Friday, July 22, 2016

SERIKALI KUPIMA VIWANJA ZAIDI YA 25,000 JIJINI DAR ES SALAAM

TZNa Jonas Kamaleki, MAELEZO
…………………………………
SERIKALI iko mbioni kutoa hatimiliki zaidi ya 25,000 kwa wakazi wa kata za Kimara na Saranga zilizopo jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kurasimisha makazi holela.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Mradi wa urasimishaji wa makazi holela Kata za Kimara na Saranga, Bi Grace Masatu wakati wa zoezi la ukaguzi wa maeneo ya mradi.
“Zoezi za la upimaji linaenda sanjari na utambuzi wa mipaka,ujazaji wa madodoso, uchoraji wa ramani za upimaji na mipangomiji,”alisema Masatu.
Viwanja zaidi ya 25,000 vinatarajiwa kupimwa katika kata za Kimara na Saranga ambapo hadi leo ramani za upimaji 14 na ramani sita (6) za mipangomiji zenye jumla ya viwanja1028 ziko tayari na zimeshawasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajli ya kupitishwa, alisema Masatu.
Aidha, Masatu amesema kuwa malengo ya mradi huo ni kuongeza thamani ya makazi kwa kutoa hatimiliki na kutambua mipaka ya wakazi wa maeneo husika.
Kwa upande wake, Afisa Mipango miji Mkuu, Bi Anna Macha, alisema kuwa hadi sasa maeneo yaliyopimwa katika kata ya Kimara ni mtaa wa Kilungule A wote pamoja na viwanja 724 vya mtaa wa Kilungule B, ambavyo vimechukuliwa mahesabu ya upimaji kwa ajili kuandaa ramani.
Ameongeza kuwa umetengenezwa mfumo maalum ambao unachukua taarifa za madodoso zinazojazwa wakati wa utambuzi wa mipaka ya wamiliki wa maeneo husika. Mfumo huo utaunganishwa na mfumo wa Kamishna wa Ardhi (MOLIS) utakaorahisisha kufahamu idadi ya viwanja vilivyopimwa na kumilikishwa.
Naye Mjumbe wa Mtaa wa Kilungule B,  Bwana Claud Misri Silayo ameonyesha kuridhishwa na zoezi zima la utambuzi na upimaji wa maeneo.
“ Nimefurahishwa na zoezi la upimaji kwani nitamiliki ardhi kisheria, kihalali na nitafaidika na ardhi ninayomiliki kwa sababu mwisho wa zoezi hili nitapata hatimiliki ambayo itaniwezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha,”alisema Silayo.
Urasimishaji ni mwendelezo wa utambuzi wa makazi holela katika jiji la Dar es Salaam unaotekelezwa chini ya Sheria ya Ardhi Na. 4 pamoja na Sheria ya Mipangomiji.

No comments: