Friday, July 22, 2016

WASIFU WA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI


MGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI WA CCM

1.0.  MAISHA YAKE

Ndugu John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 katika kijiji cha Chato, Wilayani Biharamulo katika Mkoa wa Kagera. Hivi sasa Chato ni Wilaya katika Mkoa wa Geita. Ndugu Magufuli ni Daktari wa Falsafa (PhD) ya Kemia. Ana mke  na watoto saba.  Alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba, 2015 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (C.C.M). Aliapishwa na kuanza rasmi majukumu yake ya kuiongoza Tanzania tarehe 5 Novemba, 2015.

Tangu ameingia madarakani, Rais Dkt. Magufuli, ameonesha kuwa ana sifa zote muhimu za uongozi. Ana dira, maono na malengo kuhusu anakotaka Taifa liende. Ana mikakati ya kutekeleza dira na maono yake. Haogopi kufanya maamuzi makini. Ana kiu ya kuona Taifa linapata maendeleo. Amejipambanua kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge na dhamira yake kubwa ni kuona wananchi wanapata huduma bora  za jamii na kero zao zinaondoka.

2.0.  ELIMU NA MAFUNZO

Rais Dkt. Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya msingi Chato mwaka 1967 na kumaliza mwaka 1974. Mwaka 1975 alianza masomo ya sekondari katika Shule ya Seminari ya Katoke Mkoani Kagera.  Mwaka 1977 alihamia shule ya sekondari ya Lake iliyopo Mkoani Mwanza  na kuhitimu kidato cha Nne mwaka 1978. Kuanzia mwaka 1979 hadi 1981 alifanya masomo ya kidato cha Tano na  Sita katika shule ya Sekondari ya Mkwawa Mkoa wa Iringa  .

Mwaka 1981 hadi 1982 alisoma Chuo cha Ualimu Mkwawa na kuhitimu Stashahada ya Ualimu ya Masomo ya Kemia na Hisabati.  Mwezi Julai hadi Disemba mwaka 1983, Dkt. Magufuli alipata mafunzo ya kijeshi  katika Jeshi la  kujenga Taifa kikosi cha Makutupora mkoa wa Dodoma. Mwezi Januari hadi Machi 1984 alihamishiwa kikosi cha mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa Makuyuni, Arusha.  Mwezi huo wa Machi alihamia kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Mpwapwa Dodoma na kumaliza mafunzo mwezi Juni 1984.

Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusoma Shahada ya kwanza ya Sayansi na Ualimu akijikita katika masomo ya Kemia na Hisabati. Alitunukiwa Shahada hiyo mwaka 1988.  Mwaka 1991 hadi 1994 alisoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani ya Kemia iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo Kikuu cha Salford cha Uingereza. Mwaka 2006 alijiunga na  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya Shahada ya Uzamivu katika Fani ya Kemia na kufanikiwa kuhitimu mwaka 2009.

3.0.  UZOEFU WA NDANI YA  SERIKALI

Baada ya kuhitimu masomo yake ya Stashahada ya Ualimu, mwaka 1982 hadi 1983 Dkt. Magufuli alikuwa Mwalimu katika shule ya Sekondari ya Sengerema iliyopo Mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati.  Mwaka 1989 alijiunga na Chama Cha Ushirika cha Nyanza Mkoani Mwanza, ambapo alifanya kazi kama Mkemia Mkuu  hadi mwaka  1995.

Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki Mkoa wa Kagera.  Baada ya Uchaguzi, Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi nafasi ambayo aliitumikia  hadi mwaka 2000.  Mwaka 2000 alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki lakini mara hii akipita bila kupingwa.  Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Waziri kamili wa Wizara ya Ujenzi hadi mwaka 2005. 

Mwaka 2005 Rais Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya tatu kuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki, kwa mara nyingine akipita bila kupingwa.   Baada ya uchaguzi, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 ambapo alihamishiwa Wizara ya   Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi hadi hadi mwaka 2010.

Mwaka 2010 Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya nne  kuwa  Mbunge lakini, kufuatia mgawanyo wa majimbo uliofanyika, mara hii katika Jimbo jipya la Chato.  Baada ya uchaguzi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Wakati akiwa Mbunge na Waziri, Dkt. Magufuli amefanya shughuli na kushika nyadhifa kadhaa ndani na nje ya nchi. Mwaka 2014, Dkt. Magufuli alishiriki katika Bunge Maalum la Kutunga Katiba Mpya akiwa  ni Mjumbe wa Bunge hilo. Aidha, wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza (Co-Chair) wa Mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat).

Tarehe 25 Oktoba, 2015 Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tarehe 5 Novemba, 2015 aliapishwa kushika rasmi wadhifa huo.

No comments: