Thursday, March 24, 2016

UZINDUZI WA MRADI WA USAID WA UIMARISHAJI MIFUMO YA SEKTA ZA UMMA WAFANYIKA MKOANI DODOMA

RC wa Dodoma, Jordan Rugimbana, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa PS3
RC wa Dodoma Jordan Rugibana akiteta na Mkuturenzi wa Mradi wa PS3, Dk. Emmanuel Malangalila, wakati wa uzinduzi
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Dodoma wakifuatilia mada wakati wa uzinduzi wa Mradi wa PS3 mkoani humo.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia majadiliano wakati wa uzinduzi wa mradi wa PS3 mkoani Dodoma
Dk. Conrad Mbuya wa PS3 akitoa mada wakati wa uzinduzi wa mradi mkoani Dodoma.
Mkurugenzi wa Mradi wa PS3, Dk. Emmanuel Malangalila, akitoa mada kwenye uzunduzi wa mradi wa PS3 mkoani Dodoma
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi) akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa PS3
Matiko Machonchoryo wa PS3 akitoa mada wakati wa uzinduzi wa mradi wa PS3 mkoani Dodoma
***************
Uzinduzi
wa kimkoa wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), umefanyika mjini Dodoma siku ya Jumanne na Jumatano, Machi 22-23, 2016. 
Mradi huo ujulikanao kwa Kiingereza kama Public Sector Systems Strengthening (PS3) ni wa miaka mitano, na utafanya kazi na Serikali Kuu pamoja na Halmashauri 97 katika mikoa 13 ya Tanzania bara.
PS3 inalenga kuunda ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya sekta za umma yakiwemo masuala ya utawala bora, rasilimali watu, fedha, utoaji wa taarifa, na tafiti tendaji.  Ushirkiano huu wa PS3 katika ngazi ya Serikali kuu na  Halmashauri, una nia ya kukuza utoaji, ubora, na matumizi ya huduma za umma, hususan kwa jamii ambazo hazijanufaika vya kutosha.
 
Katika uzinduzi huo, mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, na uzinduzi ulihudhuriwa pia na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Dodoma ambaye amehamishiwa mkoa wa
Songwe, Chiku Galawa.  Watu takribani 180 walihudhuria.  Washiriki wa uzinduzi huo walikuwa ni: Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Wakuu wa Wilaya za Dodoma, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa, na Wajumbe  wa Timu ya Mejenimenti kutoka kwenye
Halmashauri. 
Mkoa wa Dodoma una Halmashauri  nane, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, na Halmashauri
ya Mji wa Kondoa.
PS3 ni mradi wa miaka mitano ambao umeandaliwa na USAID kwa kushirikiana na
Serikali ya Tanzania, na unafadhiliwa na USAID.  Unatekelezwa na mashirika saba yakiwepo ya kitaifa na kimataifa, ambayo
ni:  Abt Associates Inc., kama mtekelezaji mkuu, na watekelezaji wasaidizi ambao ni Taasisi ya Benjamin Mkapa
(BMF), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Mafunzi ya Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI), Taasisi ya Ushauri Tanzania (TMA), Broad Branch Institute, Intra Health International, na Urban Institute.
Mikoa 13 ya Tanzania Bara ambako mradi utatekelezwa ni: Iringa, Dodoma, Kagera, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Rukwa, na Shinyanga.
PS3 itaimarisha mifumo katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Halmashauri. Mradi utahakikisha mifumo iliyopo katika ngazi ya Halmashauri inaimarishwa kupitia kitita cha afua zilizoundwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi wa Tanzania.  Mafanikio yanayotarajiwa ni pamoja na:
·   Utawala Bora na Ushirikishwaji wa Raia: Uimarishaji wa utawala katika ngazi ya kitaifa na ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kuweza kutumia rasilimali kwa uwazi, kuwezesha ushiriki wa wananchi katika kupanga, kufuatilia, na kutoa matokeo katika kila sekta.
·   Rasilimali  Watu: Kuongezeka kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwenye maeneo yenye uhitaji zaidi.  Kuimarisha mfumo wa ajira pamoja na kudumu kwa watumishi katika ajira serikalini.
·   Fedha: Ongezeko la pato la ndani kwa ajili ya huduma za umma, kuongeza ufanisi  katika matumizi ya fedha za umma, na pia kuongeza uwiano kati ya kiasi cha fedha kilichotumika na mali iliyonunuliwa.
·   Mifumo ya Mawasiliano: Kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa iliyopo nchini, pamoja na matumizi ya takwimu kwa wadau.
Utafiti Tendaji: Tafiti Tendaji muhimu zitakazosaidia mradi kujua changamoto na mikakati ya kuzishughulikia changamoto hizo. Tafiti hizi zitasaidia kugundua fursa zilizopo na kuzitumia kuweza kupata matokeo yanayotarajiwa.  Pia tafiti hizo zitasaidia kuboresha maamuzi serikalini.              

No comments: