Tuesday, March 15, 2016

KAMISHNA WA JESHI LA POLISI ZANZIBAR AZUNGUMZIA JUU YA MIRIPUKO INAYOTOKEA UNGUJA NA PEMBA


Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu matokeo ya uripuaji wa mabomu na kuchoma moto nyumba na maskani za CCM Unguja na Pemba. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame leo Zanzibar.

Na Mwashungi Tahir na miza Kona - Maelezo Zanzibar      15/03/2016
NYUMBA ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame imeripuliwa  na kitu kinachosadikiwa kuwa  ni bomu na watu wasiojulikana  majira ya saa 5.00 usiku huko Kijichi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Ofisini kwake Makao Makuu ya Polisi Kilimani, Kamishna Hamdani amesema tukio hilo limeathiri sehemu ya paa la nyumba na dari na  kujeruhi baadhi ya watu  waliokuwa wamelala  na kusababisha hasara kubwa.

Amesema tukio hilo linafanana lile lililotokea tarehe 03 mwezi huu katika Maskani ya CCM Kisonge Unguja hivyo polisi inaendelea kufanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wanaofanya  uhalifu huo.

Akizungumzia  matukio  mengine ya uhalifu na kuchoma moto nyumba, maskani na kituo cha Afya huko Pemba, alisema  Jeshi la Polisi limeanza msako mkali na kuwatia mbaroni watu 31 ambao wanaendelea kuhojiwa na watakaohusika watafikishwa  katika vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani amewatowa hofu  wananchi kuhusu usalama wao na mali zao kuelekea uchaguzi wa marudio utakaofanyika tarehe 20 mwezi huu na kuwepo kwa ongezeko la askari katika maeneo  mengi ya mijini na vijijini  ni  moja ya juhudi za kuimarisha  ulinzi  na kuhakikisha  uchaguzi huo utakuwa salama na amani.

Ametahadharisha kuwa mtu yoyote atakayejihusisha kuanziasha vurugu au kufanya kitendo chenye ishara ya  uvunjifu wa amani atapambambana na vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani ametowa wito kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba bila ya woga  kwani jeshi hilo limejipanga  kuimarisha ulinzi  sehemu sehemu zote.

No comments: