Wednesday, July 06, 2016

ALAT YAIPONGEZA JUMUIYA YA WAANDISHI WA HABARI MKOANI SHINYANGA

 
Mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam akikabidhi mchango/msaada wa shilingi 300,000/- kwa mwenyekiti wa SPC bwana Kadama Malunde kwa ajili ya maendeleo ya ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga 
Kushoto ni mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania,ambaye ni mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam akiwa katika ofisi ya klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club -SPC) zilizopo mjini Shinyanga alipotembelea ofisi hiyo jana.Kulia ni mwenyekiti wa SPC bwana Kadama Malunde-picha kwa hisani ya SPC .

JUMUIYA ya serikali za mitaa nchini (ALAT) imepongeza kazi wanayoifanya waandishi wa Habari mkoani Shinyanga kwa kuuhabarisha umma kuhusu shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na serikali na kuibua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii. Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ambaye pia ni Mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gullam Hafeez Mukadam ametoa pongezi hizo jana alipotembelea ofisi za Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC). 
 
Mukakadam alisema maendeleo yanayoonekana mkoani humo yametokana na mchango wao mkubwa wa kuandika,kuchapisha na kutangaza habari zinazotokea katika jamii. Alisema kazi inayofanywa na waandishi wa habari mkoani humo haiwezi kubezwa na mpenda maendeleo yoyote kwa kuwa matunda yake yanaonekana huku akitolea mfano uharakishwaji wa ujenzi wa barabara za lami katikati ya manispaa ya Shinyanga. 
 
“Ndugu zangu mimi nawapongeza sana kwa juhudi mlizo nazo za kuuhabarisha umma wa Watanzania juu ya shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikali yao lakini pia kwa kutoficha uovu unaofanywa na watu wachache ndani ya serikali na jamii kwa ujumla” ,alisema Mukadam. “Mmeibua mengi kwa faida ya taifa lenu na wananchi wake, ikiwemo ubadhirifu wa mali za umma, wizi wa fedha kwenye halmashauri zetu, matumizi mabaya ya madaraka na ofisi za umma”,aliongeza. 
Katika hatua nyingine aliupongeza uongozi wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kwa kuimarisha mshikamano miongoni mwa waandishi wa habari na wadau wa habari.
 
 Akiwa katika ofisi hizo za waandishi wa habari Mukadam alitoa msaada wa shilingi 300,000/= kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa ofisi hiyo na kusisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na waandishi wa habari huku akiahidi kutoa viti vya kisasa kwa ajili ya ofisi hiyo. Kwa upande wake mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga Kadama Malunde alishukuru kwa msaada uliotolewa na mstahiki meya na kuwataka wadau wengine kujitokeza kuisaidia SPC kwa ajili ya maendeleo ya waandishi wa habari.
 
Malunde alisema waandishi wa habari mkoani Shinyanga watatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mheshimiwa Rais Magufuli ya Hapa Kazi tu kwa kuhakikisha kuwa wanaandika mazuri na mabaya yote yanayofanyika katika jamii. 
 
“Nawapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri wanayofanya tena kwa kujitolea zaidi kwa hali na mali japo kuna vikwazo vingi wanavyokutana navyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo baadhi ya halmashauri kuwaona kama maadui hasa pale wanapofuatilia vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma na uwajibikaji mbovu wa viongozi”,alieleza Malunde. 

Post a Comment