Monday, July 18, 2016

VIJANA 559 WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU,WAHITIMU VETA

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Jumla ya vijana 559 waishio katika mazingira magumu wamehitimu elimu ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) chini ya mradi unaosimamiwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International.

Takwimu hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Jorgen Haldorsen wakati wa mahafali ya kwanza ya vijana hao yaliyofanyika katika Chuo cha VETA, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa na linahitaji jitihada za pamoja katika kulikabili hivyo, kwa Mkoa wa Dar es Salaam, mradi huo unalenga kufikia vijana 2110 ndani ya miaka mitatu kutoka Wilaya za Ilala na Temeke.

“Mahafali ya leo ni mahsusi kwa ajili ya vijana wanaoishi katika mazingira magumu, wamesoma fani mbalimbali za ufundi zikiwemo za umeme wa majumbani, ushonaji, udereva, ufundi magari, uchomaji vyuma, mapishi na mapambo ambapo zaidi ya ufundi stadi vijana wetu wamejengewa utamaduni wa kujiwekea akiba kupitia vikundi vya hisa”, alisema Haldorsen.

Haldorsen amefafanua kuwa uteuzi wa vijana wanaojiunga na mradi huu unafanywa na Viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na vijana wanaoishi katika mazingira magumu kwa kufata vigezo ambavyo ni; vijana wenye ulemavu, wasichana waliopata watoto katika umri mdogo,vijana yatima au wanaolelewa na mzazi mmoja, vijana wanaofanya kazi na kuishi katika mazingira hatarishi pamoja na vijana ambao hawakumaliza shule kutokana na changamoto mbalimbali.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Leah Lukindo ameushkuru Umoja wa Ulaya pamoja na waandaaji na watekelezaji wa mradi huu wakiwemo Wizara ya Vijana na Ajira, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Shirika la Plan International, Shirika la Volunteer Service Oversees (VSO),CCBRT, UHIKI, CODERT pamoja na uongozi wa Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha mradi huu unaogusa hitaji kubwa la kitaifa la ajira kwa vijana unafanikiwa.

Wakiwasilisha ujumbe kwa njia ya risala,vijana waliohitimu mafunzo hayo wamesema kuwa wamepata msaada na ushauri ambao umewajengea ujasiri wa kuweza kujiajiri wenyewe na hata kuajiriwa kutokana na fursa zilizopo na zitakazojitokeza.

Mradi huu unatekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara kwa kipindi cha miaka mitatu, mradi huo unagharimu kiasi cha Euro 3,874,984.53 na unafadhiliwa na Umoja wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya.
Post a Comment