii) Kibali cha kuishi nchini ambacho hakijaisha muda wake (Hati ya Mfuasi)
(iv) Vielelezo vinavyothibitisha kuwa mume wake ni raia wa Tanzania.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mtoto
Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357 (RE 2002), inatoa fursa kwa mzazi au mlezi halali wa mtoto (asiye raia) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumuombea mtoto huyo Uraia wa Tanzania. Baada ya maombi rasmi kuwasilishwa, Waziri mwenye dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto huyo aweze kupata uraia wa tajnisi.
Waziri mwenye dhamana na masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani) ndiye mwenye Mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa Tanzania kwa mwombaji yoyote kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357, rejeo la 2002.
Makala hii imeandaliwa na Timu ya Habari ya Operesheni Kimbunga -
Oktoba, 2013
Comments