Thursday, March 10, 2016

WATANZANIA WAMEASWA KUWA NA TABIA KUWEKEA AKIBA BENKI.

Na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma
Watanzania wameaswa kujenga tabia ya kujiwekea akiba kupitia mabenki kwa manufaa yao na taifa kwa kwa ujumla ikiwa ni mchango wao katika kutekeleza kaulimbiu ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ili kufikia malengo waliojiwekea katika kujiletea maendeleo endelevu.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Fedha na Utawala kutoka Bodi ya Bima na Amana (DIB) iliyo chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Richard Malisa wakati akitoa mada juu ya bodi hiyo katika semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi hao katika kuandika, kutoa na kusambaza habari za sekta ya uchumi biashara na fedha.
“Pesa zinapowekwa na kuwa benki hutumika kuchangia kuinua na kuimarisha usalama wa akiba ya mtu binafsi na kwa upande wa nchi zinatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuinua sekta ya elimu, afya, maji,  ujenzi wa barabara na kilimo” alisema Malisa.
Katika kuonesha umuhimu wa bodi hiyo nchini, Malisa alisema kuwa taasisi ama mtu binafsi anapoweka pesa zake benki, hiyo ni amana kubwa na muhimu kwa kuwa tabia hiyo ya uwekaji pesa ina tija na inaongeza usalama wa pesa ambayo ni njia salama ikilinganishwa na kutumia njia za zamani za watu kuweka pesa kwenye godoro ambayo sio salama.
Faida nyingine za mtu binafsi ama taasisi kuweka pesa zao benki ni kuongeza mtaji wake kwa kupata riba kulingana na muda pesa hizo zinapokuwa benki na mteja anauhakika pesa yake ipo salama kwa kuwa ipo mikononi mwa Bodi ya Bima na Amana endapo litatokea tatizo lolote kwenye benki alipoweka pesa zake.
Katika kufanikisha na kutekeleza majukumu yake, DIB inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa mtu mmoja mmoja katika masuala ya kibenki na fedha kwa undani wake ili aweze kufanya maamuzi yatakayomfanya awe bora zaidi kiuchumi ikilinganishwa na hapo awali kabla ya kufahamu masuala ya kibenki na fedha ikiwemo kuongeza nidhamu ya matumizi.
Akitolea mfano Malisa amewaasa Watanzania wawe makini wanapochukua mikopo ambapo alisema kuwa watu wasikope kwa kufuata mkumbo ama kwa shinikizo fulani, bali wakepo kwa lengo la kuwekeza ili kuinua hali zao za kiuchumi katika maisha.
Hadi kufikia Juni 30, 2015 Bodi ya Bima na Amana ina akiba ya jumla ya kiasi cha Sh. biloni 220.5 ikilinganishwa na wakati ilipokuwa inaanzishwa na Serikali mwaka 1994 ambapo kianzio kilikuwa kiasi cha Sh. bilioni 1.5.
Aidha, katika semina hiyo Bw. Bernard Dadi kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa alisema kuwa BoT itaendelea kuboresha mifumo ya malipo ya hundi, kielektroniki ili kuongeza ufanisi kwenye mifumo hiyo, kuongeza usalama, kuongeza njia mbalimbali za malipo ili kupunguza malipo kwa fedha taslimu na kuongeza kasi ya malipo yaweze kuwa ya wakati kwa wateja popote walipo ndani na nje ya nchi.
Ili kuendana na wakati BoT kupitia Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa katika kuwahudumia wananchi katika masuala ya fedha na mabenki, imeanza kutumia mfumo wa TACH unaohusisha malipo ya hundi na malipo madogo ya kielektroniki (EFT) ambao umeanza kutumika tarehe 30 Aprili 2015 nchini.
Mfumo wa TACH unatumika na mabenki kutuma na kupokea hundi za wateja wao ikiwemo kulipa malipo madogo madogo yaliyojumishwa pamoja, mishahara, pension na hata malipo ya mtu mmoja mmoja.
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa TACH nchini, awali hundi zilikua  na muda tofauti wa siku za kuhakiki kulingana na kanda hali iliyopelekea muda wa siku za kuhakiki  za hundi ulikua ni siku 3, 7 na 14 kutegemeana na kanda.
Baada ya kuanzishwa mfumo wa TACH hali imekuwa tofauti ambapo kwa mfumo  huo sasa, hundi zote za Tanzania popote zitakapowasilishwa zitakuwa zinafanyiwa kazi ndani ya siku moja ya kuzihakiki hundi  hizo (T+1) mpaka hapo itakapolipwa.
Hatua hiyo imewapunguzia muda wateja ili waweze watapata hela zao mapema na hivyo kuzitumia kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Bw. Dadi aliongeza kuwa nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zenyewe zinatumia unaojulikana kama EAPS ikiwa ni jitihada za kuunda umoja  wa kiuchumi miongoni mwa nchi hizo.
Mfumo huo wa malipo umeunganisha mifumo ya malipo (RTGS) ya nchi washiriki wa Afrika Mashariki ili kurahisisha malipo kati ya nchi washirika.
Kwa maana hiyo mabenki ya kibiashara ya nchi husika zina uwezo wa kutumiana na kupokea pesa za wateja wao kwa kutumia sarafu za nchi wanachama kufanya muamala.
Hadi sasa, mfumo huo umeunganishwa kwa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, wakati Burundi na Sudan ya Kusini wako mbioni kujiunga.
Post a Comment