Thursday, March 31, 2016

BARABARA YA KIGOMA-NYAKANAZI KUKAMILIKA MWEZI MEI.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kigoma tayari kuanza ziara ya ukaguzi wa miundombinu katika mikoa ya ukanda wa magharibi.
2Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) kuhusu ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na China Railway 50 Group.
3Ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na Kampuni ya  China Railway 50 Group ukiendelea.
4Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) akitoa maelekezo kwa wataalamu wa ujenzi wa kampuni ya China Railway 50 Group baada ya kukagua mitambo yao ya kupima na kutafiti udongo kabla ya kujenga barabara.
5Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya ya Kasulu mara baaada ya kukamatwa kwa vijana wawili (waliokaa chini) kutokana na wizi wa nyaya za mkongo wa taifa, mkoani Kigoma.
6Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa koti la kaki) akiangalia athari za mmonyoko wa udongo zilizoathiri mkongo wa taifa wa mawasiliano katika eneo la Kidahwe mkoani Kigoma.
……………………………………………………………..
Makandarasi wanaojenga barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 na Kibondo-Nyakanazi Km 50 wametakiwa kukamilisha ujenzi huo mwezi Mei mwakani badala ya Novemba ili kuharakisha mkakati wa Serikali wa kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo uliyogawanywa sehemu mbili, Kidahwe-Kasulu inayojengwa na China Railway 50 Group na Kibondo-Nyakanazi inayojengwa na Nyanza Road Works.
Prof. Mbarawa amewataka makandarasi hao kuongeza kasi ya ujenzi, vifaa na  wafanyakazi wenye sifa ili barabara hizo zikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Tutahakikisha ifikapo Juni mwaka huu tutakuwa tumelipa madeni yote mnayoidai Serikali hivyo fanyeni kazi kwa uhakika kwa kuwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano tayari tumeshawalipa makandarasi zaidi ya shilingi bilioni 725”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza kwamba nia ya Serikali ni kuifungua mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa kwa barabara za lami ili kufungua ukanda wa magharibi mwa nchi kibiashara kutokana na ukanda huo kuwa sehemu muhimu ya nchi katika uzalishaji na kiungo kikuu kwa nchi za Congo DRC, Burundi na Rwanda.
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), kulinda miundombinu ya reli na kujiepusha na vitendo vya hujuma ili kuliwezesha shirika hilo kupata shehena kubwa ya mzigo kufuatia wadau mbalimbali kuonesha nia ya kusafirisha mizigo kwa njia ya reli.
“Serikali imewekeza vya kutosha katika Shirika la Reli hivyo mfanye kazi kibiashara ili mpate mzigo mkubwa wa kusafirisha”, amesisitiza Prof. Mbarawa
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Kigoma na taasisi zilizo chini ya wizara yake Prof. Mbarawa amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuzuia uvamizi na uhujumu wa miundombinu ya barabara, reli, na mkongo wa taifa wa mawasiliano na wote watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua za haraka na za kisheria.
Prof. Mbarawa ametoa wiki moja kwa taasisi zilizo chini ya wizara yake kuhakiki wafanyakazi ili kubaini kama kuna wafanyakazi hewa.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa mkoa wa Kigoma umejipanga vizuri katika kudhibiti uvamizi wa miundombinu ya barabara na wale waliojenga ndani ya mita 22 kwenye barabara kuu wataondolewa maramoja bila kulipwa fidia.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya kukagua miundombinu katika mikoa ya kanda ya magharibi ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa uiboreshaji wa miundombinu ya kanda hiyo ili kuiwezesha kufanya biashara kiurahisi na mikoa mingine ya Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Post a Comment