Monday, March 07, 2016

SPIKA WA BUNGE LA EALA AZIASA NCHI WANACHAMA KUTUMIA KISWAHILI KATIKA KUFANYA KAZI NDANI YA JUMUIYA.


Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Mhe. Daniel Kidega (kulia) akitoa taarifa ya Jumuiya hiyo mbele ya ya Wabunge wa Mabunge ya Afrika Mashariki leo Jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu Jumuiya hiyo. Kushoto ni Mbunge wa Bungo hilo Mhe. Makongoro Nyerere.
Baadhi ya Wabunge wa Mabunge ya Afrika Mashariki pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wakati akisoma taarifa yake leo Jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu Jumuiya hiyo.
(Picha zote na Benedict Liwenga)

Na. Benedict Liwenga.

NCHI wanachama wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameaswa kuenzi lugha ya Kiswahili na kuifanya kuwa lugha ya kufanyia kazi katika Jumuiya hiyo.


Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Daniel Kidega alipofanya Mkutano uliowahusishwa Wabunge wa Mabunge ya Afrika Mashariki (EALA) lengo likiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Jumuiya hiyo.


Mhe. Kidega ameeleza kuwa, lugha ya Kiswahili ina umuhimu mkubwa kwa Jumuiya hiyo ambapo ameshauri kuwa kuna haja ya kupitia katika Sheria ya Bunge hilo ili kuhakikisha kuwa Kiswahili na Kiingereza vinatumika ama kuzungumzwa kila mahali katika Afrika Mashariki.


‘’Tupate muda wa kutumia Kiswahili na kuhakikisha kuwa Kiswahili kinazungumzwa katika nchi zote za Afrika Mashariki kwani ni lugha ya Afrika na sisi ni Waafrika, hivyo tutafute namna ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufanya kazi kwa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki,’’ alisema Kidega.


Aidha, Spika Kidega amegusia suala la watu wenye ualibino ambapo ameeleza kuwa, nchi wanachama hazinabudi kupiga vita masuala ya ukatili kwa watu wenye ualbino ambapo amezitaka Serikali wanachama wa Jumuiya hiyo kuhakikisha kuwa Albino wanaheshimika kama binadamu wengine na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wanaojihusisha na ukatili dhidi ya watu hao, kwani kwa kufanya hivyo kwa pamoja kutapunguza ama kuondosa changamoto zinazowakabili watu wenye ualbino.


Mhe. Kidega hakusita kuwapongeza Wabunge wanachama wa EALA waliohudhuria Semina ya Siku mbili (3 Machi- 4, 2016) iliyolenga kujadili masuala ya changamoto za uchaguzi kwa nchi za Afrika Mashariki ambapo waliweza kujadili kwa undani baadhi ya changamoto za uchaguzi na madhimio mbalimbali yenye kuleta maendeleo katika Jumuiya hiyo.


Kwa upande mwingine, Mhe. Kidega amewaasa Wazanzibar ambao hivi karibuni wanaenda kupiga kura na kuwataka kufanya uchaguzi huo kwa uhuru na haki ikiwemo kudumisha amani ya Kisiwani humo pamoja na Tanzania kwa ujumla.


‘’Niwaombe Wazanzibar ambao mda si mrefu mnaenda kurudia uchaguzi wenu, tiini sheria za nchi, jitokezeni kupiga kura kwa wingi na hakikisheni kuwa mnafanya uchaguzi wenu kwa uhuru na haki ili kudumisha amani ya Tanzania, alisema Kidega.


Mhe. Kidega pia amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ambayo inabadilisha sura ya Tanzania pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kujituma kwao katika kuwatumikia watanzania wote.
Post a Comment