Wednesday, August 19, 2026

RC CHALAMILA ATOA SIKU SABA KWA MUAFAKA WA MGOGORO WA ARDHI TOANGOMA





Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa muda wa siku saba kwa wadau wanaohusika na mgogoro wa muda mrefu wa ardhi katika eneo la Toangoma, Wilaya ya Temeke, kukutana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kutafuta muafaka kabla ya kurejea katika eneo hilo kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro huo.

Mhe. Chalamila ametoa maelekezo hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Toangoma, baada ya kusikiliza maelezo ya wananchi, NSSF pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi. Amesema kwa mujibu wa nyaraka na maelezo yaliyowasilishwa, amejiridhisha kuwa eneo linalozungumziwa linamilikiwa na NSSF.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema amepokea maombi ya wananchi wanaotaka masharti ya ununuzi wa maeneo wanayoishi yafanyiwe mapitio ili kuwawezesha kumudu gharama na kupata muda wa kutosha wa kufanya malipo.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano huo, NSSF ilikuwa imeweka bei ya Sh. 15,000 kwa mita ya mraba katika eneo la Malela na Sh. 25,000 kwa mita ya mraba katika eneo la Mwapemba. Wananchi wameomba bei hiyo ipunguzwe hadi Sh. 5,000 kwa mita ya mraba, sambamba na kuongezewa muda wa kufanya malipo kutoka kipindi cha awali cha miezi mitatu hadi kati ya miaka minne na 10.

Mhe. Chalamila amesema katika kipindi cha siku saba alichotoa, atakutana na wadau husika kwa lengo la kutafuta suluhu inayozingatia maslahi ya pande zote. Aidha, ameelekeza wananchi kutosumbuliwa katika kipindi hicho huku muda wa awali uliokuwa umetolewa kwa ajili ya malipo ukisitishwa ili kutoa nafasi ya kufikiwa kwa mpango mpya.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema Mwinuka, amethibitisha kuwa eneo hilo linamilikiwa na NSSF. Kwa upande wake, mwakilishi wa NSSF ameeleza kuwa baada ya kubaini kuwapo kwa wananchi katika eneo lake, Shirika liliamua kutoa fursa kwa wakazi hao kununua maeneo wanayoishi kwa bei zilizowekwa.

Awali, wananchi walieleza kuwa wengi wao wameishi katika maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 16, wakidai kuwa walinunua viwanja kupitia taratibu zilizohusisha viongozi wa serikali za mitaa na hivyo kuamini kuwa ardhi hiyo haikuwa mali ya NSSF.

Kutokana na mazingira hayo, wananchi wamemuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kupatikana kwa suluhu itakayowawezesha kuendelea kumiliki maeneo hayo kwa gharama na masharti wanayoweza kumudu.

Mhe. Chalamila anatarajiwa kurejea Toangoma baada ya siku saba kwa ajili ya kutoa mrejesho wa majadiliano na kuweka hitimisho katika mgogoro huo wa muda mrefu.

No comments:

RC CHALAMILA ATOA SIKU SABA KWA MUAFAKA WA MGOGORO WA ARDHI TOANGOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa muda wa siku saba kwa wadau wanaohusika na mgogoro wa muda mrefu wa ardhi katik...