Saturday, October 10, 2015

KAYUMBA JUMA MSHINDI WA BONGO STAR SEARCH 2015

 
Mshindi wa Bongo Star Search 2015 Kayumba Juma hatua ya fainali Top 2. 
TOP 2 ni Kayumba Juma Jukwaani  mshindi aliyejinyakulia kitita cha Mil 50.
 Kwenye Stage ya Bongo Star Search 2015 ni Msanii kutoka Nigeria RUNTOWN
 Msanii kutoka nchini Nigeria Run town akiwajibika jukwaani
 Kutoka Top 2 Jukwaani ni Nasibu Fonabo
Kayumba Juma wa jijini Dar es Salaam jana usiku aliibuka mshindi wa shindano la kusaka vipaji vya muziki la Bongo Star Search (BSS) kwa mwaka 2015 baada ya kuwabwaga washiriki wengine watano waliofika hatua ya fainali, hivyo kutwaa kitita cha Sh50 milioni. Mbali na kuondoka na fedha hizo, kijana huyo amepewa bima ya afya ya mwaka mzima kutoka kwa kampuni ya Jubilee Insurance.
Juma aliibuka kidedea katika fainali hizo zilizofanyika katika Ukumbi wa King Solomon Hall, Kinondoni jijini Dar es Salaam zilizopambwa na wasanii mbalimbali wa muziki.
Mshindi huyo aliwabwaga washiriki wengine watano ambao walifika hatua ya fainali; Frida Amani, Nassib Fonabo, Jacqueline Kayengi, Angel Mary Kato na Kevin Gerson. Licha ya kushindwa kutwaa taji hilo washiriki hao watano walitoa ushindani mkubwa na kuwapa burudani mashabiki waliohudhuria kwenye ukumbi huo.
Sambamba na burudani kutoka kwa washiriki hao, pia wapo baadhi ya wasanii waliolipamba jukwaa la fainali hizo ikiwa ni pamoja na Kala Jeremiah, Peter Msechu, Christian bella, Yamato Band pamoja na msanii kutoka Nigeria, Runtown.
Jaji kiongozi wa mashindano hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark, Rita Poulsen alimtangaza mshindi huyo baada ya washiriki wote sita kuchuana jukwaani na kubaki wawili.
Baada ya wawili hao, Kayumba Juma akiwakilisha Dar es salam na Nassib Fonabo kutoka Arusha ambao waliingia katika hatua ya mbili bora na kutupa karata yao ya mwisho kwa kuimba muziki wa mwisho, mashabiki walipiga kura na muda mfupi baadae Jaji huyo maarufu kwa jina la Madam Rita alipanda jukwaani na kumtangaza mshindi.
“Mnamjua mshindi…? Sina maneno mengi maana kazi yangu ni kumtangaza mshindi wa mashindano ya BSS msimu wa 8 (season eight), mshindi ni.. ni.. Kayumba Juma’’ alitangaza Madam Ritah huku mashabiki wakishangilia kutokana na burudani aliyotoa mshindi huyo. Mashindano hayo yanayoandaliwa na Kampuni ya Benchmark Production 360 yalianza mwaka 2006 kwa kusaka vipaji vya vijana wa Kitanzania kila mwaka lakini mwaka jana mashindano hayo hayakufanyika tofauti na ilivyozoeleka.
Baadhi ya washindi wa BSS kwa miaka tofauti toka shindano lianzishwe ni pamoja na; Jumanne Iddi, Kala Jeremiah, Peter Msechu, Walter Chilambo na Emmanuel Msuya.

No comments: